Friday May 24, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Ni muhimu sana kumfundisha mwanao adabu hizi za kula

20th March 2012
Print
Comments

Juzi nilimtembelea ndugu yangu mmoja hapa Dar na kwa bahati nzuri muda wa chakula ukanikutia pale. Niseme tu mapema kwamba sikupendezwa na tabia ya watoto wake kuhusu kula na ndio kisa cha kuandika makala haya.

Kwa kusema hayo sina maana kwamba mimi ama mke wangu ni fundi wa kufundisha watoto tabia njema ya kula (table manners) na inawezekana ukinitembelea na wewe ukachukizwa na tabia za wanangu, lakini niseme tu kwamba imenipendeza tukumbushane huku pia nikijikumbusha mimi mwenyewe umuhimu wa kuwafundisha watoto wetu tabia njema za mezani.

Ninaamini kwamba karibu kila mzazi angelipenda kusikia sifa nzuri za mwanae kwa jinsi anavyohusiana vyema na watu wengine katika hatua zake mbalimbali za maisha kuanzia nyumbani, michezoni, darasani hadi atakapopata ajira ama kujiajiri.

Mafanikio haya ya mwanao katika kuhusiana vyema na jamii inayomzunguka kwa kiwango kikubwa yanatokana na namna mzazi utakavyokuwa imara katika kuhakikisha mwanao anakuwa na tabia njema.

Hivyo kwa mzazi kumfundisha mwanao adabu njema ya kila kitu; kulala, kula, usafi, kutazama televisheni, kucheza ama afanye nini anapoona wageni ni sawa na kumpa mtoto huyo ufunguo wa maisha yatakayomsaidia sana katika mahusiano yake na jamii inayomzunguka

Cha kuzingatia ni kwamba watu hatukuzaliwa na tabia njema. Watoto wetu wanatakiwa kila mara kufundishwa na kuelekezwa namna wanavyotakiwa kufanya katika mazingira tofauti tofauti.

Kwa kumfundisha mwanao tabia njema za kula ni kumsaidia pia kutowaudhi wengine. Kadhalika mtoto aliyefunzwa vizuri adabu ya mezani hujiamini anapokuwa anakula na wenzake mahala kokote hata kama ni hotelini.

Hata kama mwanao anavaa nguo nzuri hana adabu mezani anaonekana hovyo.

Kitu cha kwanza kabisa ni wewe mzazi mwenyewe kujua adabu za kula kwa sababu mtoto yeyote tunategemea ajifunze mengi kutoka kwako.

Na mambo haya, kama tutakavyoyataja hapa chini uyafanye mwenyewe huku watoto wakikutazama.

La kwanza kabisa ni kunawa mikono kwa sabani, maji safi na yanayochuruzika kabla ya kuanza kula na kuhakikisha mikono inakuwa safi.

Watoto wajifunze kutonyanyukia vitu vilivyo mbali nao mezani, kama vile sabuni, maji ama chumvi na hivyo waombe walio karibu navyo kuwapa na wakishapewa waseme “asante”.

Hakikisha watoto wanakula kwa mkono wa kulia. Kama mwanao anatumia mkonowa kushoto kwa mambo mengine kama kuandika ama kubeba kitu, lakini wakati wa kula ajifunze kutumia mkono wa kulia na hilo linawezekana.

Mtoto afundishwe kutoweka chakula kingi mdomoni na pia atafune huku akiwa amefunga mdomo wake na taratibu, yaani asitafune kama anayekimbizwa huku mdomo ukiwa wazi, chakula kilionekana.

Mtoto ajifunze kutoongeaongea wakati wa chakula na hasa ‘uharamishe’ mtoto kuongea wakati idadi kubwa ya chakula kikiwa mdomoni mwake.

Mtoto afundishwe (na hii ni kwa mzazi pia) kutokulalamikia chakula kama vile kibaya, kina chumvi nyingi ama yanayofanana  na hayo. Mtoto afundishwe kutochukia chakula na kukisema kikiwa mbele yake.

Mtoto afundishwe kutoanza kula hadi mama, baba ama wageni watakapoanza kula.

Watoto wafundishwe kutotumia kisu kuweka chakula mdomoni isipokuwa kijiko, uma ama vidole vyao vya mkono wa kulia.

Watoto wafundishwe kutochokonoa chokonoa meno wakati bado wanakula na kama kuna kitu kwenye meno kinawasumbua kiasi cha kushindwa kuendelea kula basi waombe radhi na kwenda pembeni ama bafuni kukitoa.

Inapotokea kubawana na kikohozi wakati wa chakula, wazibe mdomo kwa viganja vyao na kugeuka pembeni, wakohoe.

Watoto wajifunze kumshukuru mama na hata baba baada ya chakula na wapokuwa wanakula ugenini ndio muhimu zaidi kushukuru hata kama hawakufurahia chakula.

Watoto wafundishwe kuomba ruhusa ya kuondoka mezani na hasa kama wakubwa bado wapo kwa kusema “Nimeshiba, ninaweza kuondoka mezani? Au ninaomba kuondoka mezani.”

Wajifunze kwamba kama kijiko kikidondoka chini, basi wakiokote na kukisafisha kabla ya kuendelea kukitumia.

Vile vile kwa mijini, ambako mara nyingi kila mtu anakula kwenye sahani yake, basi mtoto afundishwe kupakua chakula kiasi ambacho ana uhakika wa kukimaliza na kama hajatosheka aongeze kiasi kingine cha kumtosheleza.

Mambo haya unaweza kumfundisha mwanao kwa kutumia maswali kama vile: “Utafanya nini kama kijiko unacholia ubwabwa kitadondoka chini?” au “Utafanya nini kama chakula unachokula hakikuvutii kula?

Lingine muhimu sana ni kuwafundisha watoto kula wakiwa wamekaa na hata wakinunua vitu barabarani waambie watunze hadi wafike nyumbani na kula wameketi kitako ama watafute mahala wakae, wale na si kula wakitembea barabarani.

Ikiwezakana mzazi unaweza kukazania mtoto kujua jambo moja baada ya jingine huku pia ukimpongeza kwa kumwambia “umefanya vyema” kila hatua anayopatia.

Sisemi kwamba hayo ndio mambo pekee ya kumfindisha mwanao na bila shaka yapo, kutegemeana pia na jamii unayotoka na hata dini. Kwa mfano sisi Waislamu yapo na mengine ambayo sikuona busara kuyaandika hapa na hivyo hayo ambayo sikuyataja unaweza kuyaongezea kwa mwanao.

La muhimu jua kwamba kutomfundisha mwanao adabu za mezani, anakuwa kama watoto wa ndugu yangu niliyemtembelea majuzi na kushangaa kuona watoto wake wakila bila adabu huku wakikimbia kimbia na chakula.

Hamisi Kibari ni Mhariri wa habari, msanifu wa kurasa na mhariri wa picha za video. Anapatikana kwa simu 0713 328006/0758 143457 au email: hkibari1965@gmail.com

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment