Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

TFF yamtambua Nchunga Yanga

22nd May 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga,Lioyd Nchunga

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesema kuwa msimamo wake ni kuwa halitatambua maamuzi yoyote yanayofanywa na wanachama wake ambayo yako nje ya taratibu na maelekezo yaliyoainishwa katika katiba ya klabu hiyo.

Kauli hiyo ya TFF imekuja kufuatia mkutano wa wanachama wa Yanga uliofanyika juzi Jumapili kwenye makao makuu ya klabu hiyo ambapo walitangaza kuwa wamemuondoa madarakani Mwenyekiti wa Klabu hiyo, Lloyd Nchunga, kwa madai kwamba ameshindwa kuwaongoza na anavunja katiba yao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa wanachama wote wanatakiwa kuheshimu na kulinda katiba za klabu yao na hawana budi kufuata katiba hizo katika kufanya mabadiliko ya uongozi endapo wana sababu ya kutekeleza maamuzi hayo.

Osiah alisema kuwa hakuna mwanachama (klabu au vyama vya michezo) ambaye atafanya mabadiliko bila kufuata katiba na mabadiliko hayo yakatambuliwa.

"Wasivuke taratibu kuanzia chini halafu wakafikiri wakija huku kwetu tutawatambua, tunasisitiza kuwa msimamo wetu ni kutotambua uongozi ambao utateuliwa kwa muda, hiyo ni kwa mujibu wa ibara ya 12 (2) ya TFF inavyoeleza," alisema Katibu huyo.

Aliwataka wanachama kuwa na subira na kuwaeleza kwamba hakuna katiba inayokataa mabadiliko ya uongozi na wafahamu kwamba hakuna matatizo au migogoro itakayotatuliwa nje ya katiba.

Alieleza kuwa tayari shirikisho limeshakutana na viongozi wa Yanga na kuwaeleza kwamba wakutane na upande wa pili ili kumaliza matatizo yao kwa njia ya busara kwa lengo la kuhakikisha wanajipanga kusajili wachezaji wenye uwezo na kufanya maandalizi ya kutetea ubingwa wao wa mashindano ya Kombe la Kagame yanayotarajiwa kuanza Juni 23 hadi Julai 8 mwaka huu.

NCHUNGA ALONGA

Nchunga aliliambia gazeti hili jana kuwa kilichofanywa na wanachama wa Yanga waliokutana Jumapili si jambo sahihi na anaeleza kuwa mkutano huo ulikuwa ni kama 'sinema'.

Mwenyekiti huyo aliendelea kusema kuwa wanachama wake wanatakiwa kuwa na subira endapo wanaitakia mafanikio klabu hiyo kongwe hapa Afrika Mashariki.

Alisema kuwa Julai 15 sio mbali na Kamati yake ya Utendaji ilipanga siku hiyo kwa kuzingatia taratibu zilizoelezwa katika katiba yao kwa uongozi kuitisha Mkutano Mkuu.

Aliongeza kuwa mkutano huo aliouitisha ni Mkutano Mkuu wa mwaka na agenda zake zimeelezwa katika Ibara ya 21 ya katiba ya Yanga.

Aliwataka wanachama kuendelea na maandalizi ya kujitokeza katika mkutano huo aliouitisha huku akisema kwamba uongozi uko kwenye mchakato wa zoezi la usajili wa wachezaji na kusaka mrithi wa kocha Mserbia Kostadin Papic.

Kwa mujibu wa katiba ya Yanga Ibara ya 17, Mkutano Mkuu ni ule tu ulioitishwa kwa kufuata utaratibu na ndio wenye mamlaka ya kufanya maamuzi. Na miongoni mamlaka ya mkutano huo kama yalivyoelezwa katika Ibara ya 19 kipengele cha (13) na (15), ni kubatilisha mamlaka ya mwanachama na pia kumsimamisha au kumfukuza mwanachama.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles