


.jpg)
Yanki Edward Chritopher jana alifunga 'hat trick', likiwemo bao la dakika ya 102 ya muda wa nyongeza na kuiwezesha Simba B kuifunga Mtibwa Sugar 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya 3-3 katika dakika 90 za mchezo huo wa kuvutia wa fainali ya ligi ya Super8 kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa ushindi huo, Simba B imezawadiwa sh. milioni 40 za bingwa wa michuano hiyo ya maandalizi ya msimu inayodhaminiwa na BancABC.
Simba B ilipata bao la kwanza katika dakika ya 11 likifungwa na Chritopher baada ya kuunganisha krosi ya Haruna Athumani aliyekuwa ameitoka safu ya ulinzi ya Mtibwa kabla ya kutoa pasi hiyo.
Lilikuwa bao la tano la Christopher katika mechi tano za michuano hiyo.
Mtibwa pia ilikuwa ikichezesha kikosi cha B lakini kikipewa sapoti na wachezaji wenye majina ya Shaaban Kado, Salum Swedy, Salvatory Ntebe, Hussein Javu na wakongwe Shaaban Kisiga na Vicent Barnabas.
Kisiga, mchezaji wa zamani wa Simba, aliisawazishia Mtibwa kwa penalti iliyotolewa na muamuzi Hashim Abdallah baada ya Jamal Mnyate kukawatuliwa na Omary Salum ndani ya eneo la hatari.
Dakika nane tangu kuanza kwa kipindi cha pili Christopher aliipatia Simba bao la pili akiunganisha krosi ya Rashid Salum, lakini akipiga mpira wa adhabu ndogo Kisiga hakutaka kuzidiwa kete na 'dogo' huyo baada ya naye kuifungia Mtibwa goli la pili katika dakika ya 56.
Mpishi wa goli la kwanza la Simba B Athumani aliipa timu yake bao la kuongoza kwa mara ya tatu katika dakika ya 66.
Lakini Hassan Seif aiyeingia kutoka benchini kuchukua nafasi ya Kisiga akaisawazishia Mtibwa kwa mpira wa adhabu ndogo tena robo saa baadayem, kulazimisha mchezo huo uingie katika muda wa nyongeza.