Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kaseja nahodha mpya Stars

24th May 2012
Print
Comments
Kipa chaguo la kwanza wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Juma Kaseja

Kipa chaguo la kwanza wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Juma Kaseja, juzi usiku aliteuliwa kuwa nahodha mpya wa timu ya taifa (Taifa Stars) ambayo inajiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Malawi ambayo itafanyika keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kaseja pia ndiye nahodha wa Simba ambaye msimu uliomalizika alisimama langoni katika mechi zote za ligi na mechi sita za kimataifa za Kombe la Shirikisho ambazo timu yake ilicheza.

Nafasi hiyo awali ilikuwa inashikiliwa na beki Shadrack Nsajigwa wa Yanga ambaye safari hii ameachwa nje ya kikosi kama msaidizi wake, Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka katika kambi ya timu hiyo, Aggrey Morris wa Azam ameteuliwa kuwa nahodha msaidizi wa kikosi hicho ambacho Juni 2 kitaikabili Ivory Coast jijini Abdijan katika mchezo wa kwanza wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zitakazochezwa nchini Brazil.

"Jana (juzi) usiku benchi la ufundi tulikutana na kumteua Kaseja kuna nahodha mpya, awali Nditi (Shabani wa Mtibwa Sugar) alionekana pia anaweza kupewa cheo hicho lakini kutokana na upole wake ndio maana tukashindwa kumpa jukumu hilo," kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa maamuzi ya kumpa Kaseja hayakupingwa sana licha ya yeye kukaa langoni lakini uzoefu wa kucheza mechi nyingi za kimataifa na kuwakumbusha wenzake mara kwa mara ndio yaliyofanya apewe jukumu hilo.

Jana asubuhi kiungo wa timu hiyo, Nurdin Bakari, alianza rasmi matibabu ya nyama za paja kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutokana na maumivu aliyonayo na imethibitishwa na daktari kwamba hataweza kucheza mechi ya Jumamosi.

Kiungo huyo anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi kesho kwa sababu yuko katika programu ya kocha katika mechi dhidi ya Ivory Coast.

Stars iliyokuwa inajifua kwenye uwanja wa Karume, jana jioni ilianza kufanya mazoezi yake katika uwanja wa Taifa ambao ndio utatumika Jumamosi.

Wapinzani wa Stars, Malawi ambayo wiki ijayo itakuwa jijini Kampala kuivaa timu ya taifa ya Uganda (Cranes) inatarajiwa kuwasili nchini leo ikiwa na nyota wake 20.

 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles