


.jpg)
Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen, amefurahi kuona baadhi ya wachezaji waliokuwa majeruhi wameungana na kikosi hicho katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Gambia, wa Kundi C la michuano ya awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika, wa kesho jijini.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Karume, Poulsen alisema amefarijika kumuona mshambuliaji wake Thomas Ulimwengu akiwa fiti na kufanya mzoezi na wachezaji wenzake.
"Kwanza nimefurahi kuona wachezaji majeruhi wameanza kurudi kwenye hali yao nzuri... Ulimwengu alianza mazoezi juzi na ameonekana kuwa fiti," alisema.
"Hii ni hali nzuri kwetu... tuko tayari kwa pambano letu Jumapili."
Alisema kuwa Nurdin Bakari naye ameanza mazoezi mepesi japo hana uhakika kama atakuwa fiti kesho kuwakabili Wagambia hao.
Kikosi cha Gambia (The Scorpions) kiliwasili nchini juzi usiku kwa ajili ya mchezo huo kwenye Uwanja wa Taifa.
Stars ilianza vibaya michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 2-0 na Ivory Coast mwishoni mwa wiki iliyopita hivyo kushika mkia wa kundi lake.
Gambia ilitoka sare ya bao 1-1 na Morocco, kigogo kingine cha Kundi C hivyo kwa pamoja zinashika nafasi ya pili.
Ni timu moja tu katika makundi 10 ya michuano ya awali itasonga mbele kucheza hatua ya tatu ya mtoano kupata wawakilishi watano wa Afrika kwa ajili ya fainali za mwaka 2014 nchini Brazili.
Wakati huo huo, tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa leo kwenye vituo tofauti jijini Dar es Salaam kwa bei ya Sh.3,000, 5,000, 10,000 na Sh.20,000. Jukwaa la VIP A viingilio vimepangwa kuwa Sh. 30,000.