


Ilala imeendelea kufanya vibaya kwenye michuano ya Copa Coca-Cola baada ya jana asubuhi kuchapwa mabao 4-0 na mabingwa watetezi Kigoma katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mabao yote katika mechi hiyo ya kundi A yalifungwa kipindi cha kwanza huku Ramadhan Salum akipiga 'hat trick'. Alifunga mabao yake katika dakika ya 13, 43 na 45. Bao la pili kwa washindi lilifungwa dakika ya 19 na Athuman Rashid.
Wakati Kigoma imeshinda mechi mbili kati ya tatu ilizocheza mpaka sasa katika kundi hilo, Ilala imepoteza mechi zote tatu ilizocheza. Ilala imefungwa dhidi ya Arusha, Kigoma na Lindi wakati mechi yake inayofuata itakuwa kesho dhidi ya Kusini Pemba.
Nayo Kilimanjaro imeendelea kufanya vizuri katika kundi lake la D baada ya jana asubuhi kuitandika Shinyanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Mabao ya Kilimanjaro ambayo hadi sasa imeshinda mechi mbili na kutoka sare moja yalifungwa na Adam Soba dakika ya 11 na 46 wakati la tatu lilifungwa dakika ya 81 na James Henry.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jana asubuhi, Temeke na Mtwara zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Tamco mkoani Pwani.
Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani ulishuhudia Morogoro na Kaskazini Pemba zikitoka sare ya bao 1-0. Amin Kassim aliifungia Kaskazini Pemba dakika ya 51, na Morogoro wakasawazisha dakika ya 75 kupitia kwa Mutalemwa Katunzi katika mechi hiyo ya kundi B.
Leo ni mapumziko, na michuano hiyo itaendelea tena kesho kwenye viwanja vyote vinne.