Tuesday Jun 18, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

‘Biashara dawa za kulevya bado tishio’

27th June 2012
Print
Comments
Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema kuwa biashara ya dawa za kulevya ni tatizo kubwa nchini, ambalo linasababishwa na watu wachache wenye uroho wa utajiri wa haraka bila ya kujali madhara ya dawa hizo katika jamii.

Pinda aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya inayofanyika Juni 26 kila mwaka.

“Tatizo la biashara ya dawa za kulevya nchini linaongezeka na kukua kwa kasi, kwani kwa kipindi cha 2010/2011 jumla ya kilo 646 za heroine, pamoja na kilo 181 za cocaine zilikamatwa, pamoja na watuhumiwa 122 ambao walikamatwa, wakiwemo wanawake wanane,” alisema.

Pinda aliongeza kuwa katika kipindi hicho, ekari 315 za bangi ziliteketezwa, jambo linaloonyesha kuwa bangi nayo imekuwa ni tatizo kubwa hasa kwa kuwa inapatikana kwa wingi. 
                            
Aidha, alisema Serikali ipo mbioni kuanzisha chombo maalum kitakachokuwa na wajibu wa kupambana na biashara ya dawa za kulevya, na chombo hicho kipo katika hatua nzuri za kuanzishwa kwake.

Aliongeza kuwa nchi inapokuwa kituo cha biashara ya dawa za kulevya hujishushia hadhi na wananchi wake hupata usumbufu mkubwa pale wanaposafiri kwenda nje ya nchi kwa kuwa huwa wakaguliwa kupita kiasi, jambo ambalo huleta kero pia.

Pinda aliwaonya wafanyabiashara wa dawa za kelevya na kusema kuwa sheria itachukua mkondo wake.

Awali, Kaimu Kamishna wa Tume ya Kuratibu Mapambano ya Dawa za Kulevya nchini, Aisha Tesha, alisema katika kipindi cha Julai mpaka Mei mwaka huu kilo 234 za dawa za kulevya zilikamatwa ambayo ni asilimia 51 ya kilo za dawa hizi zilizokamatwa katika kipindi cha 2010/2011.

Tesha aliongeza kuwa pamoja na mafanikio, tume hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa rasilimali za kutosha kwa ajili ya kutolea elimu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment