Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Barclays kufunga matawi yake 10

25th May 2012
Print
Comments
Mkurugenzi Mkuu wa Barclays, Kihara Maina

Benki ya Barclays imetangaza mpango wa kufunga matawi yake 10 nchini kabla ya mwishoni mwa mwaka huu uamuzi ambao unatarajia kuathiri wafanyakazi 100, wakiwamo wanaofanya kazi makao makuu ya benki hiyo.

Mpango huo ni sehemu ya mabadiliko yanayofanywa na benki hiyo yenye matawi nchini kote. Kwa mukibu wa Mkuu wa Mahusiano na Mawasiliano wa Barclays, Kati Kerenge, benki hiyo ina matawi 32 nchini kote na kwamba kwa taarifa hiyo mtandao wake utabaki na matawi 22 nchini.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Barclays, Kihara Maina, alisema uamuzi uliochukuliwa na benki yake siyo rahisi, lakini wamelazimika kufanya hivyo ili kuboresha huduma na utendaji wao.

Hata hivyo, alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanatoa huduma bora na kwamba uamuzi huo utaiwezesha benki hiyo kuwekeza kwa umakini katika fursa zozote kadiri zinavyojitokeza.

Hata hivyo, alisema maslahi ya wafanyakazi watakaohusika yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi na sera za benki hiyo.

Alisema hatua zimechukuliwa kuwajulisha wateja wote kuhusu mabadiliko hayo kupitia njia mbalimbali na pia benki imethibitisha kuchukua tahadhari kupunguza athari za huduma zake kwa wateja.

Maina alisema timu makini za watendaji zimeundwa na kupewa majukumu ya kushughulikia matatizo ya wateja na wafanyakazi na kwamba, wateja hawatalazimika kufungua upya akaunti, kwani taarifa zao zitahamishiwa katika matawi ambayo yataendelea kutoa huduma.

“Kuhakikisha kutokuwapo na usumbufu mkubwa kwa wateja wetu na wafanyakazi watakaoguswa na zoezi hili ni suala la kipaumbele kwetu na tumechukua hatua zote madhubuti kupunguza athari ambazo kawaida zinaambatana na mabadiliko kama haya,” alisisitiza Maina.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles