Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Viatu vya Hall ni vikubwa Azam

4th August 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Klabu ya Azam ambayo ni moja ya timu zilizokua kwa kasi ndani ya muda mfupi tangu kupanda daraja la ligi kuu nchini, wiki hii imekatisha mkataba na kocha aliyeipa mafanikio yake makubwa zaidi tangu mwaka 2007.

Azam ambayo inatoka kushika nafasi ya pili kwenye ligi kuu ya Bara na Kombe la Kagame la klabu bingwa ya soka ya Afrika Mashariki na Kati, imevunja mkataba na Stewart Hall na mwalimu huyo anarejea nyumbani Uingereza.

Kinachofuata?
Taarifa ya Azam ya wiki hii pia imesema walimu kadhaa wa ndani na nje wamejitokeza kuomba kazi ya kufundisha timu hiyo.

Ni wazi kwamba kutokana na mafanikio iliyoyapata na rasilimali za kutosha za kampuni mama ya klabu hiyo ya Azam, timu itapata taabu inayokaribishwa katika mchakato wa kutafuta mrithi wa Hall.

Makocha wengi wenye viwango vya juu vya taaluma ya ufundishaji soka toka nje ya nchi watajitosa katika mchakato huo wa kutafuta mwalimu mpya, na tungependa kuchukua nafasi hii Nipashe kuikumbusha klabu ya Azam kuwa viatu vya mwalimu aliyepita ni vikubwa kwa wengi kati ya waombaji wa kazi hiyo waaotarajiwa.

Itakuwa kazi ngumu sana kwa kocha anayekuja angalau kutetea
nafasi ya pili katika ligi ambayo historia inaonyesha kutawaliwa na Simba na Yanga tu.

Simba ambayo ndiyo bingwa wa msimu uliopita itatoa upinzani mkali katika si tu kutetea kiti hicho bali pia kuhakikishia angalau, basi, haikosi uwakilishi wa nchi katika michuano ya klabu ya Afrika.

Katika ligi ambayo timu mbili tu za kwanza zinakata tiketi ya kucheza Afrika msimu unaofuata, Yanga ambayo 2011-2012 ilishika nafasi ya chini zaidi ya ligi kuu ya Bara kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1988 itapenda kuonyesha ni mgogoro wa uongozi ulioifanya ichemke vibaya, na imeshaanza kutimiza hilo.

Yanga iliifunga Azam mabao 2-0 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame ikiwa ni mara ya kwanza baada ya Jangwani kupokea vipigo vinne mfululizo ndani ya mwaka mmoja kutoka kwa timu hiyo ya watengeneza vyakula.

Ni mazingira magumu kuishi kwa timu ambayo ni ya tatu kwa umaarufu nchini kwa sasa. Hivyo mbali na uwezo wa kufundisha, uzoefu wa mwalimu katika kujenga kikosi kinachojiamini kwamba kitaendeleza umwamba wake chini ya Hall itatakiwa kuwa sifa ya kwanza kwa kocha mpya.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment