



Marehemu Patrick Mafisango ambaye alikuwa kiungo mahiri wa klabu ya Simba alitoa kauli yenye mwelekeo wa wosia wa mwisho maishani mwake siku 11 kabla ya kufariki dunia kwa ajali ya gari usiku wa Jumatano.
Akizungumza na Nipashe juzi jijini, kiungo nyota wa Yanga, Haruna Niyonzima, alibainisha kuwa marehemu alimuomba wabadilishane jezi baada ya mechi baina ya Simba na Yanga Mei 5 kwasababu 'uzi' wa Wekundu wa Msimbazi utakuwa ukumbusho wa Niyonzima juu yake.
Wachezaji hao wawili raia wa Rwanda walikuwa wakiishi kama ndugu nchini.
Niyonzima alisema kuwa katika mchezo huo ambao Simba ilishinda 5-0 kurembesha sherehe za ubingwa wa Bara 2012, marehemu Mafisango alimweleza baada ya mechi kumalizika asimpe mchezaji mwingine jezi yake kwa sababu amepanga abadilishane naye.
Marehemu Mafisango alikuwa anavaa jezi namba 30 wakati Niyonzima yeye huvaa namba 8.
"'Baada ya mechi kumalizika usimpe mtu mwingine jezi, mimi nitachukua yako na wewe utachukua yangu ili iwe ukumbusho wako kwangu'... alinisisitiza," alisema Niyonzima akimkariri Mafisango kabla ya kuangua kilio.
Niyonzima alisema msiba huo kwake ni mzito na hawezi kuusahau katika maisha yake kutokana na kuishi na marehemu Mafisango kama ndugu.
Alisema alifahamiana na marehemu tangu mwaka 2003 akiwa anaichezea Rayon na baada ya Yanga kufungwa magoli 5-0, alimueleza kuwa amelipiza kisasi.
"Sikufikiria kama Mafisango angeniambia amelipiza kisasi... aliniambia na yeye amenifunga magoli mengi kama APR ilivyowafunga Rayon magoli 8-0 katika fainali za Kombe la Amani kabla kiungo huyo hajasajiliwa na APR," alisema.
Alisema pia kama isingekuwa safari ya Simba kwenda Sudan, yeye na marehemu walipaswa kuondoka hapa nchini Mei 15 ili kujiunga na kambi ya timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi.
"Alikuwa ni kama kaka yangu, ndugu yangu, ni Mnyarwanda mwenzangu," alisema Niyonzima na kuonekana mpole pale alipokuwa akisikia watu wanasema marehemu ni Mkongo.
Niyonzima aliondoka jijini jana asubuhi akiambatana na mtoto wa marehemu Mafisango, Chris Paul (5) ambaye mama yake ni Mnyarwanda ambaye wakati msiba wa mchezaji huyo unatokea anaelezwa kwamba yuko China kwa ajili ya shughuli za kibiashara.