Tuesday May 21, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Coastal yanasa kiungo wa Yanga

27th June 2012
Print
Comments
Kiungo wa Yanga, Pius Kisambale

Kiungo wa Yanga, Pius Kisambale, jana alivunja mkataba na mabingwa hao wa mashindano ya Kombe la Kagame na kujiunga na timu ya Coastal Union ya jijini Tanga kwa ajili ya kuichezea katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, imefahamika.

Coastal Union msimu uliopita ilimaliza ligi ya Bara ikiwa katika nafasi ya tano baada ya kujikusanyia pointi 39 huku mabingwa Simba wakiwa na pointi 62 katika msimamo wa ligi hiyo iliyoshirikisha timu 14.

Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Kisambale alisema kuwa amesaini mkataba wa mwaka mmoja baada ya klabu hiyo ya jijini Tanga kufanya mazungumzo na Yanga ambayo yalifikia muafaka.

Kisambale alisema kwamba lengo la kwenda Coastal Union ni kujihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza na ahadi aliyoahidiwa na klabu hiyo kumpa maslahi mazuri.

"Ni maamuzi ambayo yananipa faraja, naamini nitacheza na nitaisaidia kufanya vizuri katika msimu ujao ukizingatia klabu hiyo imejipanga kuleta mapinduzi kisoka," alisema nyota huyo.

Alisema kuwa anatarajia kuanza mazoezi na timu yake hiyo mpya wakati wowote kuanzia leo na kwake itakuwa ni muendelezo kwa sababu alishaanza kujifua na Yanga.

"Leo (jana) ndio nimesaini mkataba mpya lakini hadi jana (juzi Jumanne) nilikuwa nafanya mazoezi na wachezaji wa Yanga, kwa sasa timu yoyote inafaa kucheza na si kama ilivyokuwa zamani kuzipa kipaumbele Simba na Yanga," alisema kiungo huyo.

Hata hivyo Coastal Union bado inasaka kocha mkuu baada ya Jamhuri Kihwelu 'Julio' kumaliza mkataba wake mfupi wa kuiongoza.

Ligi Kuu ya Bara msimu ujao inatarajiwa kuanza Septemba Mosi mwaka huu na timu zilizopanda daraja ni JKT Mgambo, Prisons ya Mbeya na Polisi Morogoro.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment