


Jumapili wiki iliyopita, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliitisha mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma na kuzungumzia maendeleo ya vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Mkutano huo wa Waziri Lukuvi na wanahabari, ulilenga kuzungumzia maadhimisho ya 'Siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani', ambayo kitaifa yalifanyika jijini Dar es Salaam, Juni 25, mwaka huu.
Katika mkutano huo, Lukuvi aliwaambia waandishi wa habari kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inakwazwa.
Kikubwa kinachokwaza vita hiyo, Lukuvi alisema ni mkanganyiko wa sheria za kudhibiti dawa hizo, ambazo zina athari kubwa kwa nguvu kazi ya taifa.
Alisema mkanganyiko wa sheria hiyo unagusa mfumo wote wa uchukuaji hatua dhidi ya watuhumiwa wa dawa hizo, kuanzia kukamatwa kwao, maandalizi ya mashtaka husika, kufikishwa mahakamani, vielelezo walivyokamatwa navyo na hata hukumu zinazotolewa.
Kutokana na kasoro hizo, Lukuvi alisema watuhumiwa wengi wamekuwa wakiachiwa hata baada ya kufikishwa mahakamani.
Kwa hiyo, akasema serikali sasa inaandaa muswada wa marekebisho ya sheria ya kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya, ambayo pamoja na mambo mengine, haitatoa tena mwanya wa chaguo la hukumu ya faini kwa wale watakaotiwa hatiani.
Badala yake, kwa mujibu wa sheria hiyo mpya, yeyote atakayepatikana na hatia atahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Alisema sheria hiyo mpya pia haitatoa mwanya wa kutumiwa kwa sheria nyingine kwa makosa ya dawa za kulevya.
Ningependa nieleze na mapema hapa kwamba, matumizi ya dawa za kulevya ama kwa kuuza au kubwia ni hatari sana.
Kwa maana hiyo daima hayawezi kukubalika, hasa katika jamii yenye maadili mema na inayoheshimu na kufuata sheria.
Kwa mantiki hiyo, anayejihusisha na dawa za kulevya anastahili adhabu kali. Hiyo ni kutokana na madhara makubwa kiafya na kimaadili yanayosababishwa na matumizi ya dawa hizo.
Kwa mujibu wa wataalamu, miongoni mwa madhara ya kiafya yanayosababishwa na dawa za kulevya, ni pamoja na ubongo kukauka na kusababisha kuchanganyikiwa, macho kuwa na giza, mapigo ya moyo kuwa dhaifu, mkakamo wa mishipa, kupooza viungo na mwanamke kutopata vizuri ada yake ya mwezi.
Wataalamu wanasema mtumiaji wa dawa za kulevya, hupata wasiwasi na hamaniko. Huona watu wako dhidi yake na hofu zimemzunguka kila upande.
Aidha, kutokana na taathira ya dawa za kulevya, makosa mengi, kama wizi, uporaji, ukabaji na hata ujambazi, yamekuwa yakitendwa. Pia machafu mengi, kama vile uzinzi, ukahaba na kadhalika, yamekuwa yakitendwa.
Vilevile, heshima zimekuwa zikivunjwa. Ni rahisi kwa mbwiaji wa dawa za kulevya kukaa uchi hata mbele ya watoto wake au wakwe zake. Sikwambii uwezekano wa hata kujamiiana na mmoja wao.
Kadhalika, kutokana na taathira ya dawa za kulevya, mali nyingi huibwa, ajali nyingi hutokea na watu wengi hupoteza maisha. Kwa uchache, huo ndio ukweli kuhusu taathira ya dawa za kulevya.
Kwa hali hiyo, ni sahihi kabisa dawa za kulevya kuitwa 'mama ya maasi'. Na kwa hiyo, vita dhidi yake ni wajibu. Wajibu huo unamhusu mtu mmoja mmoja, familia hadi taifa.
