Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Bunge liweke azimio kuwabana wezi fedha za umma

18th April 2012
Print
Comments

Bunge lilioanza mapema wiki iliyopita lilianza kwa wabunge wateule wawili kuapishwa mjini Dodoma, ambapo Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Paresso wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliapishwa.

Hata hivyo awali, zoezi la kuapishwa lilishindikana baada ya wabunge hao kushindwa kufika siku iliyopangwa katika orodha ya shughuli za Bunge, jambo ambalo lilifanya kupangiwa siku nyingine.

Hata hivyo, Bunge hili linaonyesha kutokuwa na msisimko kutokana na shughuli ambazo zimeshafanyika katika wiki hiyo ya kwanza.

Hata hivyo, uchaguzi wa Bunge la Afrika Mashariki, unaonekana kuibua hisia za Watanzania wakiwemo na wabunge kutokana na umuhimu wake kwa Taifa la Tanzania na mataifa mengine ambayo ni wanachama.
Watu waliojitokeza kuwania nafasi hizo wameonekana wakiranda randa katika viwanja vya Bunge wakijaribu kuomba wabunge ambao walipiga kura jana kuwachagua.

Uchaguzi huo ambao unalenga kuwapata wabunge tisa wanatakiwa katika kuwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki, unaonekana kugusa nyoyo za Vyama vya Upinzani.

Chadema ambacho ni chama cha upinzani kilicho na idadi kubwa ya wabunge bungeni kimeeleza kutofurahishwa na utaratibu unaotumika katika kuwapata wabunge hao.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe, anaona uchaguzi huo unalenga kuwafanya wagombea wa chama hicho kama mawakala kutokana na chaguzi zailizotangulia kukosa wawakilishi.

Anatoa mfano wa uchaguzi wa kuwachagua wawakilishi wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika ambao chama hicho hakikushinda.

Hivi karibuni Chadema kiliomba kuahirishwa kwa uchaguzi huo hadi hapo kanuni hizo zitakapobadilishwa na kuruhusu  idadi ya wabunge wa Bunge hilo kutoka kwa kila vyama uwiane na uwakilishi.

Kwa mujibu wa chama hicho, CCM ipate viti visivyozidi saba, Chadema kimoja na Chama cha Wananchi (CUF), kipate kiti kimoja.

Naibu Spika Job Ndugai, anasema uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, utafanyika kama ilivyopangwa kwasababu hakuna sababu za msingi za kuuahirisha.

Ndugai anasema Kamati ya Kanuni ya Bunge, imeamua uchaguzi huo uendelee kwa kuwa hakukuwa na sababu za msingi za kuuarisha.

“Ni uelewa tu ndio wa kanuni zetu, tumekaa muda mrefu katika kikao tukaangalia wenzetu wa Uganda na wa Kenya wanafanyaje,” anasema.

Anasema tafsiri ya neno kambi ya upinzani halieleweki vizuri  na kwamba kwa mabunge yanayofuata mfumo wa  Jumuiya ya Madola, kambi zipo mbili tu ambazo ni upinzani na chama tawala ambapo chama hicho kiligombea lakini kikajikuta kikishindwa.

Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas kashililah, vyama vilitakiwa kuleta wagombea watatu kila kundi ili wabunge waweze kuchagua wagombea wanaona kuwa wanafaa.

Lakini mbali na hiyo Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2011, ambao ulikataliwa na kurudishwa serikali katika Bunge lililopita, umerejea tena huku sheria ya marekebisho ya Bodi ya Mikopo ikiondolewa katika marekebisho hayo.

Miongoni mwa hoja ambazo zilichangiwa kwa hisia kali wakati wa kujadili muswada huo ni vigogo wa dawa za kulevya wakamatwe na kufikishwa mahakamani kwani tatizo la dawa za kulevya limezidi kuwa kubwa sanjari na kuongezeka kwa vijana wanaotumia dawa hizo maarufu kama mateja.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, anasema inashangaza kuona kiwango cha dawa za kulevya kinachoingia nchini kikizidi kuongezeka lakini idadi ya watuhumiwa ikipungua.

“Tukisema eti tatizo linakuwa kubwa kwasababu ya udhaifu wa sheria si kweli, sheria zipo tena kali lakini usimamizi na utekelezaji wa sheria ndio mbovu, serikali iseme kwanini dawa zinaingia kwa wingi sana lakini watuhumiwa hawapo,” anasema Mnyika.

Anasema serikali lazima itaje majina ya watuhumiwa wanaosafirisha dawa za kulevya kuja hapa nchini badala ya kuweka mafaili ya watu hao makabatini.

Suala lingine lililotikisa Bunge ni Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), ya mwaka jana ambayo inaeleza jinsi ambavyo kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa mabilioni ya fedha za umma.

CAG Ludovick Utouh alisema wiki iliyopita kwamba katika bajeti ya mwaka jana, serikali ilitumia Sh. 544 bilioni bila kuidhinishwa na Bunge huku ikikopa kwa kwa asilimia 38 na kufanya deni la taifa kufikia Sh. 14.4 trilioni kutoka Sh. 10.5 trilioni mwaka juzi.

Kadhalika, serikali imelipa mishahara kwa watumishi hewa mwaka jana yalikuwa shilingi bilioni moja wakati balozi za Tanzania nje ya nchi zikitumia Shilingi bilioni tatu nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kwamba bado tunakabiliwa na upungufu mkubwa kwenye mikataba mingi baina ya serikali na watoa huduma au kampuni zinazotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukosefu wa nyaraka muhimu kama vile masharti ya mikataba, michoro na maelezo ya kina ya jinsi ya kutekeleza mkataba.

Mengine ni kutotumika kwa kifungu cha fidia kwa kuchelewa kutekeleza mikataba na kutokuwepo mipango ya kudhibiti na kutoa hakikisho la ubora katika utekelezaji wa mikataba, kazi zilizokamilika hazikufanyiwa tathmini kuona kama zimekidhi matakwa ya utekelezaji aliyopewa mkandarasi katika mkataba.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Augustino Mrema, anaeleza kushangazwa na kitendo cha serikali kutowachukulia hatua wabadhirifu wa mali za umma.

Hata hivyo, alipendekeza kiundwe chombo maalum kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya CAG ili wahusika wachukuliwe hatua kama inavyostahili.

Mweyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Zitto Kabwe, anasema baadhi ya mashirika hayatendi kazi vizuri kwa kuwa Serikali inaingilia Bodi za Wakurugenzi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC), John Cheyo, anawataka wahasibu kote nchini watimize wajibu wao ili kuondoa kasoro mbalimbali ambazo zimekuwa zikisababisha upotevu wa fedha za umma.

Hii ni kwa mara nyingine tena CAG anatoa ripoti yake ya ukaguzi na kueleza ubadhirifu wa fedha za umma lakini umma hauoni hatua madhubuti zikichukuliwa kwa wahusika.

Inasikitisha kusikia taarifa hizi kila mwaka; wakati umefika sasa kwamba Bunge liweke azimio la kuibana serikali iwachukulie hatua wezi na wafujaji wa fedha za umma.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles