Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Mvua yaleta maafa familia 36 zakosa makazi Moshi

7th May 2012
Print
Comments
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonadas Gama

Kaya 36 katika kijiji cha Chekereni wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro hazina makazi kufuatia mvua kubwa zilizonyesha wilayani humo na wilaya ya Rombo.

Mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa nyumba na barabara pamoja na makalivati pamoja na barabara ya Himo/Tanga kufungwa kwa saa kadhaa kupisha maji yapite.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Mkuu wa wilaya ya Moshi, Musa Samizi alisema mvua hizo zilianza kunyesha majira ya 5:00 usiku wa kuamkia jana katika maeneo ya Mwika, Marangu, Kilema pamoja na wilayani Rombo.

Alisema nyumba 36 zimebomoka kabisa na kwamba nyumba 27 zimeharibika kwa kujaa maji pamoja na mazao ya wananchi hao kuchukuliwa na maji.

Samizi alisema mvua za namna hiyo ziliwahi kunyesha na kuleta maafa kama hayo kwa mara ya mwisho mwaka 1947 na kwamba serikali mkoani humo imejipanga kwaajili ya kuwatembea wakazi wa maeneo hayo na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo chakula.

Aidha samizi alisema kuwa mvua hizo zimeleta madhara makubwa katika vitongoji viwili vya Darajani na Pabulike ambapo wakazi wa maeneo hayo wanahitaji msaada wa haraka wa chakula.

“Kwa sasa wananchi hao hawana kabisa makazi hivyo ninatoa wito kwa taasisi binafsi pamoja na wadau wengine kutoa misaada mbalimbali ikiwemo chakula ili kuwasaidia waathirika hawa,” alisema Samizi.

Wakizungumza na NIPASHE kutoka katika eneo la tukio wananchi wa kijiji hicho, Anna Kessi pamoja na Ibrahimu Mushi walisema kwa sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosa malazi pamoja na chakula kutokana na mali zao na mazao yao kuchukuliwa na mafuriko hayo.

Walisema wanaiomba serikali kwa hali na mali pamoja na wasamaria wema kujitokeza na kuwasaidia i kutokana na kwamba kwa sasa hawana uwezo wowote wa kifedha kwaajili ya kununua vitu mbalimbali na kujitimizia mahitaji yao.

Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, alithibitisha kutokea kwa maafa hayo na kusema kwamba hayakuwa kwa madhara ya binadamu.

Jana Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonadas Gama, aliwatembelea waathirika hao na kuwapa mifuko 50 ya saruji pamoja na Sh. milioni moja.

Gama ameahidi kutuma wataalam watakaofanya tathmini juu ya mahitaji mengine muhimu.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment