Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Uko wapi Mzee Kingunge Ngombale Mwiru?

19th May 2012
Print
Comments

Nimeanza makala haya kwa makusudi kabisa kuuliza swali hili nikitarajia kwamba nitawashtua baadhi ya wadau wa siasa. Wengi wakijiuliza kulikoni. Swali hili nimeliuliza kwa nia njema kabisa kutokana na heshima ya Mzee Ngombale aliyoijijengea ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika siku za karibuni, kumejitokeza mijadala mizito yanayogusa mustakabali wa CCM na Taifa kwa ujumla, ukigusia zaidi masuala ya siasa, uchumi na kijamii.

Pamoja na mijadala hiyo kupamba moto katika kila kona ya nchi yetu, huku baadhi ya wazee wastaafu (makada) ndani ya chama hicho wakijitokeza hadharani kutoa maoni yao; sikusikia wazee maarufu wenye msimamo mkali kama Mzee Ngombal, wakijitokeza kujibu tuhuma hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zimetoa sura mbaya ya chama mbele ya jamii.

Baadhi ya wazee waliosikika wakitoa maoni yao ni pamoja na Joseph Butiku, Kaduma na Hans Kitine. Awali ya yote, naomba niweke wazi kuwa Katiba ya nchi ibara 18 (1) inatamka bayana kuwa kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila kujali mipaka ya nchi.

Kwa maana nyingine, baadhi ya hawa wazee ambao miongoni mwao nimewataja hapo juu, wako huru kutoa maoni yao kwa mujibu wa Katiba.

Jambo ambalo limenisukuma hadi kujiuliza kulikoni, mbona Mzee Ngombale Mwiru yuko kimya, ni kutokana na kauli kali ya wazee hawa ambazo ziligusa jamii bila kupata majibu kutoka kwa wazee wenzao ambao wanaaminika kuwa wana imani na itikadi kali kwenye chama tawala.

Ni ukweli usiofichika kwamba, huwezi kuzungumzia historia ya CCM na serikali yake bila kumuhusisha au kumgusa Ngombale Mwiru.

Mzee huyu na chama naweza kuwaita kama ni mapacha. Ni mtu anayeheshimu miiko na maadili ya uongozi. Hasiti kukemea jambo pale panapobidi.

Naam, sasa nijielekeze moja kwa moja, katika hoja yangu ya msingi. Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM kilichoketi karibuni mjini Dodoma, pamoja na mambo mengine, kilibariki mapendekezo ya marekebisho ya katiba ya chama hicho (CCM).

Pamoja na nia nzuri ya chama kujaribu kupanua wigo wa demockasia  kwa kupendekeza wajumbe wa Nec ngazi ya Taifa kwamba watoke kwenye ngazi ya wilaya badala ya ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.

Mapendekezo hayo ingawa yalipitishwa na Kamati Kuu (CC)  ya chama, hatimaye kupata baraka za wajumbe wa Nec. Hata hivyo walikumbana na pingamizi kali kutoka kwa Mzee Ngombale Mwiru.

Katika kikao hicho, Ngombale aliweka wazi bila kutafuna maneno kwamba yeye haungi mkono mapendekezo hayo akisema kuwa katiba imekiukwa.

Alienda mbali zaidi kwa kuiomba kikao hicho nchini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete kuweka kumbukumbu sawa, kwamba yeye hakushiriki katika kupigia kura mapendekezo hayo.

Huyu ndiye Mzee Ngombale Mwiru mtu ambaye anaishi kwa msimamo usioyumba. Ni mwanasiasa kitaaluma, hayumbi katika maamuzi yake.

Nimeshangazwa na ukimya wake hata pale ambapo wazee wenzake walipojitokeza kushambulia chama (CCM), kwamba inakumbatia mafisadi, na kwamba chama kimepoteza mwelekeo na kinaelekea kufa. Hajajitokeza Mzee wa ‘saizi’ yao kama Ngombale Mwiru kuweza kujibu tuhuma hizo kwa niaba ya wazee waliopo ndani ya chama.

Ifahamike kwamba mfumo na muundo wa vyama vya siasa kiitikadi, vinabadilika kulingana na mabadiliko ya maumbile ya dunia kwa sababu ya uvumbuzi wa teknologia ya mawasiiano na mageuzi ya mfumo wa uchumi unaotegemea viwanda.

Itikadi ina  sura ya mtawanyo wa mawazo mapya kwa kadri dunia inavyobadilika jambo linalosababisha binadamu abadilike kifikra, kimtazamo na kimfumo.

Weledi wa historia wanabainisha kwamba tangu karne ya nyuma, itikadi imekuwa ikibadilika kulingana na mazingira yaliyopo kisiasa na kiuchumi. 

Itikadi ambazo zimeshuhudiwa tangu enzi za nyuma katika anga za siasa ni itikadi  kama vile; Itikadi ya ujima; Itikadi ya ukabaila; Itikadi ya ubepari; Itikadi ya ukomunisti na Itikadi ya sayanzi ya ushoshalisti.

Ninachotaka kusema ni kwamba hawa wazee waliojitokeza kukosoa chama chao (CCM) hadharani sijui walilenga mfumo gani wa itikadi ya chama ambayo walidhani imesababisha chama kukosa mwelekeo na haiba mbele ya Jamii.

Nionavyo, baadhi ya makada wazoefu na waliobobea kwenye taaluma ya sayansi ya siasa kama akina Ng’ombale Mwiru; Paul Sozigwa; Phillip Mangulla japo kuwataja kwa uchache, ambao bado ni makada watiifu na tegemezi wa chama hicho cha CCM, wangejitokeza hadharani kuwajibu hawa wazee wenzao (Kitine, Kaduma, Butiku) ili jamii ya kizazi kipya kiweze kuchambua mazuri na mabaya.

Vinginevyo propanganda zao zitaifikisha CCM mahala ambapo historia yake iliyoheshimika ya mataifa ya nje kwa kuwa mstari wa mbele katika ukombozi wa mataifa mengi barani Afrika itafutika kabisa.

Kwa maoni yangu, ningefarijika kuona kwamba wale wazee ambao walikuwepo tangu enzi za TAA, TANU hadi CCM, akina Ngombale Mwiru, huu ndio muda muafaka kwao kujitokeza hadharani.

Watoe elimu ya itikadi ya vyama vya siasa na maana ya siasa ya uchumi na maana ya siasa inayolenga jamii ili kizazi hiki kiweze kutofautisha na kuchambua makombora ya malalamiko yanayoelekezwa kwa chama tawala na serikali yake.

Inavyoonekana kwa hivi sasa, lawama nyingi dhidi ya chama tawala na serikali yake, zinatoka kwa makada wazoefu ndani ya chama chenyewe.

Hali hii inadhihirisha kwamba hawa wakosoaji wana agenda inayolenga makundi ndani ya chama. Kwa mantiki hii, ni vigumu kwa vijana wa kizazi kipya kujifunza siasa za karne ya nyuma kwas ababu wazee watangulizi wamejikita katika siasa za makundi.

Matukio mengi yaliyoshuhudiwa ndani ya CCM kama vile; falsafa ya kujivua gamba; Makundi yanayohasimiana ndani ya chama, kuonyeshana ubavu katika chaguzi ndogo zilizopita (Igunga na Arumeru Mashariki);

Makada wa chama kushupalia hoja ya wapinzani kuhusu ufisadi; makada kuumbuana hadharani; makada kuishambulia serikali yao hadharani, wabunge wa chama kukubali kusaini hoja ya kutaka kung’oa Waziri Mkuu ambaye ni mteule wa Rais niliyotaja.

Matukio haya yote niliyotaja yanaashiria ujenzi wa falsafa mpya ya kipuuzi ya “ubinasfi na unafiki.” Binafsi naamini kwamba CCM kimuundo na kimfumo bado ni nzuri.

Tatizo ni ubinafsi na uroho wa watu wake hususan baadhi ya wazee waandamizi wa enzi ya awamu ya kwanza na ya pili, ambao bado wanaota ndoto ya kutaka kurudi madarakani.

Nasema bila kumumunya maneno kwamba hawa wazee waliopo ndani ya chama huku wakiikosoa chama  wakiwa wangali ndani ya chama ni wasumbufu na kero kwa serikali ya awamu hii ya nne.

Kwa sababu wanataka kupandikiza mbegu za chuki ilihali wapate fursa ya kuwaweka watu wao madarakani.
Kutokana na tabia hii iliyoanza ya makada kutoa maoni yao bila kujali mipaka ya maadili ya chama, nimelazimika kuuliza swali kwamba Mzee Ngobale Mwiru yuko wapi”.

Nina maana makada wa aina ya Ngombale wangefaa nao wajitokeze kukemea maovu hayo ya kisiasa yanayofanywa kwa malengo ya kumvuruga mwenyekiti wa awamu ya nne ili chama kipasuke mikononi mwake.

Kama Ngombale aliweza kuweka msimamo wake hadharani kwamba katiba imekiukwa katika kikao cha Nec, sasa atashindwa nini kukemea wazee wenzake wanaopotosha maana ya itikadi ya chama na mfumo wa serikali.

Hizi ni chokochoko ambazo hazifai kuvumiliwa . Mbona enzi zao hawakupenda wakosolewe huku wakibana wanahabari na vyombo vyao.

Hakuna lililo jema kama kutunza historia ya nchi kwa manufaa ya kizazi kipya. Sidhani kwamba yupo Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye atakubali chama kimfie mikononi mwake.

Chama kikifa leo, watakaolaumiwa ni wazee akina Ngombale Mwiru kwa sababu hawakutumia taaluma na uzoefu wao kuwafunda, kuwalea kuwaelimisha na kuwarithisha kizazi kipya elimu ya siasa inayoenda na wakati uliopo.

Namwomba Mzee Ngombale Mwiru ajitokeze kuongoza jahazi ya wazee ndani ya CCM katika kuwafunda vijana wa kizazi hiki kujua nini faida na hasara ya kuvamia siasa za chuki, ubinafsi na mengine mengi yatakayoweza kuangamiza chama na historia nzuri ya nchi yetu katika ulimwengu wa siasa.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwenye simu namba 0713-399004 au 0767 399004.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles