Thursday May 5, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Pinda atambue kuwa Wakuu wa Wilaya, Mikoa hawawezi kujikana

23rd May 2012
Print
Comments

Akifungua mafunzo ya siku 10 kwa wakuu wa mikoa na wilaya mjini Dodoma juzi, Waziri Mkuu, Mziengo Pinda, aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa kujitenga na makundi ya kisiasa katika utendaji kazi katika nafasi walizokabidhiwa na umma.

Ingawa Pinda hakufafanua hasa ni makundi gani ya kisiasa ambayo yanaweza kumfanya mkuu wa mkoa au wilaya ashindwe kuwajibika vilivyo katika dhamana walizokabidhiwa, jambo lililowazi katika miaka ya sasa ni harakati za makundi ya kisiasa ya kusaka nafasi ya kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015.

Siyo siri tena, ni wazi kuwa kuna makundi yanaumana katika kuusaka urais kwa udi na uvumba, wapo watu wametajwa kwa majina, wengine wakikanusha kuwa na mipango ya urais ilhali wengine wakikataa kusema lolote katika harakati hizo.

Hata hivyo, kama wapo wanaokataa kusema lolote juuya harakati hizo au vipi, ukweli mmoja unabakia dhahiri kuwa CCM imekuwa majeruhi wa harakati za kuutaka urais. Watu wamehujumiana, wamechezeana rafu na kila aina ya fitina katika kujipanga kwa ajili ya urais mwaka 2015.

Ni katika kujipanga huko ndiko kumewafanya baadhi ya watu wanaopewa ukuu wa wilaya au mkoa kujisahau na kubadili majukumu yao kutoka ya kuwatumikia wananchi kuwa ya mawakala wa makundi maslahi katika kuusaka urais.

Katika mazingira ya namna hiyo kazi za umma hazifanyiki na kwa kweli hali inakuwa mbaya zaidi kwani huyo mkuu wa mkoa au wilaya ambaye amekwisha kuota makengeza hawezi kuona vitu katika mwanga mwangavu wa ukweli na hivyo kufanya maamuzi ya haki katika mambo mengi yanayofikishwa ofisini kwake.

Hata hivyo, pamoja na angalizo muhimu na zuri la Pinda juu ya wakuu wa wilaya la kujiepusha na makundi ya kisiasa, inaelekea alisahau kitu kimoja kwamba chama chake, CCM, kinawatambua wakuu wa wilaya kama makada wake. Katiba ya CCM inawataja wakuu wa wilaya kama makada wake, kwa hali hiyo ni viungo muhimu wa chama katika ngazi ya wilaya.

Katika mazingira kama hayo, na hasa kama tafakari ya kina ikifanywa juu ya uteuzi wa wakuu wa wilaya wenyewe, ukweli mmoja utadhihirika kuwa nafasi hizo zimekwisha kugeuzwa siku nyingi kutoka za kiutendaji na usimamizi wa maendeleo katika ngazi ya wilaya kuwa makada wa kuendesha harakati za kisiasa katika wilaya hizo kwa manufaa yao wenyewe au wakubwa wao, au watarajiwa wengine.

Tungali tuna kumbukumbu ya mvutano ulioibuka bungeni wakati wa marekebisho ya sheria ya kuunda tume ya kuratibu mchakato wa kukusanya maoni ya katiba mpya juu ya nafasi ya wakuu wa wilaya katika sheria hiyo. Bunge lilionekana wazi kuwa limegawanyika juu ya nafasi ya wakuu wa wilaya.

Wakati wabunge wote wa CCM waliosimama walitetea kuwako kwa wakuu wa wilaya, wabunge wa kambi ya upinzani, hususan Chadema, walipinga kwa kile walichosema viongozi hao hakika walikwisha kujivua wajibu wa kiserikali na kuwa makada wa chama zaidi katika utendaji wao.

Ingawa inawezekana kujengwa dhana kwamba kelele zilizokuwa zinapigwa na wabunge wa upinzani juu ya wakuu wa wilaya ni hofu ambayo haina mashiko, ukweli mmoja unabakia kusimama imara, kwamba CCM kwa tamaa ya kutaka tu kujirundikia watumishi wa umma wawatumikie bila kujua kuwa wanaathiri hata misingi ya kutenganisha shughuli za vyama vya siasa na serikali, pengine kwa kushindwa kutambua mapema kuwa tamaa hiyo inaweza kuleta madhara, wakuu wa wilaya walikwisha kuacha kazi ya kuwa mihimili ya serikali katika maeneo yao na badala yake wamekuwa mihimili ya chama.

Katika mazingira kama haya inakuwa ni vigumu sana kuona ni kwa jinsi gani wakuu wa wilaya na hata wakuu wa mikoa watatekeleza agizo la Pinda kwa kuwa kimsingi uteuzi wao unatazamiwa na chama tawala uwanufaishe.

Hii ndiyo inafanya wakuu wa  wilaya kujiona kuwa wanafaa zaidi kuwa ndani ya harakati za kisiasa wakitumikia makundi maslahi kwa matarajio ya kuja kulipwa fadhila baadaye, suala kuwatumikia wananchi hubakia kuwa la pili kwa umimu au pengine kutokuwako kabisa katika hesabu za uwajibikaji.

Tungetamani sana kama Pinda angelitambua hili na wakuu wa mikoa na wilaya wakapewa sharti jingine la kufanya kazi kuwa ni kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa. Hili likiwezekana taifa hili linaweza kuponywa na ugonjwa siasa unaotafuna kila kitu na kuiacha nchi katika ukiwa mbaya.

 
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles