Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Wanne kizimbani kujeruhi wana-Chadema

16th May 2012
Print
Comments
Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa

Watu wanne, wakimemo watoto watatu wa Diwani wa Kata ya Nduli (CCM) katika Manispaa ya Iringa, Idd Chonanga, wamepandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kuwajeruhi kwa mapanga wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini hapa.

Katika mkutano wa hadhara wa Chadema, uliofanyika eneo la Nduli,Jumapili ya wiki iliyopita kwa ajili ya kuwapokea wanachama wapya 90 waliokihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chadema, washitakiwa hao wanadaiwa kuvamia mkutano uliokuwa ukihutubiwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa, na kuwashambulia watu watatu.

 Waliopandishwa kizimbani ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Usumamizi wa Fedha (IFM), Alex Chonanga (23); mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Juhudi, Meshack Chonanga (20); Greyson Chonanga (31) na Mussa Mtete (25), wote wakazi wa Manispaa ya Iringa.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, Mei 13, mwaka huu katika eneo la Nduli, Manispaa ya Iringa kwa kuwajeruhi watu watatu ambao ni Seleman Komba, Peter Msele na Oscar Sanga.

Akisoma kesi hiyo ya jinai namba 97 ya mwaka 2012, mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Iringa, Festo Lwila, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Prosper Ng’oro, aliiambia Mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa matatu ya kujeruhi ambayo ni kinyume na kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16.

“Watuhumiwa wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa makosa matatu ya kujeruhi, kinyume na kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002,” alidai.

Baada ya kusomwa kwa maelezo ya upande wa mashitaka, Hakimu Lwila aliwahoji watuhumiwa hao kama wanakubaliana na maelezo hayo, ambapo wote walikana.

Muda mfupi baadaye, Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali, alisimama na kumwomba Hakimu Lwila kuzuia dhamana ya watuhumiwa hao kwa madai kuwa majeruhi wa tukio hilo wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na hali zao ni mbaya.

Kesi hiyo,imeahirishwa hadi Mei 29, mwaka huu itakapotajwa tena na watuhumiwa walirejeshwa mahabusu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles