Friday Apr 29, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Uuzaji wa nyumba za serikali unakumbusha umma machungu

27th March 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Juzi Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, aliwakumbusha Watanzania juu ya machungu ya uporaji wa mali ya umma uliofanywa kwa baraka za serikali ya awamu ya tatu, huu ni ‘wizi’ wa mchana kweupe wa kuuza nyumba za watumishi wa serikali kwa kisingizo ambacho hadi leo bado hakijaeleweka kwa wengi.

Nyumba hizo nyingi zikiwa katika maeneo nyeti ziliuzwa kwa bei ya kutupa baada ya kujengwa hoja kwamba watumishi wa serikali hawana kipato kikubwa kwa maana hiyo wauziwe kwa bei ya chini bila kujali thamani halisi ya kibiashara ya maeneo ambayo nyumba hizo zilikuwa.

Nyingi kati ya nyumba hizo zilikuwa meneo nyeti na yenye thamani kubwa kibiashara kulingana na bei ya viwanja katika maeneo ya mijini, tangu kuuzwa kwake kati ya 2000-2005, kwa masharti ya kutokuzikodisha, wengi wamezigeuza kuwa vitegauchumi vikubwa kwa kuzibomoa na kujenga upya, ilahali wengine wakiendelea kusuasua katika kulipia nyumba hizo walizouziwa kwa mfumo wa kulipa kidogo kidogo.

Ni kutokana na kusuasua huko, Waziri Magufuli juzi aliuagiza uongozi wa Wakala Wa Majengo Tanzania (TBA), kuwapa siku saba watu wote walionunua nyumba hizo na kushindwa kulipa kwa mujibu wa mikataba wawe wamelipa deni lote vingenvyo watanyang’anywa.

Mbali Waziri Magufuli kwenda mbali zaidi akiutaka wakala huo kuwaandikia barua watu hao na kuwataka walipe fedha hizo ndani ya wiki moja, vingimevyo watanyanganywa, alionyesha kukerwa nah ali hiyo kwani inachelewesha malengo ya TBA kujenga nyumba zaidi.

Alitoa mfano wa mkoa wa Morogoro kuwa kati ya waliouziwa nyumba hizo, asilimia 54 wamelipa wakati asilimia 45 hadi sasa hawajalipa hali aliyoeleza kuwa imefanya wakala huo kushindwa kufikia malengo ya kujenga nyumba 10,000 za watumishi wa Serikali nchini kote, badala yake zimejengwa nyumba 1,043 tu hadi sasa, huku mkoani Morogoro wakijenga nyumba moja tu tena wilayani Mvomero.

Itakumbukwa kwamba pamoja na nia ya serikali ya kuuza nyumba hizo kwa watumishi wake kuwa ni kuwasaidia kupata makazi bora, pia ilitaka ipate fedha za kujenga na kuuza nyumba nyingine, kwa hali hiyo kushindwa kulipia madeni hayo, waliouziwa sasa wanahesabika kuwa kikwazo katika utekelezaji wa malengo hayo.

Tunasikitika kwamba hadi leo takribani miaka 12 tangu kuanza kwa mchakato wa kuuza nyumba za serikali tena kwa bei ya kutupa bado wapo watu wanaoidaiwa madeni hayo na kwa maana hiyo kukwamisha mipango ya serikali ya kujenga nyumba zaidi, hivyo kuikwaza katika kuwapa watuishi wake makazi bora; tunaamini kuendelea kuwa na madeni haya si kitu kingine chochote ila ni mwendelezo wa mzaha katika kutokuthamini mali ya umma.

Pamoja na kwamba hatujawahi kuunga mkono uuzaji wa nyumba hizo, na tukiendelea kushikilia msimamo kwamba uamuzi wa kuuza nyumba hizo hakika haukuwa sahihi hasa kutokana na kujengeka kwa hali ya kupendeleana ndani ya mfumo wa serikali; lakini pia ikijulikana wazi kwamba wapo baadhi ya watu ambao nyumba zao zilitaifishwa miaka ya mwanzo wa sabini chini ya utelelezaji wa Azimio la Arisha, lakini hawakupewa fursa ya kuzinunua, waliopendelewa wanastahili kulipa kila senti kama walivyokubali kwenye mkataba wa kuuziwa nyumba hizo.

Hata hivyo, tunaendelea kutoa angalizo kwamba pamoja na waliouziwa nyumba hizi kuwajibika kulipa deni lao lote kwa wakati, maamuzi ya kuuza nyumba za serikali katika mfumo wa kibaguzi kama ulivyofanywa na serikali ya awamu ya tatu tena kwa bei ya kutupa, si kitu kinachostahili kutajwa kama moja ya mafanikio ya serikali yoyote inayoendesha mambo yake kwa haki na usawa.

Sisi tunafikiri kama serikali ilikuwa inataka kuwasaidia watumishi wake kupata makazi bora, basi njia sahihi ingelikuwa ni kuanzisha mfuko mahususi kwa kazi hiyo ili wakopeshwe kwa utaratibu ambao ungewanufaisha watumishi wote, wakubwa kwa wadogo, kuliko ilivyotokea kwa kunufaika wakubwa tu.

Tunaungana na Waziri Magufuli kwamba waliouziwa nyumba hizo wawajibike kuzilipia haraka iwezekano, tungependa pia ifahamike kuwa suala la uuzaji wa nyumba za serikali bado ni tete na kwa kweli ni moja ya madoa mabaya kabisa kuwahi kuikumba serikali ya awamu ya tatu, ni vema hali hii isije kujirudia tena katika uhai wa taifa hili. Tukatae kutapanya mali ya umma kwa kisingizio chochote kile.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles