Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Pongezi Simba kumuenzi Mafisango

19th May 2012
Print
Comments
Maoni ya katuni

Klabu ya Simba ambayo ipo katikati ya majonzi ya kuondokewa na kiungo wake wa kigeni Patrick Mafisango imefanya jambo moja dogo, lakini lenye maana kubwa jana.

Mafisango, kiungo ambaye alikuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kutokana na uwezo wake mkubwa katika kucheza soka alifariki kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha, ambalo lilipinduka jijini usiku wa kuamkia juzi.

Ni msiba ambao umeinyang'anya Simba si tu mchezaji hodari aliyekuwa akijituma uwanjani kwa uwezo wake wote, bali pia mwanasoka ambaye hakuwa muoga kudai kutimizwa kwa stahili zake katika mkataba baina ya timu na mchezaji.

Ujasiri huu, tunakumbuka Nipashe, uliwahi kumtia matatani baada ya siku moja kusema 'mbovu' kambini kufuatia kucheleweshwa kwa malipo ya fedha za wachezaji.

Ungetaraji, kutokana na uwazi na ujasiri wake katika kudai haki labda viongozi wa Simba wangeupa umuhimu mdogo msiba huo uliosikitisha si mashabiki wa Simba tu bali wapenzi wote wa michezo kwa ujumla.

Lakini badala yake, uongozi wa Simba si tu umeonyesha ukomavu wa hali ya juu kwa kuupa uzito mkubwa msiba wa Mafisango bali pia kumuenzi marehemu huyo kama marehemu.

Makamu Mwenyekiti wa Simba Godfrey Nyange alitangaza katika msiba huo jana kuwa jezi ya Mafisango - namba 30 - imefutwa, haitovaliwa tena katika klabu hiyo.

Nyange alisema Simba imefikia uamuzi huo ikiwa ni njia ya kuuenzi mchango wake katika timu hiyo.
Na kweli. Mafisango alidumu kwa muda mfupi Simba tangu achukuliwe kutoka Azam iliyomleta nchini kutoka Rwanda.

Lakini katika kipindi kifupi hicho, na hasa msimu huu ambapo mpira ulimkubali katika kiwango ambacho hakuwahi kukionyesha Azam, mchango wake ulifunika juhudi za wachezaji wengi walioichezea timu hiyo kwa muda mrefu zaidi katika historia.

Ni kutokana na jitihada zake hizo, tunachukua fursa hii Nipashe kuipongeza Simba kwa kutambua hilo na kumuenzi marehemu ambaye ameacha mke na mtoto mmoja wa miaka mitano.

Tunaipongeza zaidi Simba kwasababu ya njia iliyoamua kuchukua kuthamini mchango na juhudi za Mafisango katika klabu hiyo.

Ni njia ambayo ingawa imeigwa jumla-jumla kutoka Ulaya, itaacha Wanasimba wa kizazi cha sasa na vijavyo si tu kumbukumbu ya kudumu ya Mafisango bali pia ufahamu wa mchango wa marehemu.
Ni njia nzuri kustaafisha jezi namba 30.

Wakati ni huu kuokoa riadha

Uchaguzi mkuu wa chama cha riadha (RT) unatarajiwa kufanyika kesho mjini Morogoro ambapo jumla ya wagombea 66 walijitokeza kwa ajili ya usaili ambao matokeo yake yanatarajiwa kutangazwa leo.

Miongoni mwa wanamichezo waliojitokeza kutaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa riadha nchini ni pamoja na wakimbiaji maarufu wa zamani na wadau wa mchezo huo.

Hivyo kwa mchanganyiko huo wa wagombea, tunaamini Nipashe, wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wana nafasi nzuri ya kuchangua viongozi ambao wana uwezo wa kuinua tena riadha kuirudisha kule ambako ilikuwa ni alama ya taifa ya mafanikio katika michezo kimataifa.

Riadha leo imeangukia kule ambako michezo mingine inalidhalilisha jina Tanzania kimataifa kwa kupeleka wanamichezo ambao huondoka nchini wakiwa tayari na kisingizio cha kufanya vibaya huko waendako, maandalizi mabovu.

Lakini sote tunakumbuka huu ni mchezo ambao ulikuwa na mashujaa kama Filbert Bayi, Suleiman Nyambui, Juma Ikangaa, Gidamis Shahanga na Joseph Isegwe ambao walirudi na medali za michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Michezo ya Olimpiki.

Ni nini kimepelekea Tanzania leo kuwa hapa ilipo kimataifa? Viongozi wapya watakaochaguliwa ni lazima si tu wafahamu sababu bali pia mikakati ya kujinasua.    


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles