Thursday May 23, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Yanga walikoroga kwa Yondani

8th June 2012
Print
Comments
Beki wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, Kelvin Yondani

Beki wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, Kelvin Yondani, huenda akakumbana na adhabu ya kufungiwa kucheza soka kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja endapo itabainika kwamba amesaini mara mbili, imefahamika.

Mbali na adhabu hiyo, pia klabu ya Yanga kupitia Afisa Habari wake, Louis Sendeu juzi alisema kuwa mchezaji huyo ni wao, nayo huenda ikakumbana na adhabu ya kufungiwa kusajili kwa kipindi cha miaka miwili pamoja na faini.

Pia kanuni za ligi zinaeleza kuwa kiongozi ambaye alihusika katika kumsajili mchezaji atafungiwa kujishughulisha na soka kwa kipindi kisichopungua miaka miwili.

Jana mchana Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema kuwa klabu yake inajipanga kufikisha malalamiko yake FIFA huku akisema kuwa Yondani ni mchezaji wao halali.

Rage alisema kuwa Simba ilisaini mkataba mpya na beki huyo Desemba 23 mwaka jana baada ya kufahamu kwamba mkataba aliokuwa nao ulitarajiwa kumalizika Mei 31 mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema pia beki huyo alifanyiwa uchunguzi wa afya Desemba 17 mwaka jana chini ya usimamizi wa daktari wa Simba, Cosmas Kapinga na wakati anasaini mkataba mpya, wakili Allan Maduhu alikuwa ni shahidi wa klabu.

"Tutaishitaki Yanga kwa kufanya udanganyifu, tunataarifa kwamba Yondani alitolewa kwenye kambi ya Stars na kwenda kusaini mkataba huo na picha inaonyesha amevaa jezi zenye nembo ya Kilimanjaro ambazo Stars imeanza kuzitumia mwezi jana (Mei)," Rage alieleza.

Alisema kuwa Yanga iliwahi kuwafuata kwa ajili ya mazungumzo ya kumsajili beki huyo lakini walishindwa kutoa dau waliloambiwa na hivyo Simba iliamua kumpa mkataba mpya kwa sababu bado inamuhitaji katika kikosi chake.

"Tunapeleka malalamiko FIFA ili kukomesha wale wanaotaka kuutia aibu mpira wa miguu, wanaweweseka na kipigo cha bao 5-0 tulichowapiga," aliongeza Rage.

Alisema pia atamshitaki Seif Ahmed 'Magari' ambaye ameonekana akishuhudia zoezi la Yondani akisaini mkataba huo wakati kwa sasa si kiongozi halali wa Yanga baada ya kuwasilisha barua ya kujiuzulu hivi karibuni.

Mkataba wa awali ambao juzi uongozi wa Yanga uliuonyesha ulikuwa na makosa mbalimbali ikiwemo tarehe ya kuzaliwa ya beki huyo ambayo ilionyesha kwamba amezaliwa Oktoba 9 mwaka 1994 badala ya 1984 iliyoko kwenye fomu za Simba za mchezaji huyo.

Wakati huo huo, Yondani, amekalia kuti kavu katika kikosi cha Stars baada ya kochaKim Poulsen kubaini kwamba nyota huyo alitoroka kambini juzi usiku.

Habari kutoka katika kambi hiyo zinasema kuwa Yondani aliomba ruhusa ya kutoka lakini alikataliwa na hivyo aliamua kutoroka na baada ya muda Kim alipata taarifa hizo na kuamua kukaa mapokezi kwenye hoteli ya Tansoma akimsubiri beki huyo.

Taarifa zinaeleza kwamba Kim alimuweka kitimoto beki huyo tangu juzi na jana mchana lakini ameshindwa kumuondoa kutokana na tatizo la mabeki alilonalo hasa baada ya Aggrey Morris, kupewa kadi nyekundu huko Ivory Coast.

Uongozi wa Yanga umesisitiza kuwa mchezaji huyo ni mali yao baada ya kusaini fomu hizo za usajili wa mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh. milioni 30.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment