Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tusahau maneno ya adui wetu, tukumbuke ukimya wa rafiki zetu

2nd May 2012
Print
Comments

“Hatimaye tutasahau maneno yaliyosemewa na adui zetu, lakini tutakumbuka ukimya wa marafiki zetu wakati tulipokuwa taabuni.”

Hayo ni maneno yanayosikika kwenye simu ya aliyekuwa Rais wa Umoja wa Vijana wa chama tawala cha African National Congress (ANC) nchini Afrika Kusini, Julius Malema, aliyetimuliwa kutoka katika chama hicho.

Kwa mujibu wa gazeti la Star la nchini humo, Malema ambaye hajatoa tamko rasmi (hadi niaandika makala haya), kuhusu kufukuzwa kwake kutoka ANC, simu yake inapopigwa inajibu kwa `mlio’ wenye maneno hayo na mengine yakisema, “hakuna kushindwa, hakuna kujisalimisha, ushindi ni lazima.”

Si nia yangu kuingia kwa undani na kujadili sakata la kutimuliwa kwa Malema kutoka ANC ama msimamo wake ulio sababu ya kufikiwa hatua hiyo, lakini ujumbe wa aina zote mbili, unaweza kutoa majawabu ya kizungumkuti kinachoikabili hali ya kisiasa nchini.

Umma unatambua wazi kuhusu uwepo wa mawaziri wanaotakiwa kushughulikiwa ili haki itendeke dhidi ya uovu wanaodaiwa kulifanyia taifa hili.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeweka wazi uovu huo unaohusisha ‘uporaji’ wa mabilioni ya fedha za umma, zilizoingizwa kwenye mifuko ya wapuuzi wachache (ingawa wengine wanawaita wajanja-hawana ujanja wowote!)

Lakini pia ipo taarifa ya kamati ndogo ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyoweka wazi uozo mwingine ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ikatoa mapendekezo kadha wa kadha.

Baada ya taarifa hizo kuwasilishwa bungeni, umma ulistuka, wananchi kwa idadi isiyojulikana wakawasiliana na wabunge wao, wakihoji ni kwa namna gani Bunge litatekeleza wajibu wake wa kuidhibiti serikali?

Kwa maana taifa limekuwa katika hali tete! Uchumi wa nchi unahujumiwa, kibaya zaidi uhujumu huo haufanywi na raia kutoka mataifa ya kigeni, bali Watanzania waliopewa dhamana ya uongozi wa umma.

Kwenye orodha hiyo unawakuta mawaziri, wakurugenzi wa halmashauri, wakuu wa idara, wakuu wa mashirika na taasisi za umma, japo kuwataja kwa uchache wakilifisadi taifa.

Watu kadhaa wakapaza sauti. Vyombo vya habari vikapaza sauti. Asasi za kijamii zikapaza sauti. Raia walio wengi wakapaza sauti wakitaka mapendekezo ya Bunge kwa serikali kuwashughulikia wahusika yatekelezwe kwa ukali na haraka.

Kupaza sauti dhidi ya wahalifu na uhalifu uliotokea si uasi dhidi chama cha siasa, si uasi dhidi ya uzalendo, si uasi dhidi ya urafiki binafsi, si uasi dhidi ya utaifa. Bali ni tendo lililo jema na lenye lengo la kuijenga na kuiimarisha Tanzania yenye manufaa kwa Watanzania wa leo na hata wa miaka zaidi elfu ijayo.

Lakini wapo miongoni mwa Watanzania walionyamaza kimya. Wana midogo lakini hawakuifungua. Wana vidole lakini hawakuvinyoosha. Wana vichwa lakini hawakuvitikisa kama ishara ya kuukataa uhalifu na wahalifu dhidi ya fedha za umma. Wakawa kimya.

Walio kimya na bado wanaendelea kuwa kimya ni raia wenzetu, wana matatizo kama ya wanaopaza sauti, wanahusika kuongeza kizazi kijacho na kitakachozitegemea rasilimali za umma kwa maendeleo na ustawi wao.

Kwa nini wanakaa kimya wakati huu wa taabu ambapo uovu, uhujumu uchumi na uporaji wa mali na rasilimali za umma vimekithiri? Wamekuwa na nidhamu iliyovuka mipaka kiasi cha kuwa waoga? Hawajui walitendalo? Ama wapo kama hawapo?

Miongoni mwa marafiki zetu walioamua kuwa kimya, wasiuzungumzie uovu uliofunuliwa na CAG na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ni wabunge, wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kuwawakilisha bungeni.

Ukimya wa wabunge walioshindwa kukemea uovu na waovu waliotajwa kwenye ripoti za CAG na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ukatoa mwanya kwa waovu kupanga mikakati ya kujisafisha, ili waonekane ni wema machoni pa umma.

Wametoa utetezi wao usiokuwa na mashiko, wamewashambulia mawaziri na wabunge wenzao, wamevilaumu vyombo vya habari, wameibua kila aina ya hoja, wamezungumza.

Dhana ya maslahi ya umma inawafanya wahusika katika wizi wa fedha na rasilimali za taifa wawe maadui wa nchi. Kwa maana waliyoyafanya ni kinyume cha misingi ya utaifa.

Maneno mengi waliyoyazungumza hayajafuta ukweli kwamba wamehusika kwa namna tofauti katika wizi wa fedha na rasilimali za umma.

Ilipotamkwa bungeni na wabunge wenye ujasiri, kwamba inatupasa kuzungumza kwa pamoja ili kupambana na uovu huo, huku wenye kufuata itikadi za kisiasa wakiweka kando tofauti zao, taifa linapaswa kuwa moja, likinuwia jambo moja lililo kuu-vita dhidi ya ufisadi.

Haistahili watuhumiwa wa ufisadi kama ulioibuliwa kwenye ripoti ya CAG na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakaachwa watambe. Haiwezekani!

Wasiposhughulikiwa, ipo siku watoto wao, wajukuu zao, wachumba zao, wenza wao ama yeyote aliye katika shirika nao, watashughulikiwa.

Kwa hali hiyo, kinachotakiwa sasa ili kudhibiti uovu kama ulioibuliwa kwenye ripoti ya CAG na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ni vita isiyohitaji kushindwa. Ni vita dhidi ya uovu. Ushindi utapatikana.

Ni kama ‘anavyojibu’ Malema wa ANC kwenye muitikio wa simu yake ya kiganjani, “hakuna kushindwa, hakuna kujisalimisha, ushindi ni lazima.”

Ushindi dhidi ya waovu na uovu unaofanywa kwa taifa hili lililopata uhuru wake Desemba 9, 1961 (wakati huo ikiwa Tanganyika) kisha ikaungana na Zanzibar Aprili 26, 1964 kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lazima upatikane.

Wakati hayo yakijiri, taifa liwatambue marafiki zetu, wale walio kimya na (pengine) wanaendelea kuwa kimya.

Lakini ukweli ni kwamba maneno ya maadui wa uchumi na ustawi wa nchi na watu wake yatasahaulika ikiwa hatua stahiki zitachukuliwa.

Wakishughulikiwa kwa mujibu wa sheria, taifa halitakuwa na kumbukumbu ya majigambo yao, lakini tutaendelea kukumbuka ukimya wa marafiki zetu hasa wakati huu ambapo taifa linataabika kutokana na kukithiri kwa ufisadi unaowaneemesha wachache.

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe: [email protected]

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles