Sunday May 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Tanzania kufungua na Lesotho netiboli Afrika leo

8th May 2012
Print
Comments
Mke wa Waziri Mkuu, Tunu Pinda akipokea msaada wa vifaa kutoka kwa meneja wa Mahusiano ya Nje wa Vodacom Tanzania, Salum Mwalim vyenye thamani ya sh. milioni 6 kwa ajili ya ushiriki wa timu ya netiboli ya Taifa Queens katika mashindano ya Afrika yanayoanza jijini Dar es Salaam leo.

Timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, itafungua la pazia la mashindano ya kuwania ubingwa wa mchezo huo Afrika kwa kuikaribisha Lesotho katika mechi itakayofanyika kwenye kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Mashindano hayo yanayoshirikisha nchi nane za Afrika yanatarajia kufunguliwa na mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Salma Kikwete.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kaimu katibu wa chama cha netiboli nchini (CHANETA), Rose Mkisi alisema mchezo mwingine wa leo utakuwa ni baina ya Malawi na Botswana.

Nchi nyingine zilizowasili kwa ajili ya michuano hiyo ni Zambia, Zimbabwe, Namibia na Uganda.

Mkisi alisema kuwa Taifa Queens wamejiandaa vizuri kwa nia ya kulibakisha kombe hilo nchini na akawataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kushuhudia mashindano hayo.

Wakati huo huo, mke wa Waziri Mkuu, mma Tunu Pinda jana alipokea michango kutoka kwa kampuni za Vodacom na Zantel ikiwa ni mwitikio wa ombi lake kwa Watanzania kuwahamaisha waichangie timu ya Taifa Queens.

Mama Pinda alipokea vifaa vya michezo kwa ajili ya mashindano kutoka kampuni ya Vodacom Tanzania vyenye thamani ya Sh. milioni sita na pia simu za mkononi 300 zenye simcard na muda wa maongezi kwa ajili ya wachezaji na viongozi wao kutoka kampuni ya Zantel zenye thamani ya Sh. milioni 10.

Akikabidhi vifaa hivyo vya michezo hiyo, Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom, Salum Mwalimu alisema wameitikia wito wa Mama Pinda wa kuichangia timu ya Taifa Queens kwa sababu wametambua umuhimu wa kuiunga mkono timu hiyo.

"Vifaa tulivyotoa ni jezi 20, suti za michezo 20, raba pea 20 na bibs 20… tuna imani timu yetu ya taifa itapenya hadi hatua ya fainali,” alisema.

Naye Meneja Biashara wa Zantel, Ahmed Mokhles akikabidhi simu hizo, alisema wametoa mchango huo kwa sababu wanaamini kwamba japokuwa watakuwa hapa nchini, wachezaji na maafisa wao wana haki ya kuwasiliana na familia zao.

Zantel pia walitoa 'router' mbili kwa ajili ya ofisi za Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) ili ziweze kuwasadia katika mawasiliano yao ya Internet.

Akitoa ufafanunuzi kuhusu michango ambayo imekwishatolewa hadi sasa, Mama Pinda alisema jumla ya Sh. milioni 178.2 zimekwishapokelewa hadi sasa zikiwa ni fedha taslimu na vifaa. Kati ya hizo, Sh. milioni 114.8 ni fedha taslimu na Sh. milioni 53.4 ni vifaa vilivyotolewa na wadau mbalimbali kuchangia mashindani hayo.


SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment