Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mt. Meru mgomo

29th June 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka

Madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, ambao tangu kuanza kwa mgomo wa kwanza na wa pili wa madaktari wamekuwa wagumu kuwaunga mkono wenzao, jana walianza kutoa huduma hizo kwa kusuasua, hususan baada ya kupata taarifa ya kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka.

Uchunguzi uliofanywa jana asubuhi katika hospitali hiyo, ulishuhudia askari mmoja wa usalama barabarani aliyefikishwa hospitalini hapo baada ya kupata ajali, akishindwa kupokelewa na hivyo alielekezwa kwenda kupata matibabu hospitali nyingine.

Baadhi ya wagonjwa walilalamikia kukosekana kwa huduma, ingawa wauguzi na madaktari walionekana wakiwa kazini.

“Kitendo alichofanyiwa Dk. Ulimboka ni cha unyama kabisa…ila kwa hili la kukosa huduma linatuumiza halitutendei haki,” alisikiza mmoja wa wagonjwa katika eneo la huduma za kutolea meno.

Msamaria wema aliyejitambulisha kwa jina la Abdallah Ally, alisema alikuwa akipita njiani akakuta vijana wawili wamegongwa na Hiace na kuwasaidia kuwaleta hospitalini hapo, ila alishangaa kukuta madaktari na kumtaka awalaze kwenye kitanda bila kuwashughulikia.

“Mimi nimeleta wagonjwa wawili ambao ni Jonas Maiko, mkazi wa Daraja Mbili na mwenzake William Eliya, mkazi wa Unga Limited, wakiwa hoi kwa kugongwa na Hiace ila nikaambiwa niwalaze kitandani na nikaona wamezungushiwa pazia la kijani bila huduma yoyote,” alisema.

Alisema kuanzia saa 5.00 asubuhi hadi majira ya saa 7.15 hawakuwa wamepatiwa huduma japokuwa madaktari walikuwepo.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Dk. Omar Chande, amekiri kuzorota kwa huduma ya tiba katika hospitali yake jana asubuhi.

“Mgomo haupo, ila wote tulikuwa tumeona huduma zimezorota kidogo, sasa tulikaa kufuatilia nini kimetokea,” aliwaambia waandishi wa habari jana jioni.

Alisema kuzorota kwa huduma kulitokana na madaktari kufanya mkutano wao uliokuwa ukizungumzia suala la kutekwa kwa Dk. Ulimboka na pia walitaka kujua hatma ya mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.

“Kuumizwa kwa daktari mwenzetu sio tukio la kawaida na hakuna mtu kwenye taaluma hii ambaye anaweza kufurahia jambo hilo,” alisema.

Akitoa tamko la madaktari hao, Dk. Chande alisema, “Ni kueleza jinsi walivyosikitishwa na kutekwa, kupigwa na kuumizwa kwa daktari kwa daktari mwenzao.”

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment