


Mitafaruku mingi katika jamii husababishwa na kukiuka maadili, lazima tukubali kuwa sehemu kubwa ya adhabu zinazotolewa katika mahakama mbalimbali nchini hutokana na makosa yanayosababishwa na watuhumiwa kukosa maadili.
Maadili ni utaratibu wa maisha unaokubalika katika jamii na ambao unaipeleka jamii katika hali ya maelewano mazuri pamoja na maendeleo endelevu. Maadili pia ni mfumo unaosababisha kila binadamu kupata mahitaji yake muhimu kihalali, mfumo huu lazima ulindwe na mfumo wa kisheria.
Hivi karibuni kulijitokeza mjadala wa wasomi wakijadili kuhusu nafasi ya maadili katika kuijenga jamii bora, majadiliano hayo yalinivutia kiasi kikubwa na kuona nichangie kwa jamii yetu kupitia makala hii ili tuweze kubadilishana uzoefu katika dhana hii ya 'maadili'.
Yapo makundi makubwa mawili ambayo yanahusika na taswira nzima ya maadili, wapo vijana pamoja na wazee, wote kwa pamoja wanawajibika katika kujenga maadili mema yanayoweza kuliletea taifa sifa njema na kuendeleza utamaduni wa kihistoria ya Mwafrika.
Maovu mengi yanatokana na ukiukwaji wa maadili, wizi, rushwa, ugomvi, ufisadi, ubinafsi pamoja na maovu mengine yanatokana na kukosa maadili. Mtu anaamua kufanya uovu kama njia pekee ya kujipatia mahitaji ili kukidhi moyo wake, kila binadamu anayo mahitaji ya kibaolojia ambayo kama akiyakosa anaweza kuathirika, mahitaji kama chakula, malazi, matibabu n.k
Wakati anaposhindwa kuyapata mahitaji hayo, huamua kuiba, kitendo hicho hufanyika kama hatua ya mwisho ya kulazimisha upatikanaji wa hitajio lake, na kitendo hicho husukumwa na dhamira yake baada ya kukosa maadili.
Zipo taasisi maalumu za kulinda na kuhakikisha kuwa maadili yanafuatwa, wazazi na walezi wa watoto ni kundi la kwanza la kujenga maadili, watoto wanapoelimishwa mambo mazuri ya kufanya, ikiwa ni pamoja na kuheshimu wakubwa, kusaidia wazazi, kushiriki katika kazi za kijamii nk. kunampa mtoto akili ya kuona anayo sehemu kubwa ya kuwajibika katika jamii.
Ni dhahiri kuwa kadri mtoto anavyoendelea kukua, heshima na adabu kwa wanajamii inakuwa kubwa na yenye kuheshimu maadili na malezi aliyopata. Yapo majukumu kadhaa kwa wazazi ya kumjengea maadili mema kuanzia utoto hadi akifikia umri wa kujitegemea.
Pamoja na jukumu hilo kubwa na muhimu kwa wazazi, walimu pia ndio wanaowajibika zaidi, vijana wanakuwa katika umri unaohitaji uangalizi wa ziada kwa kuwaelekeza katika tabia na mwenendo sahihi unaojali maadili mema kusudi awe raia mwema baadaye.
Ndio maana katika awamu hii walimu hupewa uwezo wa kutoa adhabu kwa makosa mbalimbali ili wanafunzi watambue umuhimu wa kufuata maadili mema yanayotolewa na walimu, mengi kati ya hayo huwa ni mwendelezo wa malezi ya wazazi wao.
Yamkini ipo tofauti kubwa ya maadili ya wanafunzi wa miaka ya sasa ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. Walimu wa sasa wamejikita zaidi katika kutafuta idadi ya wanafunzi wanaofaulu kuingia kidato cha kwanza.
Imekuwa kama mashindano ya shule kujua ni ipi itafaulisha wanafunzi zaidi, na msisitizo katika hilo umesababisha wasahau suala la malezi ya wanafunzi kimaadili, wengi wao wameachwa bila kukemewa kwa maovu yanayoonekana kufanywa wazi wazi. Adhabu kama za viboko zimeanza kupotea na inapotokea mwalimu kumwadhibu mwanafunzi kwa viboko kutokana na utovu wa nidhamu, hatari yake ni mwalimu huyo kuitwa katika jopo la nidhamu na kuonywa.
Wanafunzi wengi wanaohitimu masomo katika ngazi za shule za sekondari sasa hivi, huishia katika maskani ya vijana wasio na kazi maalumu, na huko hakuna kinachoendelea zaidi ya kujifunza misamiati ya kiswahili kilichokosa maadili, kile cha kejeli, matusi nk.
Hali kama hiyo haijaanza kwa bahati mbaya, ni malezi mabovu yaliyokiuka misingi ya kuimarisha maadili wakati wakiwa mashuleni. Matokeo yake tunakuwa na taifa la vijana wengi wao wakikosa maadili mema.
Maadili mengine yanategemea taifa lenyewe, namna linavyoweka mtazamo katika mwenendo wa jamii, yapo mambo ambayo taifa linaweza kukemea jamii, kama historia ya maadili ya nchi hayaruhusu wasichana kuvaa nguo fupi, au taifa linapogundua kuwakuta akina dada wakifanya biashara ya kujiuza, hayo yote si utamaduni wetu, ni ukosefu wa maadili.
Ufisadi wa aina yoyote pamoja na rushwa, vitendo hivyo havifanywi na vijana wasiokuwa na ajira, hufanywa na watu wazima, wasomi wenye madaraka wanaoelewa madhara yake, hao pia wanakosa maadili katika nafasi zao za kazi.
Vijana wanapopata taarifa za ufisadi hulazimika kutoa dukuduku zao pia kwa lugha isiyokuwa na maadili, na hapo huonyesha hasira ya namna wasivyoridhika kuona viongozi waliowaweka madarakani wanavyokosa maadili na kukaribisha umaskini.
Vyombo vya ulinzi na usalama pia vina maadili yao, ukiukwaji wa maadili waliyowekewa pia ni jinai, na huwajibishwa kutokana na ukubwa wake, kila sekta, idara pamoja na miundo mbalimbali huongozwa na maadili.
Maadili hujengeka kwa njia mbalimbali, kwa njia ya elimu, mazingira, na ikibidi kwa kulazimishwa, na mara zote jambo la kulazimishwa linafana na adhabu, ili maadili yafuatwe na kuheshimika, ni lazima uwepo mfumo thabiti wa kisheria utakaowawajibisha wote wanaokiuka misingi ya maadili mema, ili hayimaye tuwe na taifa lenye watu waadilifu na watendaji kazi bora.
Maadili mema kwa wasimamizi wa sensa yajidhihirishe kuanzia leo mpaka baada ya siku saba za sensa ya watu na makazi, ili takwimu zitakazopatikana ziisaidie serikali katika mipango ya maendeleo.