Wednesday May 4, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Utoaji mikopo Elimu ya Juu wabadilishwa

20th August 2011
Print
Comments
  Ni mapendekezo mapya ya Tume ya Rais
  Vyuo kupelekewa fedha, si wanafunzi
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawamba

Kuanzia mwaka huu wa masomo wanafunzi wa taasisi za na vyuo vya elimu ya juu nchini watapelekewa fedha zao za mikopo katika vyuo vyao badala ya kuwekewa katika akaunti zao binafsi.

Aidha, waombaji kwenye vyuo binafsi, mikopo itatolewa kulingana na ada zinazotozwa na vyuo vya umma kwa fani husika na kwamba katika fani ya udaktari ukomo wa juu wa mikopo utaendelea kupangwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawamba, alitoa kauli hizo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Dk. Kawambwa alikuwa akizungumzia kuhusiana na mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Rais ya kuangalia na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha utaratibu wa sasa wa ugharimiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya Elimu ya Juu.

Hata hivyo, alisema utaratibu huu mpya wa utoaji wa mikopo utawahusu wanafunzi wa mwaka wa kwanza tu na kwamba wanafunzi wanaondelea na masomo wataendelea kwa utaratibu uliopo sasa.

Kuanzia mwaka wa masomo 2011/12, fedha zote za mikopo zitapelekwa vyuoni ili vyuo viwalipe wanafunzi baada ya kuwahakiki.

Maelekezo na utaratibu utakaotumika utaandaliwa na Bodi ya Mikopo kwa kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu na wadau wengine husika,” alisema Dk. Kawambwa.

Alisema ili kuboresha ufanisi wa utoaji wa mikopo, kila chuo kitatakiwa kuwa na dawati la Masuala ya Mikopo ambalo litakaloendeshwa na watumishi wenye sifa stahiki na mahusiano mazuri na jamii litakuwa chini ya Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma.

 

Dk. Kawambwa alisema mikopo itatolewa tu kwa waombaji waliodahiliwa na vyuo vya elimu ya juu na ambao wanatoka shuleni moja kwa moja na wale wenye sifa kupitia mfumo wa mafunzo ya elimu ya ufundi.

Aidha, alisema utoaji wa mikopo utazingatia uhitaji wa mwombaji, fani za kipaumbele za taifa na madaraja ya ufaulu.

Utaratibu wa kubaini wahitaji wa mikopo utazingatia vigezo vinavyopimika kwa urahisi kama vile shule aliyosoma, uyatima, ulemavu na uwezo wa kiuchumi wa mzazi ama mlezi,” alisema na kuongeza kuwa:

Kiwango cha mkopo kwa wale wanaostahili kukopeshwa kitategemea matokeo ya tathmini ya uwezo wa kiuchumi wa mwombaji na mzazi ama mlezi, kwenye vipengele vya ada na mahitaji maalumu ya vitivo.”

Aidha, alisema mikopo itatolewa kwa asilimia100 katika maeneo ya chakula, malazi, mafunzo kwa vitendo kwa fani ambazo zitabainishwa na Tume ya Vyuo Vikuu, vitabu na utafiti.

Alisema kwa kuzingatia kuwa wahitaji ni wengi, umuhimu utapewa kwa wahitaji wanaochukua fani za kipaumbele za kitaifa ambazo kwa sasa ni ualimu, sayansi za tiba (Udaktari wa Binadamu, Udaktari wa Mifugo, Udaktari wa Meno, Ufamasia na Uuguzi), Uhandisi, Sayansi za Kilimo na Sayansi za Mifugo.

Pia alisema waombaji katika fani ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati na Sayansi za Tiba, watapatiwa mikopo kwa asilimia 100 na kwamba waombaji wa ualimu ambao si wa fani ya Sayansi na Hisabati watapewa mikopo kwa asilimia isiyopungua asilimia 50.

 

Waombaji wenye sifa linganishi (equivalent qualifications na mature entry) katika fani za Ualimu wa Sayansi na Hisabati na Sayansi za Tiba watapata mikopo kwa asilimia 100. Waombaji wengine wote waliobaki wenye sifa linganishi na ambao ni wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wataweza kuomba mikopo katika Mifuko hiyo, kwa Waajiri wao au kutoka Taasisi nyingine,” alisema.

Alisema mikopo itatolewa kwa wanafunzi waliodahiliwa katika Vyuo vya elimu ya Juu vyenye usajili kamili tu.

Kuhusu suala la urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi, Dk. Kawambwa alisema jitihada za makusudi zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kurekebisha baadhi ya Sheria za taasisi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa wakopaji wanarudisha mikopo.

Dk. Kawambwa alisema kiwango cha chini cha marejesho ya mkopo kitakuwa ni asilimia nane ya mshahara au kipato halisi kwa mwezi kwa mnufaika wa mkopo.

Alifafanua kuwa awali mkopaji alikuwa akilazimika kumaliza deni la mkopo huo kwa miaka 10, hali ambayo iliwafanya baadhi ya wakopaji wanaopata mishahara midogo kuumia sana kutokana na makato.

Tume hiyo iliundwa na Rais Jakaya Kikwete, Februari 14 mwaka huu kuchunguza utaratibu wa utoaji wa mikopo kutokana na malalamiko, iliwasilisha taarifa na mapendekezo yake serikalini Aprili 29, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, Tume hiyo ilizingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbali mbali ndani na nje ya nchi na kwamba serikali imeipitia taarifa ya Tume hiyo na kuyafanyia uchambuzi mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha utoaji na urejeshaji wa mikopo ya Elimu ya Juu.

TCU YADAHILI 31,093

Asilimia 77.5 ya wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vikuu nchini kwa mwaka huu wa masomo 2011/12 wamekubaliwa, huku 22.5 wakikosa nafasi ya kuchaguliwa kati ya wanafunzi 40,150.

Hayo yalisemwa jana na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Profesa Sifuniel Mchome, alipozungumza na waandishi wa habari.

Profesa Mchome alisema tangu walipoanza mzunguko wa udahili kuanzia Aprili 12 hadi Mei 31, mwaka huu walipokea maombi ya wanafunzi 40,150 na kwamba waliochaguliwa ni 31,093 na ambao hawakuchaguliwa ni 9,057 kwa kutumia mfumo wa kati wa udahili (CAS).

Alisema kuwa kati ya wanafunzi 9,057 ambao hawakuchaguliwa, 4,013 wana vigezo vya kujiunga na vyuo hivyo, lakini hawana vigezo vya kujiunga na kozi walizozichagua na kwamba waliobaki 5,044 hawana vigezo kabisa vya kujiunga na vyuo.

Hawa wanafunzi 4,013 ambao wana vigezo vya kujiunga na vyuo, lakini hawana vigezo vya kusoma kozi walizochagua wana nafasi ya kuomba tena kwa mara nyingine, lakini si kwa kozi walizoomba hapo mwanzo na mwisho ni wiki ijayo,” alisema.

Aliongeza kuwa vigezo vya kujiunga kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita ni wastani wa kufaulu masomo matatu kidato cha nne na wastani usiopungua pointi 4.5 kwa kidato cha sita na kwa wale wanaotaka kujiunga wakitokea vyuo vilivyopo chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Elimu na ufundi (NACTE) lazima wawe na vyeti daraja la kwanza au stashahada ya daraja la pili.

Alisema kuwa mfumo wa CAS hutumika katika kuchagua wanafunzi wenye vigezo bila upendeleo kwa kupitia hatua mbalimbali zikiwemo kujua taarifa za mwombaji kwa undani na kuchagua majina hayo kabla hayajapelekwa kwenye taasisi za elimu ya juu kwa ajili ya uhakiki.

WAPYA 55,777 WAOMBA MIKOPO HESLB

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema jumla ya maombi 55,777 mapya yalikuwa yamepokelewa hadi Juni 30, mwaka huu ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kupokea maombi ya mikopo kwa njia mpya ya mtandao.

Aidha, jumla ya maombi 47,657 toka kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo katika vyuo vya elimu ya juu yalikuwa yamepokelewa na bodi kufikia siku hiyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, aliiambia NIPASHE jana kuwa katika mfumo mpya wa maombi kwa njia ya mtandao ulioanzishwa Aprili mosi, mwaka huu, Bodi ilitarajia kupokea maombi mapya 60,000.

Vile vile, Mwaisobwa alisema kwamba kwa upande wa wanafunzi wanaoendelea na masomo, bodi ilitarajia kupokea maombi 51,000.

Akizungumzia idadi ya wanafunzi watakaopata mkopo mwaka huu, Mwaisobwa alisema idadi hiyo itajulikana baada ya kutolewa idadi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali nchini toka TCU.

Imeandikwa na Sharon Sauwa, Dodoma; Raphael Kibiriti, Erick Mashafi na Ashraf Khamis, Dar

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles