



Vigogo vya soka Simba na Yanga leo vina kibarua kigumu cha kusaka pointi tatu muhimu kwenye ligi kuu ya Bara zitakaposhuka kwenye viwanja tofauti kuendeleza mchuano wao kwenye kinyang'anyiro cha ubingwa wa ligi hiyo inayoenda ukingoni.
Simba inayoongoza kwa kuwa na pointi 47 itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na African Lyon wakati Yanga yenye mechi moja mkononi na pointi nne pungufu itakakuwa na nguvu mpya baada ya kurejea uwanjani kwa muda kwa wachezaji wake watano waliokuwa wamefungiwa ikipambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Lyon kwa niaba ya kocha wa timu hiyo Milovan Cirkovic, msemaji wa Simba Ezekiel Kamwaga alisema watalazimika kucheza kwa nguvu ili kupata ushindi utakaowaongeza morali wachezaji wake kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika dhidi ya ES Setiff ya Algeria wa Ijumaa nchini Algeria.
Kamwaga alisema kikosi cha Simba kipo kamili kwa ajili ya mchezo wa leo na watahakikisha wanashinda ili pia kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Bara kutoka mikononi mwa Yanga.
"Tunatambua ushindi wa mchezo huu wa kesho (leo) utaongeza morali kwa wachezaji kabla ya kwenda Algeria na pia utatufanya tuendelee kuongoza ligi na ndicho tunachokitaka," alisema.
"Wachezaji wetu wako tayari kwa ajili ya mchezo huu."
Afisa habari wa Yanga, Luis Sendeu alisema kuwepo kwa wachezaji waliokuwa wamefungiwa kabla ya adhabu zao kusitishwa kutaongeza hali ya ushindani kwenye mchezo wa leo wa ugenini dhidi ya Coastal.
Hata hivyo Sendeu alisema kuwa maamuzi ya wachezaji hao kucheza au kutocheza kwenye mchezo wa leo yatakuwa chini ya kocha Kostadian Papic ambaye amepanga kuhakikisha timu yake inaibuka na ushindi.
Kamwaga alisema ukiacha beki wa pembeni Juma Jabu, kikosi hicho hakina majeruhi zaidi.
Kwa upande wake, kocha msaidizi wa African Lyon, Charles Otieno alisema wanajua mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa wanacheza na vinara wa ligi kuu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa mchezo kati ya Azam FC itakayoikaribisha timu ngumu ya JKT Ruvu kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi.