Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mataifa yakitaka wakimbizi watafutika

21st June 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Jana ilikuwa ni siku ya wakimbizi duniani. Ni siku ya kutafakari maisha ya wanadamu na mahusiano yao ndani ya jamii ambayo yanawahakikishia ama amani ya kuendelea na shughuli zao, au hali ya kupotea kwa amani kwa sababu ya vita na vurugu za aina nyingine kiasi cha kuwalazimisha wengine kuyakimbia makazi yao na nchi zao na kwenda kuishi maisha ya udhalili ya ukimbizi.

Tatizo la ukimbizi hutengenezwa na binadamu kutokana na mifumo ya maisha wanayoishi ambayo aghalabu husababisha baadhi ya makundi katika jamii kukosa haki zao, kuishi kwa hofu na mwishowe kuyakimbia makazi yao na kuwenda kuishi katika nchi jirani katika hali ya ukiwa sana.

Katika bara la Afrika tatizo la wakimbizi limekuwa ni sehemu ya maisha ya watu wake, ni nadra sana kusikia kuwa katika bara hili hakuna mkimbizi ambaye ama anakimbia vita vya wenywe kwa wenyewe katika nchi yake ya asili, au anawakimbia watawala katili katika nchi yake.

Kwa sasa Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ndizo nchi zinazoongoza katika katika bara la Afrika kwa kuwa na wakimbizi waliokimbilia nchi jirani kwa muda mrefu zaidi kuliko nchi nyingine; tangu mwaka 1993 alipoondolewa madarakani Siad Barre kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa vikiendeshwa na wababe wa vita, Somalia siyo tu kwamba imekuwa chimbuko la wakimbizi katika eneo kubwa la bara la Afrika, bali pia imezaa maharamia wanaoteka meli na kuleta usumbufu mkubwa wa kiuchumi katika pwani ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.

Hali ni hiyo hiyo kwa DRC ambayo kwa zaidi ya miongo miwili eneo la mashariki mwa nchi hiyo limekuwa ni sehemu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuwa chanzo kikubwa cha wakimbizi katika ukanda wa maziwa makuu. Wakimbizi hawa wamekuwa ni tatizo kwa nchi wanazokimbilia kwa sababu kuna wakati wanazidi hata idadi ya wenyeji katika maeneo husika, lakini pia wakiwa chanzo kikuu cha kuzagaa kwa silaha ndogo ndogo katika maeneo wanakokimbilia na kuchochea uhalifu.

Wakimbizi ni changamoto moja kubwa inayokabili dunia kwa sasa, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria yamekuwa chanzo cha wakimbizi kwa malaki wanaoikimbia nchi hiyo kutokana na mapigano ambayo sasa yanaingia mwaka mmoja, huku jamii ya kimataifa ama ikiogopa kuingilia katika kuzuia vita hivyo au ikikwepa wajibu huo kutokana na migongano ya kimaslahi baina ya mataifa makubwa.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba kuna kusita kwingi miongoni mwa jamii ya kimataifa katika suala la Syria.

Kukosekana kwa utawala bora, watawala kukataa kuwajibika kwa wananchi wao, na tabia ya wachache kujilimbilizia mali au kujinufaisha na keki ya taifa huku kundi kubwa katika jamii likiishi katika maisha ya ufukra mkubwa ni baadhi ya mambo ambayo yanaamsha hisia mbaya na hatimaye kuingia katika mapambano kama vita vya wenyewe kwa wenyewe na kila aina ya uasi ambao huwa chimbuko la wakimbizi.

Mara nyingi wakimbizi wengi wamekuwa ni watoto, wanawake na wazee ambao hawana nguvu ya kupambana katika dhana ya mwenye nguvu mpishe na hulazimika kikimbilia ukimbizini huku wakiishi maisha ya udhalili mkubwa.

Kwa maana hiyo tunaposhuhudia dunia leo ikiadhimisha siku ya wakimbizi kama ya mwaka huu, tunadhani ni wakati mwingine mwafaka kwa jamii ya kitaifa na kimataifa kutafakari jinsi ya kuongeza juhudi za kuboresha mifumo ya utawala katika mataifa mbali mbali ili katika kila nchi wananchi wake wajione kuwa na haki katika kuamua juu ya mustakabali wao, kikubwa zaidi waone wakinufaika na matunda ya rasilimali za taifa lao bila kubaguliwa.

Ni jambo la bahati mbaya jamii ya kimataifa haifanyi mambo kwa usawa kwa matukio yanayofanana kati ya taifa na taifa; hali hii imesababisha maafa makubwa kwa binadamu na wakimbizi wengi mno.

Mfano halisi ni jinsi Umoja wa Mataifa ulivyopitisha azimio juu ya Libya kwa kuzuia ndege za iliyokuwa serikali ya Kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi kuruka katika anga la nchi hiyo huku NATO wakiendesha doria katika maeneo hayo kwa kutungua ndege zilizokaidi azimio hilo, hali hii iliyapa majeshi ya waasi nguvu hadi kuimuondoa madarakani Gaddafi, lakini hali kama hii ya Libya ndiyo inayotokea kwa sasa Syria, hakuna hatua madhubuti za kumshurutisha Rais Bashar Al Assad kuacha kuua watu wake na kuzalisha wakimbizi kwa malaki kwa sasa.

Tunafikiri ni wajibu wa jumuia ya kimataifa kuhakikisha kuwa mazingira yanaozalisha wakimbizi yanashughulikiwa kwa nia ya kujenga ustawi wa utu wa binadamu kwa kila nchi ili kauli mbiu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) ya ‘hata mtu mmoja kulazimika kuwa mkimbizi ni tatizo kubwa’ (One person forced to flee is too many), tunahitaji mabadiliko makubwa na haki sawa kwa mataifa yote.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment