Saturday Apr 30, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mnyika mashine kubwa

25th May 2012
Print
Comments
  Ambwaga Ngh’umbi kortini
  Dar yalipuka, abebwa juu juu
Mbunge wa Ubungo (Chadema),John Mnyika baada ya kushinda kesi jana

Mahakama ya Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesema kuwa ushindi wa Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, ni halali baada ya mlalamikaji Hawa Ngh’umbi kushindwa kuthibitisha madai ya kukiukwa sheria ya ushaguzi na kura hewa 14,854 ziliathiri vipi uchaguzi wa jimbo hilo.

Kadhalika, Mahakama hiyo imesema haiwezekani mlalamikaji ambaye alikuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuutupia upande wa walalamikiwa jukumu la kuthibitisha madai yake wakati jukumu hilo lilikuwa la kwake.

Hukumu hiyo ilisomwa jana mahakamani hapo na Jaji Upendo Msuya kwa muda wa saa 1:20 kuanzia saa 4:10 hadi saa 5:30 asubuhi alipohitimisha hukumu hiyo mbele ya umati wa wafuasi wa Chadema na CCM waliokuwa wamevaa sare za vyama vyao waliofurika ndani ya ukumbi namba moja wa Mahakama hiyo na nje ya ukumbi huo.

Akisoma hukumu hiyo kwa kuchambua ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, Jaji Msuya alisema Ngh’umbi alidai kuwa Mnyika alimkashifu kwamba ni fisadi na aliuza jengo la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mbele ya wananchi wakati akifanya kampeni Septemba 11, mwaka 2010.

“Shahidi huyo wa kwanza ambaye ni mlalamikaji katika kesi hii, aliieleza Mahakama kuwa kitendo cha kuitwa fisadi kwenye kampeni hizo kiliathiri wapiga kura kushindwa kumchagua… lakini ushahidi huo ni wa kuambiwa, Ngh’umbi hakuwepo eneo la tukio,” alisema Jaji Msuya huku akisikilizwa na wafuasi hao ambapo wengine walisikiliza kupitia spika zilizokuwa zimefingwa nje ya Mahakama hiyo.


Jaji aliendela kufafanua kwamba, shahidi wa pili upande wa mlalamikaji ambaye alikuwa wakala Robert Kondela (54), katika ushahidi wake alidai kuwa kashfa ya kumuita mlalamikaji fisadi iliyotamkwa na Mnyika siku hiyo ya kampeni katika viunga vya Ubungo River Side iliathiri kura za mlalamikaji kwa watu zaidi ya 500 kwa kuwa wangeweza kushawishiana.

“Ushahidi wa utetezi walijibu hoja hiyo kuwa Septemba 11, 2010 Chadema walifanya kampeni katika viunga vya Ubungo Msewe na sio River Side kama upande wa mlalamikaji walivyodai,” alisema Jaji Msuya.

Akifafanua kuhusu madai hayo, Jaji Msuya alisema hakuna shahidi mwingine aliyeweza kuthibitisha tuhuma hizo kati ya wananchi zaidi ya 500 wanaodaiwa kumsikiliza Mnyika eneo la River Side.

“Mahakama imeona katika madai hayo upande wa mlalamikaji umeshindwa kuthibitisha kama kuna watu walishindwa kumpigia kura Ngh’umbi kwa sababu ya kashfa za ufisadi wa kuuza jengo la UWT kama hati ya mlalamikaji inavyosema,” alisema Jaji Msuya huku akisikilizwa na umati mkubwa wa watu.

Kuhusu madai ya mlalamikaji kutosaini fomu ya matokeo, Jaji alisema hakuna shahidi mwingine aliyetoka nje zaidi ya wakala aliyekuwa katika chumba cha majumuisho, hivyo swali la ushahidi bila kuacha shaka halijajibiwa.

Pia alisema kutokusaini hakukuwa na athari yoyote bali mlalamikaji alitakiwa kujaza fomu ya malalamiko kwa mujibu sheria ya uchaguzi zilivyoelekeza.

Jaji Msuya alisema madai ya kutumia laptop za Mnyika na za Manispaa ya Kinondoni katika majumuisho bila kufanyiwa uhakiki na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), shahidi wa tatu aliyekuwa wakala wa jimbo hilo, Andrew Kishatu (46)  alitoa ushahidi bila kuungwa mkono na kwamba wengine walitoa ushahidi wa kuambiwa.

Jaji Msuya alifafanua kwamba mlalamikaji alikuwa na jukumu la kuthibitisha madai ya kuwepo kwa laptop ambazo hazikufanyiwa uhakiki, lakini hakuna ushahidi zaidi wa kuunga mkono ushahidi wa shahidi wa tatu.

“Haiwezekani kuutupia jukumu upande wa walalamikiwa kuthibitisha madai hayo, mlalamikaji alitakiwa kumuita Mkurugenzi wa Uchaguzi, Rajabu Kiravu aliyedaiwa kuruhusu laptop kutoka nje ya NEC kufanya majumuisho kwenye jimbo hilo na wengine ili mlalamikaji kuunga mkono ushahidi wa shahidi wake,” alisema.

Kuhusu kuzidi kwa kura hewa 14,854, Jaji Msuya alisema yalikuwa ni makosa ya kibanadamu na kwamba kila mgombea akiwemo Mnyika, idadi ya kura itabaki kama ilivyoorodheshwa katika fomu ya majumuisho.

Jaji alisema kwa kuzingatia ushahidi huo, bila kuacha shaka, mlalamikaji ameshindwa kuithibitishia mahakama kuhusu madai hayo, hivyo yanatupiliwa mbali.

“Kuhusu madai ya wafuasi wa Chadema kuzidi katika chumba cha majumuisho, madai hayo ni mazito, hivyo ilitakiwa mashahidi wengine zaidi ya yule wa tatu wa upande wa mlalamikaji ili kuithibitishia Mahakama madai hayo,” alisema Jaji Msuya huku akimalizia kufafanua madai ya msingi ya kesi hiyo iliyofunguliwa Desemba 2, mwaka 2010.

“Mahakama iko makini kuzingatia ushahidi kama huo uliotolewa na upande wa mlalamikaji... imeona madai ya mlalamikaji hayajathibitishwa, hivyo mlalamikaji anatakiwa kulipa gharama za kesi hiyo kuanzia mwanzo hadi hukumu iliposomwa,” alisema Jaji Msuya huku wafuasi wa Chadema waliokuwa wanasikiliza hukumu hiyo kupitia spika kushangilia wakisikika wakisema “people’s Power”.

MNYIKA: NAWASHUKURU WANANCHI WA UBUNGO


Akizungumza baadaye na NIPASHE alisema: “Nawashukuru wananchi wa Ubungo waliokuwa wakisali maombi na sala zao zimemuongoza Jaji kutoa haki katika kesi hiyo pamoja na kwamba wakati mwingine mahakama zetu huwa zinaingiliwa.”

Alisema ufisadi uliojitokeza katika uchaguzi huo umezidiwa na uadilifu, uwajibikaji na uaminifu na kwamba ushindi huo ni nguvu ya umma.

NGH’UMBI: NIMEKUBALI HUKUMU

Akizungumzia hukumu hiyo, Ngh’umbi alisema amekubaliana na maamuzi yaliyotolewa na mahakama na kwamba kwa sasa hana kitu cha kusema.

“Nawasihi wana-CCM kuwa watulivu na kukubaliana na hukumu ya mahakama… bado sijaamua chochote kwa sasa mpaka nikitulia,” alisema Ngh’umbi.


KAULI YA MBOWE

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema CCM wanakawaida ya kukimbilia mahakamani mara wanaposhindwa kwenye uchaguzi hata kama ushahidi hawana.

Alisema kesi za uchaguzi zinagharimu fedha nyingi sana kuziendesha pamoja na muda hivyo sheria isitumike vibaya.

“Chadema tunashukuru Mahakama imetoa hukumu ya haki kwa wakazi wa Jimbo la Ubungo kwa kuwathibitishia ushindi wa mbunge wao kwa mara ya pili… Mnyika ni mbunge wa kutumainiwa kwa chama na wananchi, tunathamini sana kazi zake,” alisema Mbowe.

HALI ILIVYOKUWA

Mapema jana saa 1:00 asubuhi NIPASHE ilishuhudia askari polisi waliovaa sare na wengine kiraia wakizungushia utepe kuzuia watu wasiegeshe magari yao katika maegesho yaliyokuwa mbele ya jengo la Mahakama Kuu.

Aidha, NIPASHE ilimsikia mmoja wa ofisa wa jeshi hilo akizungumza kwa simu kwamba: Ofisi yote imehamia Mahakama Kuu, hakuna mpelelezi hata mmoja hapo.”

 Kauli hiyo ilidhihirishwa na  idadi kubwa ya askari polisi waliokuwa wamezagaa nje na ndani ya Mahakama hiyo.

Hata hivyo, ilipofika saa 1:12 asubuhi, makundi tofauti ya wafuasi wa Chadema waliovaa sare za chama chao waliingia katika viunga vya Mahakama.

Lango kuu la kuingiliwa mahakamani hapo lilikuwa limefungwa huku likilindwa na askari hao na watumishi wachache wakiruhusiwa kuingia huku waandishi wa habari wakisubiri muda wa Mahakama kuanza shughuli zake.

Saa 3:00 watu waliofurika nje ya jengo hilo walifunguliwa geti na kuruhusiwa kuingia katika ukumbi namba moja kusikiliza hukumu hiyo.

Saa 3:10 Ngh’umbi aliingia mahakamani hapo akiwa na wafuasi wa chama chake waliovaa sare za chama hicho.

Hali ilibadilika gafla saa 3:26 asubuhi katika ukumbi huo uliokuwa na sehemu mbili ya chini na ya ghorofa ya kwanza, ulilipuka kwa vifijo baada ya Mbunge Mnyika kuingia ndani ya ukumbi huo huku wafuasi wa chama chake wakishangilia kwa kupiga makofi na kusema ‘People’s… na kuitikia Power’.

Hali hiyo ilidumu kwa dakika tano na utulivu ulichukua nafasi yake.

Saa 3:46 asubuhi, Mbowe aliingia kwenye ukumbi huo ambapo wafuasi wa chama chake walilipuka kwa kumshangilia, wakipiga makofi na miluzi huku wakisema ‘People’s… na kuitikia Power’ hali iliyodumu kwa dakika kati ya sita hadi nane.

Baada ya hukumu hiyo kumalizika kusomwa saa 5:30, wafuasi wa Chadema walimbeba juu juu Mnyika huku wakishangilia na kumpandisha kwenye gari lake kisha kuondoka katika viunga vya mahakama hiyo mara moja.

Desemba 2, mwaka 2010, Ngh’umbi alifungua kesi ya kupinga ushindi wa Mnyika. Wengine aliowalalamikia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, akidai kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 uliompa ushindi Mnyika haukuwa huru na haki na kwamba sheria zilikiukwa katika kumtangaza mbunge huyo kuwa mshindi.

Katika uchaguzi huo Mnyika alipata kura 66,742 wakati Ngh’umba alipata kura 50,544.

Kesi hiyo ilisajiliwa mahakamani hapo kwa namba 107/2010.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles