Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Utii wa sheria bila kushurutishwa utatekelezeka polisi wakibadilika

15th April 2012
Print
Comments
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema

Katika makala yangu ya Jumapili wiki iliyopita kwenye safu hii, nilijadili kwa uchache mambo ambayo nimeona kuwa ni kikwazo kinachokwaza mafanikio ya dhana ya 'Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi' iliyobuniwa na ambayo imekuwa ikisisitizwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema.

Mambo hayo ni pamoja na baadhi ya askari polisi kushirikiana na wahalifu, kuficha wahalifu na kutoa siri za taarifa za uhalifu.

Wasomaji wengi waliunga mkono hoja yangu hiyo kupitia simu walizonipigia na ujumbe mfupi wa simu za mikononi (sms) walioniandikia.

Lakini yupo msomaji aliyehoji kama nina ushahidi wa wazi unaohusu askari polisi kushirikiana na wahalifu.

“Una ushahidi wa wazi wa askari kushirikiana na wahalifu au ni hisia na stori za vijiweni?” alihoji.

Kwanza, lazima nikiri kwamba nafasi katika safu hii haitoshi kueleza kila kitu. Ndio maana ushahidi unaohojiwa na msomaji huyo haukuweza kutajwa.

Hata hivyo, upo ushahidi mwingi tu wa wazi kuhusu baadhi ya askari polisi kushirikiana na wahalifu.

Hatua iliyochukuliwa na Jeshi la Polisi hivi karibuni ya kumvua madaraka ya Ukuu wa Polisi Wilaya (u-OCD) ya Serengeti, mkoani Mara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Paulo Mng’ong’o, ni ushahidi tosha kuhusu ukweli huo.

'OCD' Mng'ong'o na watuhumiwa wengine saba, akiwamo Afisa Usalama wa Taifa Wilaya hiyo, Said Mussa, na dereva wa gari la polisi, Koplo Phillimatus, walikamatwa na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani humo, ambako waliingia bila kuitaarifu mamlaka husika, na kuchimba madini.

Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Robert Boaz, Machi 27, mwaka huu.

Hivyo, pengine ningechukua fursa hii kumkumbusha msomaji huyo kuwa hoja yangu kuhusu baadhi ya askari polisi kushirikiana na wahalifu haikuwa stori za vijiweni.

Pengine ningemkumbusha pia kwamba yanapoelezwa mambo kama hayo, nia huwa si kushindana au kubishana. Pia haimaanishi kwamba katika dunia hii yupo mtu asiyekuwa na dhambi. La hasha!

Ukweli ulio dhahiri ni kwamba, hakuna aliye mkamilifu isipokuwa Mwenyezi Mungu Muumba peke yake. Hiyo ina maana kwamba kila binadamu ni mkosaji. Lakini aliyebora ni yule tu anayetubu na kuacha kutenda makosa.

Ni wajibu kwa waungwana kurekebishana, kusahihishana, kuelekezana na kuongozana njia iliyo sawa.

Ndio maana hata Jeshi la Polisi limekuwa likitumia fursa lilizonazo kuelimisha jamii. Haliishii hapo tu. Lakini pia hukamata na kuwafikisha mahakamani wanaotuhumiwa kwa uhalifu, wakiwamo wafanyabiashara, wanasiasa, waandishi wa habari nakadhalika. Nia ikiwa ni ileile. Kurekebishana na kuwekana sawa.

Katika kuwekana sawa, ipo kampeni ya “Utii wa Sheria bila Kushurutishwa”. Kampeni hiyo imebuniwa na jeshi hilo ili kuiwezesha jamii kutambua umuhimu wa utii wa sheria za nchi na taratibu za jamii bila shuruti.

Ni kampeni nzuri. Iwapo itafanikiwa itasaidia kupunguza uhalifu. Pia itapunguza gharama katika operesheni za kupambana na uhalifu, msongamano wa kesi mahakamani na idadi ya mahabusu na wafungwa katika vituo vya polisi na magerezani.

Hata hivyo, nionavyo kampeni hiyo inaweza kufanikiwa iwapo tu polisi wenyewe watakuwa wa kwanza kubadilika.

Inavyoonekena, askari polisi wengi ama hawajafundishwa au hawatumii ujuzi wao wa kukamata watuhumiwa bila kushurutishwa.

Kwa mfano, mara nyingi imeshuhudiwa, pamoja na kutii amri ya kupanda karandinga la polisi, mtuhumiwa amekuwa akisindikizwa na kipigo cha virungu hadi anaingia ndani ya gari la polisi.

Hali kama hiyo haidhaniwi kama inaweza kujenga mazingira ya kuwafanya wananchi watii sheria bila kushurutishwa.

Ukweli ni kwamba, watatii sheria pale tu watakapokuwa wakimuona askari.

Polisi wana wajibu wa kuelimisha watu, kwani elimu ya utii wa sheria haijafika vizuri kwa jamii.

Watu hawajaandaliwa kutii sheria bila kushurutishwa. Wamezoea kwamba hata ikitokea wao kutii, polisi hutumia nguvu hata kama wanatii.

Ili kampeni ya utii wa sheria bila shuruti iweze kuleta mafanikio ya kweli, lazima kwanza wananchi, wakiwamo polisi wenyewe waanzie kusomea hilo, kuanzia shule ya msingi. pia polisi watoe elimu ya namna ya kuwa na mwenendo na tabia ya watu kutii sheria bila kushurutishwa. Vinginevyo wananchi wataendelea kuwa na nidhamu ya woga.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles