


.jpg)
Nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Juma Kaseja, amesema kuwa kikosi cha timu hiyo kinachoondoka nchini leo alfajiri na kuelekea jijini Abdijan kucheza dhidi ya wenyeji Ivory Coast, kinakwenda huko kupambana ili waweze kupata ushindi na kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2014 huko Brazil.
Akizungumza jana jijini baada ya kukabidhiwa bendera ya nchi, Kaseja alisema kuwa wamefanya maandalizi mazuri na kila mchezaji anajiamini kwamba atacheza kwa juhudi ili kuwafurahisha Watanzania ambao wana hamu ya kuona timu yao inapata mafanikio.
Kaseja alisema kuwa licha ya mchezo huo kuwa mgumu wanawaomba wapenzi wa soka wawaombee dua ili waweze kutimiza malengo ya kupata ushindi.
"Tumejiandaa vizuri, tunakwenda huko kupambana, tutapambana sana ili tupate matokeo mazuri, tunawaomba mtuombee dua ili tuweze kushinda," Kaseja alisema.
Kocha wa timu hiyo, Kim Poulsen, alisema kuwa wachezaji wake wako tayari kwa mchezo huo na wanajiamini kwamba wanaweza kuibuka na ushindi licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali kutoka kwa wapinzani wao.
Kim alisema kuwa kukutana na wachezaji wenye majina makubwa peke yake ni hali inayoongeza changamoto ya mchezo huo lakini wao wamejiandaa kuwakabili kitimu na si kutumia vipaji binafsi.
"Wachezaji wana nidhamu, wamefanya mazoezi kwa nguvu, tuko tayari, naahidi kwamba tutacheza soka la kiwango cha juu," alisema kocha huyo raia wa Denmark.
Aliongeza kuwa wachezaji wote wanajiamini na wanafahamu sababu ya wao kuwepo kwenye kikosi hicho.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni, Amos Makala, aliwataka wachezaji wa timu hiyo wakacheze kwa bidii ili kutunza na kulinda heshima ya Watanzania.
Makala alisema kuwa wakafanye vizuri zaidi ya kile walichokionyesha wakati wa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi na wasirudi na visingizio vya hali ya hewa au walifanyiwa hujuma nje ya uwanja.
"Mafanikio yana rafiki wengi, matatizo ni mtoto yatima," Makala aliwaambia wachezaji wa Stars akimaanisha kwamba ushindi ndio utakaowavuta zaidi wadhamini.
Aliwataka wajiamini na kujiona kwamba wanakwenda kuivaa Ivory Coast na si timu za Manchester City au Chelsea ambazo wanatoka baadhi ya nyota watakaokutana nao huko.
Wachezaji wote walioitwa na kocha huyo wataondoka isipokuwa mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayecheza timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kiungo wa Yanga, Nurdin Bakari ambao ni majeruhi.
Kiongozi wa msafara wa Stars ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Crescentius Magori na kwa upande wa Zanzibar, ni Makamu wa Rais wa Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA), Haji Ameir Haji.
Stars itarajea nyumbani Juni 5 mwaka huu saa 1:40 asubuhi na kuingia moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Gambia itakayofanyika Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.