



Tanzania ina upungufu wa marubani na wahandisi kwa asilimia 60 kutokana na serikali kujitoa katika mpango wa ufadhili wa kuwasomesha ambapo kwa sasa kuna marubani asilimia 40 wa kutoka nchini na asilimia 60 wanaotoka nje.
Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Fadhili Manongi alisema jana kuwa awali serikali ilikuwa inatoa ufadhili kwa ajili ya kuwasomesha wahandisi na marubani nchini Ujerumani, lakini kutokana na mabadiliko ya sera, imejitoa katika mpango huo.
“Awali serikali ilikuwa ikichagua watu wenye uwezo na kipaji cha urubani na uhandisi kisha kuwafadhili masomo yao, kinachofanyika sasa wazazi wenye uwezo wanawasomesha watoto wao wenyewe bila kuangalia vipaji na uwezo, lakini hii inaleta shida kwa sababu wengi wanaohitimu masomo hayo hawakidhi viwango vya mtu kuwa rubani au mhandisi jambo linalosababisha matatizo hususan ajali,” alisema Manongi.
Alisema ili kuondokana na tatizo hilo mamlaka hiyo imeanzisha utaratibu mpya ambao kila mwendeshaji anatakiwa kuchangia katika mchango wa kuwasomesha marubani na wahandisi na kwamba michango hiyo itakapofikia lengo, watawapeleka wahandisi 10 na marubani 10 kusoma na kuongezewa uwezo zaidi ili waweze kuwa wakaguzi pia.
“Kwa sasa tuna wakaguzi 13, lakini alengo letu ni kuwa nao 18, tumepeleka marubani watatu kwa ajili ya kupata kozi ya ukaguzi ili wawe na uweze wa kuwa wakaguzi na marubani kwa swababu kuwa marubani peke yake haitoshi, na gharama ya hao watatu ni Shilingi milioni 300 ambapo kozi yao itakuwa si chini ya miezi sita,” alisema Manongi.