


.jpg)
Juzi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ilitangaza kubaini ufisadi za Sh. 2,075,065,082 zilizochangwa na Halmashauri tatu za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa machinjio ya kisasa ambazo zimeyeyuka katika mazingira ya kutatanisha huku machinjiyo hayo yakiwa hayajajengwa hadi sasa.
Kuyeyuka kwa mabilioni hayo ya fedha kumebainika baada ya kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Mbunge wa Vunjo, Agustino Mrema, kuziweka kitimoto Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni, Temeke, Ilala na Jiji la Dar es Salaam katika mkutano uliofanyika juzi mjini hapa. Ilieelezwa kuwa mradi huo ulikuwa ujengwe eneo la Gombo la Mboto mwaka 2009, lakini hadi sasa hakuna kilichojengwa na fedha zilizochangwa hazijulikani zilipo.
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilichangia Sh. 223,283,088, Ilala Sh. 364,205,993, Temeke Sh. 224,000,000 wakati Halmashauri ya Jiji ilichangia Sh. 1,263,576,001.
Ilielezwa kuwa baada ya fedha hizo kuchangwa, mradi huo ulikuwa ukisimamiwa na Halmashauri ya Jiji ambayo ndiyo ilikuwa inamiliki kiwanja cha kujenga machinjio hayo, kampuni ya MEATCO ilipewa zabuni kwa ajili ya ujenzi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Fotunatus Fwema, alisema baada ya mchakato wa ujenzi kutaka kuanza huku fedha hizo zikiwa zimechangwa, ilibainika kuwa kampuni hiyo iliyopewa zabuni ya kujenga machinjio hayo ilikuwa hewa.
Ni kutokana na hali hiyo inaelezwa kuwa ujenzi wa machinjio hayo ulisitiswa baada ya baraza la madiwani kuamuru mkataba kati ya kampuni iliyopewa zabuni ya kujenga kuchunguza suala hilo.
Wakati kumekuwa na utata juu ya mradi huo, huku Halmashauri ya jiji ikisema kuwa kampuni iliyokuwa imeingia ubia na halmshauri hizo ilifilisika kabla ya kuanza kwa mradi, na kwamba hakuna mtu wa kubebeshwa lawama wala kubeba mzigo wa madeni hayo, pia kumekuwa na kauli za kutatanisha kwamba Jiji lenyewe lililokuwa linasimamia mradi huo na ambalo lilialika halmashauri nyingine tatu za Dar es Salaam, halikuweka fedha taslimu katika mradi huo isipokuwa walitoa kiwanja ambacho kingejengwa machinjio hayo.
Habari za kutatanisha juu ya kuchangwa kwa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kisha zikaishia kwenye mifuko ya wajanja katika halmashauri nchini, si mpya. Umekuwa ni mfumo wa kuendesha mambo, lakini kwa bahati mbaya sana haijawahi kusikika hatua za kisheria za kutosha zikichukuliwa dhidi ya wahusika wote bila kuingiza vizingizio vya aina mbalimbali.
Si mara moja malalamiko yametolewa juu ya utendaji wa kiwango cha chini kabisa wa halmashauri nchini; mwezi mmoja na ushei uliopita alionekana Naibu Waziri wa TAMISEMI akifoka hadi kutangaza wazi kuwa hali katika halmashauri ya Chato ni mbaya.
Alionyesha kushangazwa kwake na uendeshaji wa ovyo kabisa wa mambo huku fedha za walipa kodi zikiishia mifuko ya wajanja wachache.
Inawezekana hali hii katika halmashauri imegeuzwa kuwa kawaida, kwa sababu hata katika kashfa hii ya machinjio ya jiji la Dar es Salaam wanaotajwa kuhusika ni walewale wanaotajwa katika sakata la uuzaji wa UDA.
Serikali kwa miaka ya hivi karibuni imeongeza kiasi cha fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini pia imeongeza majukumu ya uendeshaji na usimamizi wa huduma za kijamii kwa halmashauri hizi kama vile sekta ya elimu na afya.
Wakati ni jambo jemba kuelekeza madaraka zaidi kwenye halmashauri kwa kuwa ndiko waliko wananchi na ni katika kudumisha kwa vitendo dhana nzima ya kuachia madaraka kutoka serikali kuu kwenda kwa wananchi (D by D), tunaona kuwa matarajio ya kuwawezesha zaidi wananchi yanaweza yasifikiwe kwa kuwa ndani ya halmashauri hizi kuna ulaji wa kutisha.
Tumesikia baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wakisimamishwa kazi, wengine kufukuzwa na kuchukuwa hatua za kisheria kama vile kufikishwa mahakamani, lakini bado hatujaona cheche za kutosha zikiwaka kukabiliana na uharamia unaofanywa kwenye halmashauri hizi ili kweli kuwe na hofu dhidi ya utafunaji wa fedha za umma.
Hatujasikia kwa mfano mtumishi wa umma akifunga jela kifungo cha kutisha na kufilisiwa mali zake; hatujasikia pia walidokoa fedha za umma wakishurutushwa kurejesha na kama wakishindwa mali zao kutaifishwa na kuuzwa kulipa kodi za wananchi walizotafuna. Tunafikiri bado makali ya kutosha hayajawafikia mafisadi wa mali ya umma.
Kashfa ya machinjio ya Dar es Salaam ni moja tu ya rundo la vitendo vya kifisadi vinavyofanyika katika halmashauri mbalimbali nchini, kila uchao ni wizi wa mali ya umma, ndiyo maana tumefikia mahali baada ya kuwaza sana tunajiuliza tutakwenda hivi hadi lini.