


400 wapewa barua kurudi wizarani
Huduma Muhimbili bado shida.jpg)
Hali ya huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI), imezidi kuwa tete kutokana na madaktari kuendelea na mgomo, huku madaktari walio katika mafunzo wakifungasha mizigo yao na kuondoka.
Madaktari hao walianza kufungasha mizigo yao na kuondoka ikiwa ni siku moja baada ya juzi madaktari bingwa nao kutangaza kuanza rasmi mgomo.
NIPASHE ilitembelea hospitalini hapo na kushuhudia baadhi ya madaktari wakiwa wamefungasha mizigo yao na kuondoka eneo la hospitali hiyo, huku kukiwa na hali isiyokuwa ya kawaida ambapo idadi ya wagonjwa waliofika kupata matibabu ilikuwa ndogo ikilinganishwa na siku zilizopita.
Katika baadhi ya wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwemo ya Mwaisela ambayo mara nyingi hujaza wagonjwa, vitanda vilikuwa tupu.
Hellen Mjema, ndugu wa mgonjwa aliyelazwa katika moja ya wodi jengo la Mwaisela, alisema tangu mgomo wa madaktari uanze wiki iliyopita, mgonjwa wake amekuwa akipata matibabu katika hali ya kusuasua kutokana na madaktari kupita kwa nadra.
Kwa mujibu wa Mjema, mgonjwa wake anasumbuliwa na maradhi ya figo anatakiwa kufanyiwa operesheni, lakini tangu mgomo huo uanze hadi jana, alikuwa hajafahamu hatma yake.
Kiongozi wa madaktari bingwa, Dk. Catherine Mng'ong'o, alisema kuwa madaktari bingwa wote hawajahudhuria katika sehemu zao za kazi na hata waliofika kazini walisaini tu kitabu cha mahudhurio na kuondoka.
Alisema wamefikia hatua hiyo kutokana na makubaliano yao waliyofikiana juzi kwamba hawako tayari kufanya kazi bila kuwepo madaktari wanaofanya kazi chini yao.
400 WARUDISHWA WIZARANI
Kwa upande wake, Kiongozi wa madaktari kwa vitendo, Elisha Osati, alisema hadi kufikia jana, madaktari 400 wa vitendo (interns) nchini kote, walikuwa wamekabidhiwa barua za kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutokana na kukaidi amri ya kuacha mgomo.
Osati alisema pamoja ya madaktari hao kupewa barua za kurudi wizarani, bado hawajaenda kuripoti.
Alisema hatua hiyo inatokana na madaktari hao kusubiri kupata idadi kamili ya madaktari wenzao watakaofukuzwa ili wafike kwa pamoja.
WATAKIWA WIZARANI KESHOKUTWA
Wakati huo huo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imewataka madakari wote wa mafunzo kwa vitendo (Interns) waliopewa barua za kurejea wizarani, wafike wizarani hapo keshokutwa.
Taarifa hizo zilitolewa jana Kitengo cha Mwasiliano cha wizara hiyo, lakini haukuwekwa saini na yeyote.
MUHIMBILI WAZUNGUMZA
Wakati hayo yakitokea, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema huduma hospitalini hapo zimerejea katika hali yake ya kawaida katika baadhi ya vitengo.
Aligaesha alisema huduma katika vitengo vya Idara ya Tiba, Watoto, Magonjwa ya Nje, Magonjwa ya Afya ya Akili, Mazoezi ya Viungo zinaendelea kutolewa kama kawaida na madaktari wote jana walifika kutoa huduma.
Hata hivyo, alisema huduma katika vitengo vya Kurugenzi ya Tiba, Magongwa ya Dharura, Upasuaji, Tiba Shirikishi na Uuguzi, zimeendelea kutolewa kwa kiwango cha kati ambako wagonjwa wanaofika kutibiwa ni wachache huku idadi ya madaktari waliofika ikiwa ni ndogo.
"Huduma za upasuaji zinafanyika lakini si kama kabla ya mgomo, kwani wagonjwa ni wachache kwenye baadhi ya kliniki, wagonjwa wa upasuaji waliopo wodini wanaonwa ingawa ni wachache," alisema Aligaesha.
AMANA, MWANYAMALA WAANZA KUREJEA
Baadhi ya madaktari katika Hospitali za Mwananyamala na Amana jijini Dar es Salaam wamerejea kazini.
Kwa mujibu wa Katibu wa Hospitali ya Amana, Tunu Abdul, madaktari walio katika mafunzo hawajagoma na kwamba wanaendelea na kazi.
Abdul alisema shughuli za utoaji huduma hazijaathirika kwa kiwango kikubwa hospitalini hapo.
"Sisi tulijipanga kabla ya kuanza mgomo kwa kuwaandaa madaktari ambao wapo kwenye mafunzo ili watusaidie kutoa huduma," alisema.
Hata hivyo, uongozi wa Hospitali ya Amana umewaagiza madaktari wote ambao hawakuwepo kazini kuanzia Julai 25, mwaka huu, kuandika barua za kujieleza kwenda kwa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala na madaktari walioko kwenye mafunzo kwa vitendo, waandike barua kwenda kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana.
Kwa upande wake, Katibu wa Hospitali ya Mwananyamala, Edwin Bisakala, alisema madaktari wanaendelea na kazi kama kawaida huku wale walioko katika mafunzo kwa vitendo, wakiondolewa rasmi na kurejeshwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii baada ya kubainika kuwa walishiriki mgomo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa uongozi wa hopsitali hizo, hadi kufikia jana hakuna daktari aliyekuwa ameandika barua ya kuacha kazi kama Rais Jakaya Kikwete, alivyowataka wafanye hivyo badala ya kuendelea na mgomo.
KAMATI YA ULINZI DAR YAONYA
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, imefanya ziara katika hospitali za serikali za jijini humo na kutoa onyo kwa madaktari wanaowatisha wenzao wanaoendelea na kazi wakibainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama imefanya ziara katika hospitali tatu za Amana, Mwananyama na Temeke na kubaini kuwa asilimia kubwa ya madaktari wanaendelea na kazi kama kawaida.
Alisema katika Hospitali ya Amana kati ya madaktari 13 waliopo hospitalini hapo ni watano tu ambao hawajaripoti kazini, Mwananyamala ni wawili ambao hawapo kazini wakati madaktari bingwa wote wapo kazini kama kawaida isipokuwa mmoja tu wa Hospitali ya Amana.
Sadick alisema madaktari wasaidizi hawajashiriki mgomo na wamekuwa wakiendelea na kazi kama kawaida na kwamba madaktari wa mafunzo 66 waliosimamishwa na kurejeshwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wameanza kuomba warejee kazini, lakini kwa kuwa tayari wamepelekwa huko, wizara itaamua cha kufanya.
Alisema katika ziara hiyo, tatizo walilolibaini ni baadhi ya madaktari wachache wanaowatisha wenzao wanaoendelea na kazi na kuonya kwamba wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema daktari yeyote atakayetishwa na mwenzake ambaye amegoma, atoe taarifa kwake kupitia simu ya mkononi namba 0754 034224.
Kamanda Kova aliwataka wananchi waendelee kuwapeleka wagonjwa katika hospitali za Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa madaktari wengi wanaendelea na kazi kama kawaida.
KCMC WAOMBWA KUREJEA
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, amezidi kuwasihi madaktari kurejea kazini ili kuwasaidia Watanzania maskini ambao ndiyo wanaoathirika na mgomo huo kwa kiasi kikubwa.
Askofu Shao ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi iliyo chini ya Shirika la Msamaria Mwema (GSF), alisema kwa kiasi kikubwa mgomo huo umeathiri utoaji wa huduma kwenye hospitali hiyo.
“Tunasikitika sana hakukuwa na sababu ya mgomo, umeathiri wanyonge wengi wa Tanzania, wenye uwezo wa kifedha wao wana mahali pa kutibiwa, huyu mnyonge hajui la kufanya. Tunawaomba na tunahitaji msaada wao, wawe na huruma na kuwatendea haki wagonjwa kama wanavyodai haki,”
alisema Askofu Shao.
Alisema wakati wawakilishi wao wakiendelea na mazungumzo na serikali, ni vyema madaktari wengine wakaendelea na kazi ili kumsaidia Mtanzania wa kawaida.
Aliongeza kuwa, wameendelea kuwasihi madaktari wote kwa ujumla wakiwemo madaktari bingwa kuendelea na kazi katika mazingira magumu yaliyopo kwa sasa ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi ili pia wawape haki wagonjwa huku nao wakidai haki zao.
Kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete, kwamba anayeona hawezi kufanya kazi hadi alipwe mshahara wanaodai, ni vema akaacha kazi, alisema ni kweli hiyo inatokana na uwezo wake.
Askofu Shao alisema na hivyo ndivyo inavyoonekana hata kwa watumishi wengine wa umma kwani Tanzania siyo ya madaktari pekee bali kila mmoja ana haki ya kujenga taifa.
Hata hivyo, NIPASHE ilipofika hospitalini hapo, ilishuhudia hali ya utoaji wa huduma kwa wagojwa ikiwa bado tete kutokana na uchache wa madaktari.
JWTZ WATUA MBEYA
Madaktari sita kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ili kunusuru hali iliyopo baada ya madaktari waliogoma kutorudi kazini.
Ujio huo umefuatia ahadi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, aliyesema madaktari kutoka vikosi ya JWTZ vilivyopo mkoani hapa watapelekwa hospitalini hapo ili wasaidie kutoa huduma kwa wagonjwa.
Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Eliuter Samky, aliliambia NIPASHE jana kuwa, tayari madaktari sita kutoka JWTZ wamewasili hospitalini hapo na kuanza kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa.
Hata hivyo, Dk. Samky, alisema licha ya madaktari hao sita wa JWTZ kuripoti hospitalini hapo, lakini hawakidhi haja.
Kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Wazazi iliyopo eneo la Meta mjini hapa, Dk. Samky, alisema inaendelea kufanya kazi kama kawaida, ingawa idadi ya wagonjwa wanaokwenda hapo kupata huduma ni ndogo mno.
NIPASHE jana lilitembelea katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na kuona watu wakiingia na kutoka, lakini baadhi yao walidai hawakupata huduma.
Mmoja wa wagonjwa katika hospitali hiyo, Ezekia Jackson, anayesumbuliwa na maumivu kwenye viungo vya uzazi, alisema tangu afike hapo Jumapili iliyopita, hajapata huduma yoyote zaidi ya kitanda anacholalia.
“Nimefika hapa siku ya Jumapili kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mbarali ambako niliandikiwa rufaa ili niwahi huduma Jumatatu, lakini sijapata hata kidonge cha Panadol na huduma niliyoipata ni kitanda tu hiki nilicholalia, hata wauguzi wanakuja kuniona kwa nadra," alisema Jackson.
Imeandikwa na Ninaeli Masaki, Gwamaka Alipipi, Enles Mbegalo Fransisco Haule na Thobias Mwanakatwe, Dar; Salome Kitomari, Moshi na Nebart Msokwa, SJMC, Mbeya