Vita dhidi ya dawa za kulevya imeanza muda mrefu nchini. Mbinu na silaha mbalimbali zimekuwa zikitumika kujaribu kushinda vita hiyo. Nafasi katika safu hii haitoshi kuzitaja.
Kwa bahati mbaya Waziri Lukuvi kwa niaba ya serikali leo anauambia umma wa Watanzania kwamba, vita hiyo imefeli. Akitaja mkanganyiko wa sheria za kudhibiti dawa hizo kuwa ndio kikwazo!
Lakini je, kuna ukweli kiasi gani katika madai hayo ya Waziri Lukuvi? Hilo ni swali linalohitaji kukaliwa kitako.
Kikwazo cha vita dhidi ya dawa za kulevya si mkanganyiko wa sheria peke yake. La Hasha! Unafiki uliokithiri katika vita hiyo ndio kikwazo. Huo ndio ukweli, ambao watu hawataki kuusema.
Ni ukweli usiopingika kuwa asili ya matumizi ya dawa za kulevya, ni unywaji wa pombe, ambapo siku zote lengo la mnywaji wa pombe ni kulewa.
Kabla ya dawa za kulevya hazijagunduliwa, wanywaji walikuwa wakinywa pombe ya kawaida. Pombe ya kawaida ilipoonekana inachelewesha lengo (kulewa) la mnywaji, ikatengenezwa pombe kali, kama vile Konyagi, John Walker, gongo, kang’ara na chipumpu nakadhalika. Lengo likiwa kumuwezesha mnywaji alewe haraka.
Hatimaye, kadiri siku zilivyozidi kwenda, wanywaji wakaizoea pia pombe kali. Ikafikia kipindi pombe kali nayo ikaonekana kufeli kumuwahisha mnywaji kufikia lengo (kulewa).
Kwa hiyo, pombe kali ilipoonekana inachelewesha lengo, ndio sasa zikavumbuliwa dawa za kulevya. Lengo likiwa lilelile. Kuharakisha kulewa. Huo ndio ukweli, ambao watu hawataki kuusema.
Sasa, leo kufumbia macho na kupigia debe kuhamasisha na kuchochea unywaji wa pombe, huku unapiga vita matumizi ya dawa za kulevya, kuna tofauti gani na kumpa mgonjwa wa malaria vidonge vya kumtibu, huku unamdunga sindano yenye vijidudu vya kuambukiza ugonjwa huo?
Pia unafiki ulioje kuwaambia watu wenye akili zao timamu kwamba, kuna pombe haramu na pombe halali?
Kwamba, iwapo leo askari polisi mathalan atakutana na watu wawili; mmoja akiwa kabeba chupa yenye pombe aina ya Tusker Lager, na mwingine kabeba chupa yenye pombe aina ya gongo, atashughulika na yule tu wa gongo. Lakini yule wa Tusker Lager atamuacha! Hivi lengo la mnywaji wa gongo lina tofauti gani na lile la mnywaji wa Tusker Lager?
Ukweli lazima usemwe. Kwamba, pamoja na manufaa ya kiuchumi yaliyomo kwenye biashara ya pombe, madhara yake (pombe) ni makubwa sana kwa jamii.
Maadamu kuna ugumu wa kuzuia na kupiga vita unywaji wa pombe, sheria ya kutoa adhabu ya kifungo cha maisha jela, kamwe haiwezi kupunguza tatizo la dawa za kulevya nchini.
Pia haitasaidia kitu iwapo wenye mamlaka au jamaa wa wenye mamlaka wataendelea kuwa sehemu ya dawa za kulevya, na pia vyombo vinavyohusika na mapambano vitakabiliwa na tatizo la rushwa.
Vilevile, haitasaidia iwapo maadili katika jamii yataruhusiwa kuendelea kumomonyoka. Kama vile kuruhusu mfano, kila kona au kila baada ya nyumba kumi kujengwa ama baa au grosari!
Muhibu Said ni mwandishi wa habari wa gazeti la NIPASHE. Simu: 0717055551 au 0755925656. Barua pepe: muhibu72@yahoo.co.uk