


.jpg)
Baraza la Wazee wa klabu ya Yanga limesema litatumia mkutano wa wanachama lililouitisha kesho bila ridhaa ya uongozi kukusanya saini 500 ambazo kikatiba zinaruhusu kuitishwa kwa mkutano maalumu halali.
Baraza la wazee na kundi la vijana wamekuwa wakijaribu kumlazimisha mwenyekiti Lloyd Nchunga kung'oka Jangwani na katika moja ya mikakati yake ni kuitishwa kwa mkutano wa kesho ambao unatarajiwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na uongozi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa wazee hao Ibrahim Akilimali alisema ingawa lengo la mkutano huo ni kuwa kama mkutano mkuu wa kila mwaka, utabadilishwa lengo lake kama Nchunga atashindwa kuhudhuria.
Endapo mwenyekiti atashindwa kuhudhuria, alisema Akilimali, wazee hao pamoja na vijana watafuata utaratibu kikatiba.
Chini ya utaratibu huo, wanachama watakaohudhuria watakusanya saini za wanachama wasiopungua 500 na kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Michezo ili kuomba kuitishiwa kwa nguvu kwa mkutano mkuu wa wanachama, alisema.
"Kama Mwenyekiti ataleta ubabaishaji wa kukwepa kuja kwenye kikao, tutafuata taratibu zinazokubalika kikatiba," alisema.
"Tutamuomba msajili wa vyama vya michezo atuitishie mkutano.
"(Hivyo) tunataka tuwaeleweshe wanachama wenzetu, mkutano wetu wa wazee pamoja na wanachama wa klabu hii (ya Yanga) utafanyika Jumapili kama tulivyopanga hapa klabuni."
Katika kuepusha kutoelewana huko kulikotawala habari za Yanga tangu kufungwa na Simba 5-0 Mei 5, Nchunga alitangaza mkutano huo ni batili na kuitisha kikao baina yake na wazee hao pia kesho Jangwani.
Lakini Akilimali alisema "hicho kikao cha mwenyekiti na wazee wa klabu hatukitambui... tunatambua mkutanao wa wanachama wa klabu na mwenyekiti wetu."
Alisema kuwa mkutano huo wa kesho utatoa picha ya hatma ya uongozi wa klabu hiyo.