


.jpg)
Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimeshtukia njama zinazofanywa na baadhi ya watu kutaka kuvuruga mgomo wa walimu nchi nzima kwa kuanza kueneza propaganda kuwa una mkono wa chama kimoja cha siasa.
Rais wa CWT, Gratian Mukoba, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Slaam, alisema upo mkakati unaofanywa na wadau wa mgogoro huu ili kuhakikisha kuwa walimu hawagomi hata kama wametimiza matakwa ya kisheria.
Alisema mkakati huo ni pamoja na kuwarubuni wananchi kuwa mgogoro wa walimu unachochewa na wanasiasa kwa kuratibiwa na chama fulani cha siasa wakati siyo kweli.
Mukoba alisema lengo kubwa la mkakati huo ni kuwachonganisha walimu na viongozi wao na jamii ili wahame kwenye ajenda yao ya kudai maslahi yao na waone kuwa mgogoro huu ni maslahi ya viongozi wa CWT na siyo kwa maslahi ya wanachama.
Alisema mkakati mwingine uliopangwa ni kuwatisha walimu kwa kuwatumia Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Elimu wa mikoa na wilaya, Walimu Wakuu, Wakuu wa Vyuo na Waratibu Elimu kata.
“Wadau wa mgomo wamefanya utafiti wao na kubaini kuwa walimu ni waoga sana wakitishwa tu wataachana na kudai maslahi yao, kwa hivyo wanawatumia viongozi kutoa vitisho kwa walimu kwamba wakigoma watafukuzwa kazi,” alisema Mukoba.
Alisema chama kinapenda kuwaeleza wananchama wake pamoja na jamii kwa ujumla kuwa walimu walitangaza mgogoro wa kimaslahi na mwajiri wao chini ya kifungu cha 80 (1) cha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004.
Aliongeza kuwa mgogoro huo namba CMA/DSM.ILA/369/12 ulisajiliwa Juni 8 mwaka huu na kwasasa uko kwenye hatua ya usuluhishi na kwamba muda wa usuluhishi utakapokwisha bila kuafikiana walimu watalazimika kugoma nchi nzima.