Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Tumimine misaada kwa Twiga Stars

26th May 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, ipo nchini Ethiopia ambako kesho itaingia uwanjani kutafuta nafasi ya kucheza fainali za pili mfululizo za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya wenyeji hao.

Twiga Stars ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa fainali hizo baada ya dakika angalau 180, katika kizingiti chake cha mwisho hicho ambacho ni timu ambayo si tishio katika soka la wanawake barani.

Aidha, kwa mujibu wa nchi za Afrika Kusini na Malawi, Twiga Stars ni timu ambayo huzipa ushindani wa hali ya juu timu zao ya taifa za wanawake kila zinapokutana na ndiyo sababu, kwa mfano, zilisafiri kuja nchini kucheza mechi za kirafiki katika wiki mbili zilizopita.

Ni mafanikio yaliyovuka mipaka, ya Twiga Stars, hasa ukizingatia kuwa yanakuja huku nchi ikiwa haina msingi wa maendeleo wa soka la jinsia hiyo.

Hakuna vituo vya kutambua na kukuza vipaji vya wacheza soka wanawake, inafahamika.

Hakuna ligi ya taifa ya wanawake kutokana na kutokuwepo kwa ligi za madaraja ya chini, inafahamika.
Twiga Stars hufanya maandalizi ya 'kitoto' kutokana na timu hiyo kutokuwa na mdhamini, inafahamika pia.

Ndiyo maana tulifarijika sana, Nipashe, wiki hii baada ya kampuni za SBL na NMB kutoa shilingi milioni 30 na vifaa kwa Twiga Stars ili kusaidia ushiriki wa kizingiti cha mwisho kwa timu ambayo haijawahi kupata mdhamini mwingine tangu kampuni ya RBP Oil Industries 'ibipu' miaka miwili iliyopita, kabla ya fainali za Afrika Kusini.

Ukizingatia kuwa Taifa Stars pamoja na kuwezeshwa kwa mabilioni ya shilingi katika miaka ya karibuni haijawahi kurudia mafanikio ya kikosi cha ridhaa cha mwaka 1980, kuna kila sababu ya Twiga Stars kupigiwa debe la nguvu ili misaada ya aina ya kampuni za SBL na NMB izidi kumiminika kwayo kwani inalipa.

Inalipa kuisaidia Twiga Stars, Nipashe tunaona, kwasababu ni timu ambayo haihitaji nguvu kubwa sana kifedha kutokana na, kwanza, inaelekea kujenga tabia ya kufika fainali za kimataifa kila inaposhiriki michuano hiyo sasa.

Pia, inalipa kuisaidia Twiga Stars kwasababu soka la wanawake halina michuano ya kucheza mpaka kwa miaka miwili ya kalenda kama michuano ya awali ya wanaume ilivyo hivyo kutogharimu sana.
Tumesikia, Nipashe, kauli ya NMB kwamba imefungua akaunti maalumu kwa ajili ya michango ya kuisadia Twiga Stars kifedha.

Lakini tuna wasiwasi, Nipashe, kama shirikisho la soka, TFF, ambalo bado lina wajibu wa kubeba majukumu ya uendeshaji wa timu hiyo kutokana na chama cha wanawake nchini kuwa kichanga mno bado, limesikia tangazo hilo la kufaraji la benki hiyo.

Hivyo ni fursa kwa TFF sasa, Nipashe tunaona, kuhamasisha wapenzi wa mchezo huo (makampuni yakiwemo), kuchangia walichonacho kwa ajili ya si tu fungu la kusaidia Twiga Stars endapo itacheza fainali kama ambavyo wengi tunataraji bali pia: Kuchangia akaunti hiyo ili fedha zitakazopatikana zitumike kama kasma endelevu ya kusaidia kuinua maendeleo ya soka ya wanawake kwa ajili ya kupata timu bora zaidi ya taifa ya wanawake.
 

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles