


Takribani miezi 10 tangu kuzama kwa meli ya MV Spice Islander na kuua watu walioripotiwa kufikia 1,529 na karibu 1,000 kupotelea baharini, Taifa limepata msiba. Meli ya MV Karama Star get inayojulikana pia kama MV Skagit, imepinduka Julai 17, mwaka huu.
Meli hiyo ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar, ilipinduka na kuzama baada ya kupingwa na mawimbi mara tatu katika eneo la Pingume, umbali wa maili 12 kutoka bandari ya Malindi kisiwani Zanzibar.
Maiti 68 (hadi ninaandika safu hii) zimepatikana na watu 150 waliokolewa na wengine kupotea. Meli hiyo inadaiwa kuwa na abiria 290 na mabaharia tisa.
Kama tukio la MV Spice Islander la mwaka jana, huduma za uokoaji zilichelewa baada ya meli kuzama majira ya saa 7:30, lakini uokoaji ulifanyika kuanzia saa 10: 30 na kusababisha watu wengi kupoteza maisha na maiti nyingi kutawanyika kutokana na mawimbi makubwa ya baharini.
Boti mbili za uokoaji za polisi zikiwa na wazamiaji zilikwama kuondoka katika bandari ya Malindi, kutokana na ukosefu wa mafuta na kusababisha, pamoja na ile ya Kikosi cha Kuzuia Magendo (KMKM), kuondoka saa 11:15 kwenda katika eneo la tukio.
Wazamiaji wa kujitolea kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Wavuvi wa Kojani walifika kwa muda muafaka yaani saa 8 mchana, lakini waliondoka Malindi 11: 15. Inasemekana ni kutokana na ukosefu wa usafiri wakati boti mbili za kikosi cha wanamaji na bandari cha Polisi walianza kazi ya uokoaji siku ya pili tangu kutokea ajali hiyo!
Itakumbukwa kuwa Septemba 10, mwaka jana, Mv Spice Islander ilipinduka na kuzama katika mkondo wa Nungwi kutokana na kubeba abiria na mizigo kupita kiwango chake, hivyo kusababisha vifo.
Abiria katika meli hiyo walianza kutapatapa wakitafuta msaada wa kuokolewa kwa kutumia njia mbalimbali, wengine walipiga simu baada ya ajali kutokea saa 8 usiku, lakini huduma za uokoaji zilianza kufanyika saa moja Asubuhi.
Juni mwaka 2009 Meli ya MV Faith ikitokea Darees Salaam, ilizama na kuua watu sita, mbele ya sura ya bandari ya Malindi na ripoti ya uchunguzi kubainisha kuwa kulikuwa na vitendo vya uzembe.
Kufuatia tukio la kuzama kwa Meli ya Mv Karama Star Get, Waziri mwenye dhamana katika sekta ya usafirishaji, Hamad Masoud, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mipango ya Mwenyezi Mungu, kama matukio ya tsunami au kimbunga. Yaani yanapotokea duniani binadamu hawezi kuzuia!
Anasema kwa msingi huo hakuna mtu wa kulaumiwa na yeye haoni sababu za kujiuzulu wadhifa wake na kusisitiza kuwa wanaomsakama achukuwe hatua hiyo, wana chuki binafsi.
Akichagia ripoti ya uchunguzi ya kuzama kwa meli ya MV Fatih, ilipowasilishwa katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar akiwa Mwakilishi wa Jimbo la Ole (CUF), Hamad alisema viongozi na watendaji wakuu wa serikali wajenge utamaduni wa kuwajibika yanapotokea makosa ya uzembe na kusababisha vifo.
Hamad alisema (wakati huo) utamaduni wa kuwajibika ni utekelezaji wa misingi ya utawala bora kwa vitendo, na kwamba yeye ndio alikuwa mchangiaji wa kwanza katika ripoti ambayo iliwasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, Machano Othuman Said.
Mambo ya msingi ya kujiuliza ni kwamba, wakati huo Mwenyezi Mungu hakuwepo, kwamba yupo wakati huu baada ya Hamad Masoud kuwa Waziri au tuamini kwamba madaraka ni matamu kulikoni roho za binadamu?
Kwa mtazamo huo, ninakubalia na Waziri kwa asilimia 100 kuhusu hoja yake, lakini tusimsingizie Mwenyezi Mungu kwa makosa yanayofanywa na binadamu, tena kwa uzembe na kuweka mbele maslahi binafsi, mbele na kusahau maslahi ya Taifa.
Tangu kutokea ajali ya MV Spice Islander, Wizara ya Miundombinu visiwani Zanzibar, imeshindwa kuimarisha huduma za uokoaji katika kukabiliana na majanga.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wakasema walitoa taarifa kuhusu kuwepo upepo mkali kutokea baharini kwa vyombo vya usafiri, lakini watendaji wa serikali wakaruhusu boti na meli kufanya safari kama kawaida, wakiamini msemo wa ‘punda hafi, mzingo wa bwana ufike.’
Wanasema upepo ulikuwa ukivuma kwa kasi ya kilomita tatu kwa saa, mbali ya kuchafuka kwa bahari lakini SUMATRA na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) walichukua hatua gani kufuatia taarifa hiyo ya wataalamu?
Wakati Rais wa Zanzibar anasema meli ilikuwa na abiria 290 na mabaharia 9, Kaimu Mkurugenzi wa ZMA, anasema iliruhusiwa kupakia abiria wasiozidi 250 tena ikiwa chini ya uangalizi, kuona kiwango chake cha ubora.
Vyombo vya habari vya kimataifa vimeshangazwa na meli hiyo kuuzwa na kuletwa Tanzania, wakati imezuiwa kutoa huduma tangu mwaka 2009 huko katika jimbo la Ne Orleans nchini Marekani, kufuatia matukio mabaya yaliyowahi kuikumba meli hiyo.
Pamoja na matatizo ya meli hiyo kuwekwa hadi katika mitandao ya kijamii, bado ZMA baada ya meli kuwasili mwaka 2011 waliisajili na kutoa huduma na hadi inazama, ilikuwa imebakia na muda wa matumizi wa miaka miwili.
Nani wa kulaumiwa katika mazingira hayo au mipango ya Mwenyezi Mungu?
Kwa kuwa wizara imeshindwa kusimamia sera na sheria za usafirishaji, bila shaka wakati umefika kwa Waziri mwenye dhamana kujiuzulu kabla ya wananchi kufanya maamuzi yao kwa njia ya demokrasia.
Muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa isiwe ‘kichaka’ cha kujificha viongozi walioshindwa kusimamia majukumu yao, au kutumia vibaya nyadhifa kwa sababu hakuna uhusiano wowote kati ya kuzama meli na muudo wa serikali hiyo.
Tukubali kwamba ajali za meli zinazoendelea kutokea siyo mipango ya Mwenyezi Mungu, ni uzembe wa viongozi na watendaji wakuu kwa kushindwa kusimamia majukumu yao na kuheshimu haki za kikatiba za wananchi.