Tuesday May 3, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Ripoti sakata la Blandina Nyoni yatua kwa JK

6th May 2012
Print
Comments
Blandina Nyoni

Ripoti ya uchunguzi dhidi ya sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa, imetua kwa Rais Jakaya Kikwete ikisubiri kutolewa maamuzi.

NIPASHE Jumapili ilibaini kuwa tayari ripoti hiyo imeshawasilishwa Ikulu ili Rais aweze kutolea tamko juu ya sakata hilo.

Akiithibitishia NIPASHE Jumapili, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu, Peter Ilomo, alisema kuwa tayari wameshapatiwa ripoti hiyo.

Alisema Rais Kikwete ndiye mwenye maamuzi katika suala hilo na kwamba alitaka kutolea tamko hivi karibuni lakini kutokana na muingiliano wa mambo ameshindwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, alisema yeye sio msemaji wa Rais, anachokifahamu ni kuwa ripoti imewasilishwa kwa mheshimiwa mwishoni mwa mwezi Aprili, mwaka huu.

Alipoulizwa kama ana taarifa juu ya kutolewa kwa ripoti hiyo, Ilomo alisema kwa kuwa Rais Kikwete alikuwa katika wakati mgumu, hivyo anategemea akishawaapisha mawaziri hao ndipo atatolea tamko juu ya suala hilo.

Januari, mwaka huu madaktari walifanya mgomo kwa lengo la kuishinikiza Serikali kutimiza madai yao nane ikiwemo nyongeza ya posho ya mazingira hatarishi, posho ya muda wa ziada wanapokuwa kazini, kupatiwa nyumba, usafiri, kadi ya bima na pia kupatiwa vitendea kazi pamoja na dawa ili waweze kufanya kazi katika mazingira bora.

Mgomo huo ambao ulisababisha vifo uliendelea mpaka Februari 8, mwaka huu ambapo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alikutana nao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ili kujadili suala hilo na kuhakikisha analimaliza.

Awali kabla ya Pinda kukutana nao tayari walishawasilisha malalamiko ya kutaka viongozi wa Wizara ya Afya waondolewe kwa kuwa wameshindwa kusikiliza madai ya madaktari na kusababisha suala hilo la mgomo kuendelea bila kulidhibiti.

Hata hivyo, walidai kuwa Blandina Nyoni amekuwa ni kikwazo kikubwa katika wizara hiyo na pia amekuwa akiitumia ofisi hiyo kwa ajili ya maslahi yake binafsi bila kutekeleza changamoto zinazowakabili na hata anavyoambiwa jambo fulani hutoa majibu ya dharau.

Mbali na madaktari kueleza kujibiwa majibu mabaya pia walieleza Nyoni amekuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali katika wizara hiyo.

Mbali na tuhuma hizo za Nyoni anadaiwa na tuhuma mbalimbali 18 za ufisadi katika wizara hiyo.

Wakati huo huo, Ilomo amesema ucheleweshaji wa uteuzi wa wakuu wa wilaya katika baadhi za wilaya linafanyiwa kazi na kwamba mara baada ya Rais kuwaapisha mawaziri kesho (Jumatatu) litafuatia suala la wakuu wa wilaya.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles