Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Maadili yazingatiwe kwenye sanaa

17th April 2012
Print
Comments

Nadhani tukio la hivi karibuni la watoto kushindanishwa kucheza utupu, yaani dressing down, kwa stahili aliyoianzisha Madona miaka kadhaa iliyopita na sasa inaonekana kurithiwa na Msanii mwingine wa Marekani, Rihana, linahitaji kutafakariwa kwa makini na jamii linapofika Tanzania na watoto wadogo kuingizwa.

Kuna mambo ya msingi sana ambayo tunatakiwa kuyatafakari kama tunataka kuwa na mustakabali mwema wa taifa letu.

wanza kabisa ni suala la mfumo wa uchumi unavyowafanya vijana kuamini kuwa unaweza kutajirika na kuwa mmojawapo wa wenye fedha kwa njia ya mkato.

Matangazo ya biashara, matangazo ya makampuni ya simu (hasa) yanaongoza kwa kujenga dhana hii ya kuwa ukikwanyua vocha, ukatuma pesa kwa mtandao wao, unapata mamilioni.

Na kwa milioni moja Tanzania unaweza kuwa milionea? Lakini ni itikadi ya kibepari inayowafanya vijana kushindwa kutafuta ajira za maana na kukimbikia njia za mkato. Na sanaa inaonekana kuwa ni njia ya mkato.

Nadhani kuna kirusi kilianza na kuenea katika jamii yetu kuamini kuwa ukiingia kwenye sanaa si lazima uwe umesomea na kujenga ujuzi. Eti ni kipaji. Kuna wachache wamefanikiwa kifedha, na wanadhani kufanikiwa kifedha umefanikiwa kiusanii. Ni kwa sababu tu kuna pengo la kukosekana wasanii waliosomea halijazibwa. Lakini wengi ni wasanii wa miaka mingi lakini kiujuzi hawajafanikiwa kabisa.

Wao hawaoni mbele , na wanakaa na wenzao ambao pia uelewa wao ni finyu, na hawaendelei, kuangalia kazi zao za sanaa kwa jicho la uhakika unaona kabisa amefanikiwa katika safari ya kupata fedha, lakini safari ya kisanii hajafanikiwa kabisa. Na inapokuwa kwa wasichana ni mbaya zaidi!

Kwa sasa hivi wasichana wengi wanaingizwa kwenye sanaa kama kwa kupendelewa, kujuana, na kuahidiwa kuwa atakuwa msanii mkubwa mwenye jina, fedha na maisha bora.

Lakini sidhani kama kuna wasanii wa kike wa kutosha hapa Bongo ambao unasema wameingia kwa ujuzi kamilifu na sasa wanafedha zao. ni wachache, na hadithi nyingi ni za kuleta aibu kama zikianikwa.

Tunapowaingiza wasichana wadogo (na hata wavulana) ambao hawana utashi mkubwa wa kutafakari, na hawajasomea sanaa achilia mbali kuwa hawajamaliza elimu ya msingi, au wameishia hapo tu, na sekondari, ni wazi kuwa tunataka kuwarubuni wakaharibu maisha yao.

Sidhani wanalipwa fedha ya kutosha kuweza kujikimu, lakini mara moja huyu mtoto anakuwa nje ya mfumo wa kijamii- an outcast, analazimika kuishi kama “msanii” wakati hana ujuzi wa kazi yenyewe.

Aidha kuna matajiri na wasanii ambao wameanzisha vikundi na kumbinza starehe ambazo zinawatumikisha wasichana kwa sababu wana dhiki. Nafahamu Ubugo , kuna ukumbi wa kunywa bia ambako wanawake wanalazimika kukata mauno wakiwa wamevaa chupi tu na kanga moja, jamii inaona, serikali inaona.

Lakini kwa malipo yapi? Wengi wanalipwa ujira mdogo sana kama hao wa watoto walioambiwa wacheze kwa kukaa uchi.

Ni kichele ambacho hakiwezi kuwatosheleza kwa wiki hata moja. Lakini pia wanajikuta wakifanya mambo ambayo hawastahili: Nina ushahidi wa wasichana hao kutumia mirungi, bangi, madawa ya kulevya na pombe ili kuondoa aibu wakati wa kufanya maonyesho. Sio kwa kupenda ila kwa sababu, wengi wao, wasipofanya hivyo siku haitapita, chakula hawatakula.

Nadhani kuna mabadiliko yanayotakiwa kufanyika sasa. Kama serikali kweli, na vyama vya sanaa na vyama vya wafanyakazi, vikaamua kufanyakazi yake, kuna mengi yanaweza kurekebika.

Kwa mfano tukiwauliza hawa watoto waliochezeshwa uchi, je, walishirikishwa wazazi? Je, kuna mikataba ya malipo ya fidia kwa kushiriki na malipo ya  mshindi, na kuwa kiasi gani cha awali, na kiasi gani cha mwisho. Na  namna gani atafuatilia malipo kama kutakuwa na mgogoro.

Aidha mkataba lazima ueleze namna gani mshiriki anaweza kukatiza ajira yake kama haridhiki na baadhi ya mambo. Inapokuwa tangazo linaita tu mtu aje kwa kudra yake na malipo yanakuwa kwa maneno na sio maandishi. Na pili umri wa chini kabisa kushiriki uainishwe.

Aidha ni vizuri vyama vya sanaa na vyama vya wafanyakazi vikasimamia uandikaji na utekelezaji mikataba hiyo na kuwa wasanii wajue wapi pa kulalamika endapo wamedhulumiwa.

Hili ni jambo rahisi sana, kuwa elimu ya umma inaimarishwa, wasanii wanajua haki zao, na viwango vya chini vya malipo kwa aina mbalimbali vya usanii au kazi za sanaa, hasa washiriki, vinawekwa kwa kuzingatia uwezo wa msanii kadri ya alivyosomea.

Isije kuwa watu wanalipwa fedha ya soda tu.  

Kama tutaanza kujenga msingi wa kuheshimu maana ya kazi, na kuishi kwa kuheshimu mikataba, maadili yanaweza kurudi kwenye sanaa.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles