Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Katiba mpya iwawajibishe wabunge

16th May 2012
Print
Comments

Mjadala wa Katiba mpya ambao ulitawala kwa mwaka mzima wa 2011, unaendelea katika maeneo mbalimbali nchini, Mwandishi Wetu, amezungumza na MKurugenzi Mkuu wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen-Kijo Bisimba, kuhusu mambo mbalimbali ambayo wanaharakati wanaona ni vyema yakajumuishwa kwenye Katiba ijayo.

Kwa mujibu wa Katiba iliyopo, Mbunge akichaguliwa basi analazimika kukaa bungeni kwa muda wa miaka mitano na baada ya hapo huingia upya kwenye Uchaguzi Mkuu kuwania muhula mwingine.

Katiba haitoi fursa kwa wananchi kumwajibisha mbunge wao iwapo atashindwa kutimiza ahadi zake kwa wananchi kama alivyoahidi wakati akiwaomba kura.

Kutokana na hali hiyo, Bisimba anasema lazima katika Katiba mpya viwepo vifungu vinavyotoa fursa kwa wananchi kumwajibisha mbunge wao iwapo atashindwa kutimiza ahadi zake za kuleta maendeleo.

Bisimba anasema kuna nchi kama Uganda ambazo kwenye Katiba zao zinatamka waziwazi kwamba wananchi wanahaki ya kumwita mbunge wao na kumtaka atoe maelezo kuhusu utekelezaji wa ahadi zake na akishindwa wanamwondoa kwa kura.

Anasema utaratibu wa sasa unaweza kusababisha wabunge wengi kubweteka wanapopata ubunge na kushindwa kwenda kuwatatua kero za wananchi wakijua kuwa hakuna sehemu ya Katiba inayowafanya wawajibike kwa wananchi waliowachagua.

“Katiba za wenzetu zinasema iwapo mbunge atashindwa kutimiza ahadi zake ataitwa na kuhojiwa na wananchi na wasiporidhika wanamwondoa, kwa sasa hapa kwetu Tanzania mbunge atasita kuwa mbunge akifa,” anasema.

Anasema kwa kuwa wananchi ndio waliomchagua mbunge wao kwa njia ya kura, basi Katiba hiyo hiyo inapaswa kuwapa haki wananchi hao hao ya kumwondoa mbunge iwapo wataona anafanya kinyume na mkataba wake na wananchi waliomwingiza bungeni.

Vyeo vya wakuu wa wilaya vimekuwa vikilalamikiwa na wanaharakati mbalimbali kuwa hakuna sababu ya kuwepo kwani vinaingilia majukumu ya wakurugenzi wa halmashauri.

Kwenye suala hilo, Bisimba yeye anaunga mkono maoni ya wanaharakati walio wengi kuwa haoni sababu ya kuwepo kwa nafasi hizo kwa kuwa vinasababisha shida ya kiutawala.

Anasema wakuu wengi wa wilaya wamekuwa wakiingilia kazi za wakurugenzi wa halmashauri (DED) na watendaji wa kata hivyo kukwamisha mipango ya maendeleo.

“DC yupo, hana kasma yoyote, hana kazi.Halmashauri ina Mkurugenzi wake na inakasma yake, inamipango yake ya maendeleo lakini kwa kuwa DC hana kasma yoyote mara nyingi kazi yake imekuwa kusigana na DED hali inayokwamisha mambo,” anasema.

Anasema watendaji wa kata wako chini ya DED lakini mara nyingi wakuu wa wilaya wamekuwa wakitumia mabavu kuwashurutisha wafanye kazi kwa matakwa yao wakijigamba kuwa wao ni wateule wa Rais.

Anasema mara nyingi wakuu wa wilaya wanaingilia mipango ya Halmashauri ambayo wala haiwahusu katika utendaji wao wa kila siku wakijigamba kwamba wao ni wateule wa rais.

“Nimetembelea halmashauri nyingi sana, huko maDC wanatumia mabavu kujiingiza kwenye shughuli zisizowahusu, wanasema wameteuliwa na Rais lakini wanashindwa kujua kwamba hata DED naye ni mteule wa Rais, hapo inatokea migongano isiyo na maana kwa kuwa DC kimsingi hana kazi,” anasema

Kuhusu uhuru wa watu kutoa maoni yao kwenye mchakato wa Katiba mpya, Bisimba anasema hakuna haja ya kuwawekea watu mipaka bali waachwe kusema lolote litakuwa na manufaa kwa ustawi wa nchi yao.

Anasema ilimradi mwananchi hamtukani mtu lazima aachwe aseme anataka Katiba ya aina gani kwani kila mtanzania anajua anataka Katiba iweje.

“Tuwe makini ili mwisho wa siku tupate Katiba nzuri, turuhusu watu waseme watakavyo na wasiingiliwe wala kuzuiwa na mtu, mchakato huu wa katiba uwe mali ya wananchi ili kila mtanzania awe na haki ya kujieleza,” anasema

Bisimba anasema watanzania wanapaswa kuutumia mchakato wa kudai Katiba mpya kama shule ya demokrasia ili Katiba itakapopatikana tuweze kujua namna demokrasia inavyofanyakazi.

“Tuhakikishe mambo yote tunayoona  yana umuhimu mkubwa yaingie katika Katiba mpya, vyombo vya kusimamia mifumo ya utendaji itafanyaje kazi, hayo yote ni muhimu tukiyazingatia ili tuwe na Katiba itakayotufikisha tunakotaka kwenda,” anasema.

Aidha, anasema kuna mambo mengi yanayotokea nchini kwa sababu ya udhaifu wa sheria zilizomo kwenye Katiba hivyo wadau wote wakiwemo wananchi wanapaswa kuyasema ili yaingizwe kwenye Katiba ijayo.

“Mfano Rais alipoteua wabunge na kuwapa uwaziri bila kuapa bungeni kulitokea mkanganyiko wa kisheria, wapo wengine walisema makosa yamefanyika, Mwanasheria Mkuu akakanusha kwamba hakuna tatizo la kisheria lililotokea, haya yote yalitokea kwa sababu ndani ya Katiba kuna mambo ambayo hayajakaa vizuri,” anasema.

Bisimba anasema hata haki za binadamu ndani ya Katiba ya sasa hazijawekwa vizuri na Katiba ya sasa haijaangalia masuala ya haki za binadamu kwa upana wake kwani sheria zingine zimekuwa vikwazo.

Anatoa mfano wa Ibara ya 30 ya Katiba ya sasa inayozungumzia haki za binadamu na wakati huo huo ikitamka kwamba sheria hiyo haizuii sheria zingine za kuharamisha yaliyotajwa kwenye Ibara hiyo.

“Hii ni kutoa haki kwa upande mmoja na kuipokonya  kwa kutumia mlango mwingine, tunataka Katiba itamke haki za binadamu kwa usahihi ili watanzania kweli wafaidi haki zao zote, “ anasema

Kuhusu Muungano, Bisimba anasema hakuna sababu ya wananchi kuzuiliwa kuzuungumzia kwa kuwa ni haki yao kusema wanachoona kwa manufaa ya taifa lao.

Anasema kwa kuwa muungano ni wa watanzania lazima wapewe nafasi waseme wenyewe kama wanataka kuendelea nao ama ufanyiwe marekebisho sehemu fulani fulani.

“Wako watanzania wanaoona muungano ukosafi kabisa na hawataki uvunjwe, wako wenye mawazo tofauti na hayo, wao wanaona hauna manufaa, wapo pia wanaoona unakasoro ufanyiwe marekebisho kidogo wote hao wasifungwe kuzungumza waachwe watoe sababu zao mwishoni itajulikana yapi ni maoni ya watanzania wengi, hata wanaosema hauna maana waachwe waseme tu” anasema.

Tume ya Katiba yenye wajumbe 30 ilitangazwa mwezi uliopita na Rais Jakata Kikwete na inatakiwa kufanyakazi zake kwa miezi 18 kisha kumkabidhi rais ripoti yake.

Baada ya kukabidhi ripoti, Rais katika kipindi kisichozidi siku zisizozidi 21 atalazimika kuitisha Bunge maalum la Katiba ambalo litajadili na kuwasilisha tena kwa Rais mapendekezo ya Katiba mpya.

Baada ya hapo Tume ya kura za maoni itafanyakazi ya kukusanya maoni ya watanzania wanaoiunga mkono Katiba hiyo na iwapo wanaoiunga mkono watavuka asilimia 50 basi itapitishwa na kuwa Katiba mpya.

Iwapo kura za maoni kwa wanaoiunga mkono haitavuka asilimia 50 basi Katiba ya sasa itaendelea kutumika hadi kura za maoni za marudio zitakapofanyika ndani ya siku 30.

Mjadala mkali wa kudai Katiba mpya ulitawala siasa za mwaka 2011 kuanzia mwanzo wa mwaka hadi mwishoni mwa mwaka ambapo wanasiasa,wasomi, wanaharakati na wananchi walishinikiza kuandikwa kwa Katiba mpya.

Vuguvugu lilianza baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na baada ya shinikizo kubwa, hatimaye Rais Jakaya Kikwete wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2011 alikubali kuwa kuna haja ya kuwa na katiba mpya itakayokidhi hadi miaka 50 mingine ijayo hivyo akaagiza mchakato uanze.

Awali, kabla ya Rais Kikwete kutoa kauli hiyo kulitokea kauli mbalimbali za viongozi wawili serikali ambao walikuwa wakibeza kelele za umma kutaka kuandikwa kwa katiba mpya na kujikuta wakikurupuka kusema maneno yaliyoamsha hasira za umma.

Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, mwanzoni mwa vuguvugu za madai haya Desemba mwaka 2010, alinukuliwa akisema hakuna haja ya kuandika katiba mpya kwani iliyopo inatosheleza mahitaji.

Kombani, alikaririwa akisema kuwa suala la kuunda Katiba mpya haliwezekani kwa kuwa serikali haina fedha na kwamba itaendelea na utaratibu uliozoeleka wa kufanya marekebisho ya Katiba pale inapohitajika.

Mwingine aliyekurupuka na kutoa kauli ya kuudhi na kejeli dhidi ya wanaodai Katiba mpya ni Mwanasheria Mkuu wa serikali, Jaji Fredrick Werema ambaye kama Kombani naye alibeza kelele za umma na kusema kuwa Katiba ya sasa inatosheleza mahitaji na hakuna umuhimu wa kuandika katiba mpya, akasema marekebisho ya kawaida yanawezekana ila Katiba mpya hapana.

Lakini kwa bahati nzuri wote wawili walizodolewa na bosi wao, Rais Kikwete, ambaye wakati akitoa salamu za mwaka mpya jioni ya Desemba 31,2010 alisema kuna haja ya kuandikwa Katiba mpya itakayotosheleza hadi miaka 50 ijayo.

Hatimaye Muswada wa Kukusanya Maoni kuhusu Mabadiliko ya Katiba ulitinga rasmi bungeni Aprili mwaka 2010 kwa mara ya kwanza ambapo baada ya kuujadili kwa kina wabunge wote wa CCM na wa vyama vya upinzani waliukataa na kutaka wananchi watoe maoni yao kabla ya kufikishwa tena bungeni.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles