Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Slaa aonya polisi kuhusu kujeruhiwa wabunge wake

24th April 2012
Print
Comments
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa

 Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa, ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wote waliotajwa kuhusika katika tukio la kuwacharanga mapanga wabunge wa Chadema, Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemli wa Ukerewe.

Ameonya kwamba iwapo Jeshi hilo la Polisi litashindwa kufanya hivyo, atarudi jijini Mwanza na kuhamasisha wananchi kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuteka kituo cha Polisi.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jijini Mwanza juzi jioni wakati alipokuwa akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Sahara.

Alisema  Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linazo taarifa zote kuhusu watu waliowacharanga mapanga wabunge hao wa Chadema, lakini hadi sasa hakuna aliyekamatwa wala kufikishwa mahakamani.

“Watu wangu hapa Mwanza wametoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kuwataja walioshiriki kuwakata mapanga wabunge wetu, sasa natamka hivi, ndani ya wiki moja kama watakuwa hawajawakamata wahusika nitakuja hapa tutakusanyana na kwenda kuvamia kituo cha polisi,” alisem Dk. Slaa huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi.

Alisema: “Jeshi la Polisi andaeni mabomu, bunduki na risasi, lakini tunakuja, uvumilivu umefika mwisho.” Alisema Jeshi la Polisi chini ya IGP Said Mwema wanapaswa kutambua kwamba Tanzania ni ya Watanzania wote, hivyo lazima kila mwananchi atendewe haki.

Alidai kuwa kwa vile wanaotajwa kushiriki kuwacharanga mapanga wabunge wa Chadema, ni makada wa CCM ndio sababu Jeshi la Polisi linasita kuwakamata na kuwafikisha mahakamani.

“Mwanzoni tulisema kuwa ukombozi wa taifa hili utaanzia Arusha, lakini sasa naona utaanza hapa Mwanza, Polisi wakishindwa kuchukua hatua nitakuja hapa tutaanza na kuvamia kituo cha polisi,” alisema bila kufafanua zaidi.

Katika hatua nyingine Dk. Slaa ametoa siku tatu kwa Serikali na Bunge kuchukua hatua za haraka kushughulikia matibabu ya Mbunge Kiwia ambaye uchunguzi wa kitabibu unaonyesha ameumia sana sehemu za pua na macho ambapo kuna mishipa imepoteza fahamu na kwamba asipopata matibabu ya uhakika anaweza kupata ulemavu wa kudumu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles