Thursday Jun 20, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Suala la utegemezi halina majawabu ya haraka

2nd September 2012
Print
Comments
Maoni ya Katuni

Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu juzi alifanya mapitio ya hali ya uchumi na kinachofanywa na Benki Kuu kukabiliana na changamoto zilizopo, na kwa jumla alichokieleza kilikuwa cha kufurahisha, na isitoshe, kinaonekana katika hali halisi.

Ni kweli kwa mfano kuwa fedha ya nchi imejizatiti zaidi kuliko ilivyokua mwaka jana, na licha ya kuwa yako maeneo ya kuendelea kwa mfumuko wa bei za vitu, kwa jumla kuna utulivu kiasi fulani, nje ya kutopanda kwa vipato na hivyo kila ongezeko la bei linaongeza machungu miongoni mwa kaya nyingi. Hivyo kwa taarifa hiyo hakuna la kuongeza au kutanguliza ubishi.

Ambacho kinaweza kujadiliwa kwa kina zaidi kama changamoto aliyoiinua gavana wa Benki Kuu ni kilio chake kuhusu utegemezi kwa wafadhili katika Bajeti ya Serikali, kuwa mwaka jana serikali ilipokea asimilia 72 ya fedha zilizoahidiwa kama misaada kutoka nje, na juhudi za kujazia kwa fedha za ndani hazifanikiwi kwa kiasi kinachohitajiwa.

Wakati gavana akiongea hayo, juhudi za Benki Kuu katikati ya wiki ya mauzo ya dhamana za serikali ni kama zilikwama, labda maofisa wa Benki Kuu watasema haukuwa msimu wa fedha kupatikana katika soko. Mara nyingine hadi fedha za misaada zije ndipo ‘tuwashe jiko.’

Alipoongelea suala hilo, Gavana Ndulu alionekana kuridhika na viwango vya ukusanyaji kodi ambavyo vimefikiwa, na kuashiria (bila shaka) kuwa tungekusanya zaidi ingekuwa bora zaidi, lakini hakusema hivyo moja kwa moja.

Suala la kuongeza kodi ni moja ya masuala magumu katika mustakabali wa sera za uchumi kwa jumla, na baadhi ya juhudi za kuongeza kodi katika Bajeti iliyopita zimeanza kuonekana, pale wafadhili wa shughuli za kijamii wanapohofia soko kupungua kutokana na ongezeko la kodi kwa walaji, na hivyo kuanza kupunguza michango yao kijamii. Serikali haiwezi kulifidia pengo kwa hizo kodi.

Kwa maana hiyo inabidi ieleweke, licha ya kuwa Gavana Ndulu ameliachia suala hilo ‘hewani,’ yaani kila mtu achukue maamuzi yake kihisia kama kuna haja ya kuongeza kodi, na kama ndiyo, kwa kiasi gani, inabidi tumhitaji akumbushie zaidi nafasi yake ya utaalamu wa uchumi, na hasa wa masuala ya fedha.

Kodi haziongezwi ili kufanikisha tu mipango ya serikali, ila pale inapokuwa hasa ni suala la ustawi wa jamii, yaani usawa wa raia, kwani kwa mahitaji mengine ni suala la kurekebisha Bajeti, na hasa kwa ukubwa wa Bajeti yenyewe. Nchi haijipangii Bajeti yoyote ile na kupania kuifikia kwa kuongeza kodi.

Moja ya matokeo ya ongezeko la kodi ni kupungua kwa kiasi kikubwa kwa pato halisi la mfanyakazi na uwezo wa kununua bidhaa, hali inayosababisha migomo na kuparaganyika kwa nidhamu katika kutoa huduma, pamoja na kufanya rushwa ndogondogo katika taasisi za serikali iwe jambo la kawaida.

Kuzidi kuchochea hali kama hiyo ni makosa, na kinachotakiwa ni kufungulia milango ya kufanya biashara, ili ukusanyaji wa kodi uongezeke bila kuongeza kodi zenyewe, suala ambalo halifanyiwi kazi na wachumi, labda hapo wakiwemo washirika wa Profesa Ndulu kitaasisi. Wanasisitiza tu ‘kupangua wigo’ wa kodi.

Suala la kufungua milango ya biashara ni la msingi katika mikanganyiko ya sera za uchumi zilizopo leo, ambazo msingi wake ni nafasi muhimu inayotolewa kwa mashirika ya umma.

Taasisi hizi zinamega mabilioni ya fedha ambayo yangetumika katika ustawi wa jamii, kwa mfano elimu na huduma za afya, kutokana na mifumo mibovu ya uendeshaji ambako suala la wizi na ubadhirifu ni sehemu ya tatizo na siyo tatizo lenyewe. Halafu yanazuia mabilioni ya fedha kutoka nje kuingia nchini kuinua biashara hizo.

Kwa jumla inabidi Watanzania wakumbuke kile Mwalimu Nyerere alichosema mwaka 1964, licha ya kuwa changamoto hiyo inagusa pia fikra za Mwalimu na mwelekeo wake hasa katika sera za uchumi, kwa ule msemo wa ‘kupanga ni kuchagua.’

Pale tunapopanga kuwa mashirika ya umma yatakuwa ndiyo msingi wa maendeleo, pamoja na kuzuia ardhi kuingia katika milki binafsi kwa kila mwananchi kuwa na hati halisi ya umiliki wa ardhi na kuweza kuuza kama mtu anavyouza nyumba yake, lazima pia turekebishe viwango vyetu vya kutazamia kuondoa umaskini, au ufanisi huduma za jamii.

Kwa maana hii Gavana Ndulu aivumilie serikali, ihudumie mashirika na ingojee wageni walete misaada, isiongeze kodi.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment