


Vurugu zisizotarajiwa zimefanyika kisiwani Unguja, ndani ya ardhi ya Zanzibar. Mali zikiwemo nyumba za ibada na misa takatifu, zimechomwa moto! Inakera, haistahili.
Sababu za vurugu hizo, pamoja na mambo mengine ni kile kinachotajwa kama vuguvugu la kuukataa mchakato wa kuwepo Katiba Mpya, kwamba Zanzibar haipaswi kuwa sehemu yake.
Kikundi cha watu wenye haki kama raia wengine, kimeibuka na kudai Zanzibar ni nchi huru, ina Katiba yake, ina Rais wake, ina serikali yake, ina majeshi yake, ina bendera yake ya taifa na vigezo vingine vingi.
Wanaoshiriki vuguvugu hilo wanadai kuwa Zanzibar ina kila sifa ya kuwa nchi huru isiyohitaji kuwa sehemu ya Muungano, wanataka wajitenge!
Wabaki kuwa Wazanzibar na Zanzibar yao, hivyo kuweka ufa katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Hilo likifanikiwa, Tanzania haitakuwepo katika ramani ya dunia. Itafutika.
Kwa mujibu wa Katiba iliyopo, hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa ni uhaini. Kuifuta nchi huru inayotambulika kwa mujibu wa sheria za nchi na zile za kimataifa, ni kosa la jinai. Halistahili kuvumilika.
Kwa upande mwingine, wanaodai Zanzibar ijitenge kutoka katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanafanya hivyo kwa lengo la kuwasilisha matamanio yao, hisia zao, fikra zao na mawazo yao.
Kwamba katika kutafakari, wamebaini kuwa Zanzibar haipaswi kuwa sehemu ya Muungano, bali ijitenge. Ndivyo wanavyowaza, ndivyo wanavyofikiri na ndivyo wanavyotamani. Ni mtazamo tu hata kama utaonekana wa kijinga.
Inapochukuliwa kwa mtazamo huo, wanaotoa madai hayo wana ajenda inayopaswa kusikilizwa, kuchambuliwa, kufanyiwa tathmini na baadaye ijulikane kama ina mashiko ama ni mbio zinazochochewa na mahafidhina wa vurugu.
Katika kuitafakari hoja hiyo, binafsi ninaamini kwamba walioitoa wanastahili pongezi na si kupigwa, kukamatwa, kuwekwa rumande ama kufanyiwa unyanyasaji wa aina yoyote.
Ni raia waliotumia haki zao za kiraia kuwasilisha ujumbe wa kile wanachokisimamia, hata kama hakina maana kwa jamii pana. Upeo wao umejikita hapo…Zanzibar ijitenge!
Kwa maana nyingine, wanaodai Zanzibar kujitoa kwenye Muungano hawashinikizi, wanahitaji jawabu litakalokidhi haja, nia na matamanio yao. Kwamba Zanzibar ijitoe, iwaache Wabara na eneo la kijiografia lisilovijumuisha visiwa vya Unguja na Pemba!
Pamoja na kuwapongeza kwa ujasiri wa kujitokeza na kutumia haki zao za msingi kuidai ‘Zanzibar yao’, kuna jambo moja ambalo kikundi hicho, kama kingeshawishi kwa nguvu stahiki na ikadhihirika hivyo machoni pa umma na jumuiya za kimataifa, wangesaidia kufikia malengo yao.
Hapa ieleweke wazi kwamba si nia yangu kuwachochea wafikie hatua hiyo, lakini kwa mtazamo huru, ninaamini kwamba, hili ninalotaka kulijadili, linaweza kuchochea uhalali wa madai ya kutaka wao wajiite ‘Wazanzibar” na wale wajiite ‘Wabara’-pasiwepo na Muungano.
Na ninawazungumzia Wazanzibar kwa sababu, hoja ya kutaka kujitenga imetamkwa huko, haipo upande wa Bara, ipo Zanzibar ikiibuliwa na Wazanzibar ingawa kwa uchache katika hesabu yao.
Kama kikundi kinachodai Zanzibar kujitenga na Bara kina dhamira safi, ninakishauri kifuate sheria na taratibu zilizopo.
Lakini zaidi, ili kiungwe mkono zaidi na zaidi, kiisifanye Zanzibar kuwa ngome ya harakati hizo, kwa maana huku wapo raia wanaoendelea kuusihi Uzanzibar, wakifanya shughuli zao, wakimiliki mali na kujihusisha na maendeleo yao.
Kama kikundi hicho kinataka kuongeza uzito wa madai yao, kijipange kimkakati, kifanye sensa ya kuwatambua Wazanzibar wanaoishi, kufanya kazi ama biashara upande wa Bara.
Wazitambue mali wanazomiliki na mahali wanapotoka huko Visiwani. Wawatambue kwa kuwaorodhesha majina yao, mali zao, makazi yao na kila aina ya vitegauchumi wanavyovimiliki.
Wakishawatambua, wazungumze nao kwa lugha ambayo wataikubali, kwamba Muungano hauwafai Wazanzibar, hivyo kusudio la kutaka kujitenga kwao, litekelezwe.
Wakikubaliana hilo, Watanzania wa Zanzibar wanaoishi na kufanya kazi ama biashara upande wa Bara, waisusie Bara.
Waonyeshe kwa vitendo vya dhahiri kwamba Bara haiwafai, warejeshe leseni za biashara zao, warejeshe ama kuuza mali kama nyumba walizozijenga na kuishi na familia ama ndugu zao.
Isiishie hapo, wanaotaka kuitenga Zanzibar kutoka kwenye Muungano, wawashawishi Wazanzibar waliopo Bara, wafute kila aina ya uhalali unaowafanya kuwepo huko, badala yake warejee Unguja na Pemba, na kusema ‘tunaitaka Zanzibar yetu’.
Ninaliona hili kama hatua muhimu ya kuchagiza kasi ya kudai Zanzibar inayotaka kutengwa kutoka kwenye Muungano kwa sababu, hali ilivyo sasa haitoi ishara kwamba lililoibuliwa ni hitaji la Wazanzibar walio wengi.
Inavyojulikana na kudhihirika hata sasa, Wazanzibar walio wengi wananufaika na Muungano kwa maana pana kuliko inavyoelezwa na wanaotaka kujitenga.
Ukiacha sababu za kiulinzi na usalama, Muungano umetoa fursa pana kwa Wazanzibar kutanua shughuli za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hilo lipo hata kwa Wabara waliopo Zanzibar.
Ni ukweli usiofichika kwamba wapo watu wa kada tofauti waliowahi kuzungumzia haja ya Zanzibar kujitenga na kujiondoa kwenye Muungano. Miongoni mwao ni wanasiasa hususani walio katika uwakilishi wa umma.
Lakini sehemu kubwa ya wazungumzaji wanaohitaji Zanzibar ijitenge ndio wanaonufaika wakubwa wa Muungano uliopo. Wanamiliki biashara kubwa kwenye mikoa mingi katika Muungano, wana makampuni yanayofanya biashara kubwa pande zote za taifa hili.
Wanaonufaika na Muungano wanamiliki mashamba, nyumba za kupangisha na biashara nyinginezo. Si rahisi kuwakuta maeneo kama Kojani kule Pemba, ambapo eneo lake ni dogo ikilinganishwa na idadi ya wakazi wake, achilia mbali wale waliopo nje ya kisiwa hicho.
Kwa maana hiyo, sababu za kiuchumi, mahusiano, ulinzi na usalama wa maisha na mali za kila raia, vinapaswa kupewa wigo mpana katika kuwasilisha hoja, ili kuushawishi ulimwengu kwamba Zanzibar ipo katika hitaji la kujitoa kwenye Muungano.
Vinginevyo, hekaya hizo zinatoa taswira ya uchochezi na vurugu za walio wachache, tena kwa maslahi binafsi ama ya ‘walio nyuma’ ya mpango huo, wakitaka kuuaminisha umma kwamba Zanzibar inatakiwa kujitenga.
Tufikirie kwa pamoja, tuchukue hatua kwa pamoja ili Tanzania yenye amani na utulivu, iendelee kuwa mahali salama pa kuishi.
Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kwenye simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe: mgeta2000@yahoo.com