


.jpg)

Hatma ya mabeki wa Simba, Juma Nyosso, Juma Jabu na kiungo Uhuru Suleiman, kuichezea timu hiyo katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa itajulikana kati ya leo na kesho wakati Kamati ya Usajili ya mabingwa wa Bara itakapokutana jijini Dar es Salaam.
Nyosso tayari inadaiwa ameshasajiliwa na Yanga huku pia akiwa na nafasi finyu ya kurejea tena Msimbazi kutokana na taarifa mbalimbali ambazo kamati hiyo imezipokea.
Akizungumza na gazeti hili jana, mmoja wa viongozi wa Simba, alisema kuwa Kamati ya Usajili itakutana na kufanya maamuzi ya mwisho kabla ya Juni Mosi na kilichokuwa kinasubiriwa ni mazungumzo na baadhi ya wachezaji wa nje ya nchi.
Kiongozi huyo alisema kuwa katika msimu ujao Simba itakuwa na wachezaji wengi chipukizi ambao wana lengo moja la kutaka kuonekana na hatimaye kupata timu za nje.
"Nafasi yao ni ndogo, hata kama Yanga watawachukua, hatutashtuka kwa sababu tayari tulishaamua zamani," alisema kiongozi huyo.
Alimtaja kiungo Uhuru kuwa ndiye anayeweza kupenya katika usajili huo kwa sababu anaamini kwamba Simba ndio nyumbani kwake kwa sababu ilikuwa pamoja na yeye wakati wa shida na raha, akikumbushia ipindi alipopelekwa India kufanyiwa upasuaji wa goti.
Aliongeza kuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu, Geofrey Nyange 'Kaburu' alikwenda Uganda kuangalia wachezaji wengine hivyo kamati itajadili mapendekezo yake na hatimaye kuyafanyia kazi endapo wataridhika na taarifa za nyota aliokwenda kuwaangalia.
Simba tayari ilishatangaza kuwatema wachezaji wawili wa kigeni ambao ni Derick Walulya kutoka Uganda na Gervais Kago wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kufuatia maamuzi hayo, mabingwa hao wa Bara sasa watakuwa na nafasi tatu za kusajili wachezaji wageni ambapo nyingine ni iliyoachwa wazi na kiungo, marehemu Patrick Mafisango, aliyefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari mapema mwezi huu.