Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Meya ataka mtoto akapimwe

3rd June 2012
Print
Comments
  Ni aliyezaliwa mama akiwa amesimama
Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa

Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa amemuagiza Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo kuchukua vipimo vya mtoto, Arafa Ahmada, aliyezaliwa wakati mama yake akiwa amesimama kufanyiwa vipimo.

Slaa aliyasema hayo wakati alipomtembelea mama huyo eneo la Majohe.

Mwanamke huyo anadaiwa alijifungua mtoto huyo akiwa amesimama.

Baada ya kumjulia hali Arafa, baba wa mtoto, Ahmada Yahaya, alimueleza Slaa kuwa mwanawe hajafanyiwa vipimo vya awali ili kujua kama amepata madhara wakati kichwa chake kilipogonga chini wakati anazaliwa.

Alisema baada ya mkewe, Kuruthumu Abdalah kujifungua kwa kusimama mtoto huyo aligonga kichwa chini na baada ya tukio hilo hakuna kilichoendelea na baada ya siku mbili aliruhusiwa kutoka hospitalini.

Yahaya alisema anachotaka ni kufahamu uhakika wa afya ya mwanawe kama alipata madhara yoyote kwa ajili ya kupata matibabu mapema.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Slaa alimuagiza Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala kuhakikisha mtoto huyo anapatiwa daktari wa watoto ili aweze kufanyiwa vipimo vya kitaalamu juu ya afya yake.

Hata hivyo, Slaa aliwashauri akina mama kwenda kliniki kwa wakati ili kutoa fursa ya kujifungua salama.

Alisema tukio hilo lililotokea katika Hospitali ya Amana ni la kitaalamu kwani inategemea mama huyo alifika katika wakati gani.

“Amana ni hospitali inayozalisha akina mama wengi na hili suala ni la kitaalamu zaidi na inategemea mama huyo alifika katika wakati gani kutokana na hali yake aliyokuwa nayo,” alisema Slaa.

Tukio hilo lilitokea Aprili 18, mwaka huu katika Hospitali ya Amana ya jijini Dar es Salaam ambapo mama huyo alifika hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa huduma ya uzazi hali ambayo inadaiwa wauguzi walimchelewesha kumpa huduma na kujikuta akijifungua huku akiwa amesimama ambapo kichanga hicho kiligonga kichwa chake sakafuni.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment