Wednesday May 22, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mwenge wa Uhuru watumia `chopa` kwenda kufungua miradi Mang`ola

12th August 2012
Print
Comments

Mwenge wa Uhuru ambao ulianza mbio za siku moja wilayani hapa, ulilazimika kutumia helikopta (chopa) kutoka eneo la kijiji cha Kibaoni hadi Mang’ola umbali wa kilomita zaidi 60.

Waandishi wa habari walipigwa chenga wakati wa kuupandisha Mwenge kwenye chopa nyakati za asubuhi baada ya kuambiwa watangulie kwa magari kwenda Mang’ola na hata wakati wa kuuteremsha walipelekwa eneo lingine tofauti na pale walipokusudia uteremshwe. Waandishi wa habari na wakimbiza Mwenge wengine kutoka mkoani na wilayani hapa walilazimika kutumia usafiri wa magari na wale wa kitaifa walitumia chopa.

Uamuzi wa kutumia chopa hiyo ulitokana na kile kilichoelezwa kwamba kulikuwa na njia moja tu ya kwenda Mang’ola na kwa utaratibu Mwenge usingeweza kutumia njia hiyo hiyo kwa kurudi tena mjini Karatu. Wakiamua kukwepa kutumia njia moja mara mbili yaani wakati wa kwenda na kurudi, jambo ambalo sio utaratibu, uongozi wa Wilaya ya Karatu chini ya Mkuu wa Wilaya Felix Daud Tibenda, aliamua kutumia chopa wakati wa kwenda na wakati wa kurudi ulikimbizwa kwa gari. “Tunataka kuwazidia watu wa Wilaya ya Monduli, sisi tutatumia njia mbili kukimbiza Mwenge, kwa vile wakimbiza Mwenge wamechoka tutatumia ndege kwenda Mang’ola kufungua miradi yetu,” alitamba Mkuu wa Wilaya Tibenda wakati WA makabidhiano ya Mwenge yaliyofanyika jana asubuhi eneo la Kibaoni wilayani hapa.

Mamia ya watu waliofurika kuupokea na kuona Mwenge huo ukipakizwa na kushushwa ndani ya chopa walijikuta wakiambulia patupu baada ya kuzidiwa maarifa ya jinsi ya kupakiza na kuushusha. Mapema Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Kapteni Honest Ernest Mwanossa na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, alizindua vyumba viwili vya madarasa na mradi wa utunzaji mazingira kwa kupanda mti katika Shule ya Msingi Kibaoni.

Baada ya kumaliza kuzindua miradi hiyo, msafara wa magari ulianza kuelekea Kijiji cha Mang’ola na dakika chache chopa ya polisi iliwasili shuleni hapo kisha kuwachukua maofisa wanne wakiwamo wakimbiza Mwenge kitaifa.

Katika kile wananchi waliamini jana ilikuwa ni siku yao maalumu kushuhudia Mwenge ukiingizwa ndani ya chopa, ghafla matumaini hayo yalipotea baada ya Mwenge huo kupakizwa kwenye gari nyingine ya wazi kisha kupelekwa uwanja mdogo wa ndege wa Manyara. Ukiwa huko dakika chache baadae chopa hiyo ilirejea na kuelekea katika uwanja huo wa ndege ambao hutumika kwa shughuli za kitalii na shughuli nyingine za kupokea viongozi wa serikali.

Dakika 10 hivi baadae, chopa hiyo ilisikika ikiondoka na kuonekana angani ikielekea Mang’ola kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kuzindua miradi ya maendeleo.

Mamia ya wananchi waliofurika katika uwanja wa Barazani huko Mang’ola walijikuta wakipigwa chenga baada ya chopa hiyo kwenda kushuka sehemu nyingine tofauti na walivyoelezwa hapo awali. Kwa mujibu wa maelezo ya awali na chopa kutua kwenye uwanja wa Barazani kuwateremsha wakimbiza Mwenge kitaifa, awamu ya pili ya chopa ikiwa na Mwenge haikuweza kwenda kutua kwenye uwanja huo na badala yake ilitua kwenye uwanja mdogo wa Qangdedd uliopo jirani na ofisi za katibu tarafa katika kiwa Haikuweza kujulikana mara moja lengo la kuwapiga chenga wananchi na waandishi wa habari lilikuwa ni nini, lakini wengi walitaka kupata picha ya Mwenge huo ukiwa umezimwa na kuingizwa kwenye chopa. Mwenge wa Uhuru leo unakabidhiwa kwa Wilaya ya Ngorongoro.

Miradi iliyofunguliwa Mang’ola ni kuweka jiwe la msingi ujenzi wa barabara, kuweka jiwe la msingi maabara ya Sekondari ya Baray, kukagua mradi wa umwagiliaji shamba, kuzindua wodi ya zahanati ya Mbuga Nyekundu, kuweka jiwe la msingi nyumba za walimu mbili za watumishi ambazo ni za ‘two in one na kutoa vyeti kwa watumia maji.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment