Sunday May 1, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Jinsi ya kukabiliana na visumbufu vya mazao

10th February 2012
Print
Comments

Mwandishi maarufu wa vitabu vya Kilimo, Pius B. Ngeze, ameandika kitabu kingine kiitwacho Visumbufu vya Mazao ya Kilimo. Nimependelea kukihakiki kitabu hicho cha kurasa 41, kwa sababu maudhui yake yatadumu zaidi ya miaka 41.

Hii inatokana na ukweli kuwa, katika kilimo chetu, wakulima wakivijua visumbufu hivyo na kuvichukilia hatua uwezo, maarifa, na   kiwango cha kujiamini utaongezeka.

Kitabu hicho kimegawanyika katika sura kuu sita ambazo ni: Visumbufu  Vikuu vya Mazao (Sura ya I), Magugu na Jinsi ya  Kuyadhibiti (Sura ya 2), Magonjwa  na Njia za Kuyadhibiti (Sura ya 5) na  Uangallifu katika kutumia Dawa za Mimea (Sura ya 6). Baada ya kukamilisha sura hizo sita Ngeze ameongezea kitu ambacho amekiita Tafsiri. Hiyo ni tafasiri ya maneno ya Kiingereza ambayo ameyatumia katika kitabu na kuyatafasiri kwa Kiswahili.

 Kitabu hicho kimechapishwa na Tanzania  Educational Publishers Ltd (TAPS). Sasa tuangalie maudhui yake.

Neno usumbufu, linatokana na neno sumbua, ambalo maana yake ni: kitendo  kinachosababisha kukosa utulivu au raha, kitu kinachotia tabu au kinachoudhi, kinachokera, au kuhangaisha.

Kwa mujibu wa kitabu cha Ngeze, visumbufu ni magugu, wadudu, magonjwa ya mimea, upatikanaji wa madawa ya kuuwa wadudu na kadhalika.

Ngeze amechukua jukumu la kuainisha visummbufu hivyo, kwa lengo la kuwaelimisha wakulima ili waelewe vikwazo vinavyowakabili kwa lengo la kupata mafanikio maridhawa katika  kilimo .

Katika utangulizi wake Ngeze ameeleza kuwa uwingi wa mazao na ubora wake  unaweza kupungua endapo mazao hayo yamepata kuathiriwa  na visumbufu  vya aina fulani.

Mwandishi huyo ametaarifu kuwa hapa nchini Tanzania, kuna aina 100 za mazao ambayo yanaweza kuathiriwa na visumbufu vya aina mbalimbali. Pengine amesahau kwamba miongoni mwa visumbufu vilivyopo, binadamu yumo.

 Hata hivyo, Ngeze amesisitiza kwamba maelezo yaliyotolewa katika kitabu hiki, licha ya udogo wake, yanatoa  mafunzo ya msingi na namna ya  kukabiliana na  visumbufu hivyo.

Ameainisha madhara yanayoweza kupatikana kwa kutumia hovyo madawa ya kuulia wadudu.

Visumbufu ambavyo mwandishi amevibaini viko sita. Amevigawa  katika makundi makuu saba ambayo ni:  magugu, minyoofundo (nematoda), magonjwa, ndege,  wadudu, wanyama wakubwa na jamii ya mchwa.

Hata hivyo mwandishi amesahau visumbufu vingine ambavyo ni hatari zaidi. Kwa mfano, wezi wanaongojea kuiba mazao ya watu wengine.

Wanavunja juhudi na ari ya wakulima. Kisumbufu kingine ni urasimu na ucheleweshaji wa pembejeo. Kukabiliana na visumbufu hivyo, Ngeze ametoa njia kuu mbili.

Kuzuia visitokee, kama vile wadudu, na magonjwa ya mimea, kwa kuchukua hadhari zifuatazo: (a) kuweka dawa katika udongo na hivyo kuwaua wadudu wanaopendelea kuishi ardhini. (b) Kutumia dawa kwenye mbegu na hivyo kuua viini na kwa kuwafuata huko huko wanakozaliana na kuwawahi kabla hawajafika eneo la shamba.

 Hatua hiyo inaweza kufanywa kwa wanyama, ndege na wadudu. Sijui  kwa binadamu kutafanyika nini! Uzoefu wa kukabiliana na binadamu wa aina hiyo  unahitilafiana sehemu na sehemu.

Ipo haja ya kubadilishiana uzoefu katika swala hili ili kujua tunavyoweza kukabiliana nao.

 Njia kuu zilizopendekezwa na mwandishi wa Visumbufu vya Mazao ni pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya visumbufu vifuatavyo .

MAGUGU

Magugu ni aina yoyote ya mimea inayoota mahali popote isipotakiwa. Kwa mfano, mpunga ukiota ndani ya shamba la mahindi, basi ule mpunga ni gugu.

Magugu nayo yamegawanyika katika makundi  makuu  matatu ambayo ni: Magugu mwaka, magugu jozi na magugu dumu. Magugu mwaka na aina yoyote ya magugu ambayo huishi kwa  mwaka mmoja tu. Magugu jozi ni yale ambayo huishi si zaidi ya miaka miwili . Magugu dumu nayo, huishi zaidi ya miaka miwili.

Hayo ni wakubwa shambani. Je, unajua magugu hayo yanaingiaje shambani mwako?

Yanaingia shambani kwa njia ya upepo, maji, kwa  kutambaa, kuchanganyika na mbegu, na mabaki ya  mazao   ya kulishia  mifugo au kutumiwa kama mbolea.

 Baada ya kujua magugu yanavyovamia mashamba yetu sasa tuone na tuzielewe hasara za kuvamiwa na magugu.

Kimsingi, magugu hupora maji, chakula na kubana nafasi inayotakiwa kupanda mimea katika kilimo. Magugu mengine hunyonga mimea iliyopandwa kwa kujizungusha kwenye mimea  na ikashindwa kutoa mazao yanayotakiwa.

Kitu kingine ambacho magugu hayo yanaweza kufanya ni kuhifadhi wadudu wabaya ambao ni hatari kwa mimea iliyoko shambani.

 Magugu hayo yanapojinyonga au kujizungusha katika mimea iliyopandwa, inazuia mionzi ya jua kuifikia mimea iliyopandwa na hivyo kuudhoofisha  mimea  ile iliyopandwa. Aidha kuna aina nyingine ya magugu ambayo  inawasha.

 Magugu hayo hufanya kazi za kupalillia na kuvuna iwe ngumu sana kwa vile usipoangalia, utawashwa mwili mzima. Tusisahau pia kuna magugu ambayo yana miiba na huleta usumbufu wakati wa kupanda, kupalilia na kuvuna.

Orodha ya madhara ya magugu ni ndefu.Tusisahau kuwa magugu mengine hutoa harufu mbaya, yananuka.Harufu hiyo inaweza kuambukiza kwenye nguo za mkulima, katika maziwa ya mifugo hata nyama yenyewe.

Ikitokea hivyo, mkulima anaweza kula hasara kwa sababu wateja hawatapendelea kununua vitu vya kunuka..

Hasara moja kubwa ambayo magugu huleta shambani, ni kule kuifanya ardhi iwe ngumu mno wakati wa kulima. Huko nyuma imeelezwa kwamba magugu yana tabia ya kupora majimaji au unyevu uliomo shambani.

Kwa kufanya hivyo, magugu hufanya ardhi iwe ngumu na matokeo yake ni kukausha ardhi na kuifanya iwe ngumu

Mbinu za kutumia

Tukitaka kukabiliana na magugu kama adui wa mkulima ni muhimu kutayarisha vizuri mahali pa kupanda mbegu,. Kutenganisha mbegu za magugu na zile utakazopanda, kutandaza nyasi shambani ili kuyazuia magugu yasiote kwa urahisi.

 Kuacha ardhi ipigwe jua kwa muda wa wiki mbili hivi baada ya kulima , na kabla ya kupanda, kubadilisha mazao shambani,  kupalilia mara kwa mara na kung’oleang’olea pale ambapo jembe halipiti kwa urahlisi.

Njia nyingine ambayo inaweza kuangamiza magugu ni kwa kutumia viangamizi au viuamagugu. Hiyo ni dawa ambayo huangamiza magugu ya aina yote. Dawa inayotumika ni ile iitwayo Kloreti ya natiri. Magugu yatakufa na mimea yako itabaki salama kabisa.

Kuna njia nne zinazojulikana za kutumia viuamagugu ambazo ni:-Njia ya kwanza ni kunyunyizia dawa shambani kabla ya kupanda mbegu. Njia hii huzuia kabisa kutoa magugu na ni sehemu ya maandalizi ya shamba.

Unachotakiwa kufanya ni kungojea tu siku mbili tatu hivi baada ya kupiga dawa.  Upande wakati mimea ikichipua, utakula hasara.

 Njia ya tatu ni kunyunyizia dawa baada ya mbegu kuota au baada ya mimea kufikia umri fulani. Hata hivyo uangalifu mkubwa unatakiwa, kujua dawa ipi itumike na wakati gani.

Maafisa Kilimo wanahitajika kushauriwa jambo ambalo Mwandishi wa  Kitabu hakusisitiza. Njia ya tatu  ni ya kutumia dawa kwa kulimia udongoni.

Magonjwa

Viumbe vyote vyenye uhai vinasumbuliwa na magonjwa au maradhi ya aina mbalimbali. Magonjwa hayo yanaleta usumbufu mkubwa na hurudisha nyuma kilimo pamoja na maendeleo kwa jumla .Kwa upande wa mimea inaweza kushambuliwa sehemu yoyote kwenye maua, mbegu, majani, matawi, magome, shina, hata mizizi yake.

Baadhi ya mambo ambayo Ngeze ameyataja kuwa yanakaribisha magonjwa ya mimea ambayo yako katika sura ya tatu ni: tabia ya kupanda mazao yaleyale katika shamba lilelile kwa misimu mingi mfululizo. Kubadilisha kupanda mazao kunasaidia.

Tukwepe kupanda mazao ambayo yanashambuliwa haraka na magonjwa.

Ngeze hakuyataja mazao gani yanayoshambuliwa kwa urahisi. Bila shaka anategemea busara za wakulima wenyewe zitatumika pamoja na utaalamu wa maafisa kilimo.

Ila  jambo moja ambalo husababisha kukaribisha maradhi ya mimea ni matumizi ya kuzidi ya mbolea ya nitrojeni.   Mbolea hiyo hufanya mimea inenepe na kuwa kijani na hivyo kuvutia magonjwa yanayoletwa na kuvu.

Hali ya hewa pia huchangia katika kueneza maradhi. Ukosefu wa mvua na hali ya joto vinaweza kukaribisha  maradhi kwa urahisi.

Moja ya njia ya kudhibiti magonjwa ya mimea kama ilivyo kwa magonjwa mengine ni kujua namna maradhi hayo yanavyosambazwa na wadudu, wanyama na ndege.

 Kuvu ni aina ya mimea midogo sana ambayo haionekani kwa macho matupu.Ni mimea tegemezi. Hupata chakula chao kwa kujibanza kwenye mimea iliyopandwa na wakati huohuo kuidhuru.

Maafisa Kilimo wanaweza kuoyesha  namna madhara hayo yanavyotokea.

Kuna wadudu wengine wadogo sana ambao hawaonekani kwa macho yetu ya kawaida, mpaka kwa darubini. Wadudu hao ni bakteria. Bakteria hushambulia` mboga na matunda. Kwa mfano kuna ugonjwa  unaoitwa  Bakamoto.

Aina zote hizo za wadudu na hatua za kuwachukulia zimo katika sura ya nne ya kitabu hicho cha Ngeze.

Kuzuia kuenea kwa magonjwa ya mimea ni jambo muhimu. Wakulima sharti  waelewe  kuepukana na  visumbufu hivyo. Wakulima waelimishwe kubadilisha upandaji wa mazao shambani, kuyachoma na kuyateketeza masalia  ya mazao yote yaliyobainika yana maambukizi.

Wakubali pia maagizo ya wataalamu  kutopanda mazao yaliyopigwa maarufuku. Wapande  mimea kinzani ambayo haishambuliwi kwa urahisi na maradhi. Mimea hiyo ikipandwa na mimea mingine  huwa kinga.

Unyunyuziaji wa dawa  ni njia nyingine. Kemikali hizo zipo za maji, vumbi na mvuke ambazo zinaweza pia  kutibu udongo usilete maambukizi.

Matumizi ya  dawa mbalimbali yanahitaji umakini. Watalaamu wanatakiwa kuwaelimisha wakulima namna ya kutumia pembejeo hizo.

Aidha bei za dawa na pembejeo hizo zisiwe  kikwazo kwa mkulima kutokana kuwa ghali.

Hitimisho

Katika kukipitia  kitabu hiki cha Ngeze,  utaona amerudiarudia mambo. Ametumia utaratibu huo kusisitiza suala la kuangamiza wadudu na magugu.

Mbinu za kukabiliana nazo zinafana na  ameandika hivyo ili  kuweka bayana kila Kisumbufu na namna ya kukabiliana nacho. Kama nilivyoeleza hapo nyuma, msumbufu mkubwa ni binadamu mwenyewe.

Watu wamekuwa wasumbufu zaidi kuliko wadudu, ndege na wanyama. Binadamu  hutumia ujanja kuwaibia wenzao,  wakitafuta utajiri wa haraka haraka. Huo  si umbufu?

Ngeze ametoa maelezo  mafupi ya kumsaidia mkulima endapo ameingiwa na sumu. Sumu humwingia mtu kwa hewa, kunywa, kula au kugusa. Mtu aliyepatwa na sumu hukosa nguvu, hutetemeka, huashwawashwa mwilini na tumbo huchafuka.

Mtu huyo apelekwe haraka hospitali. Inashauriwa yaaandikwe maelezo yake kabla hajapoteza fahamu.

 Kuepusha matatizo hayo, dawa zote na mbolea ziwekwe mbali na watoto. Aidha, vyombo vyote ambavyo  vilitumka vikoshwe mara  baada ya kuvitumia. Wakulima wasile matunda au mazao mara tu baada ya kunyunyizia dawa.

 Ngeze hakusema ni  baada ya muda gani mtu anaweza  kula matunda baada ya kutia dawa. Ushauri huo anategemea utapatikana kwa wataalamu wa kilimo walio karibu. Hata hivvo, Ngeze anastahili pongezi kwa. kazi aliyoifanya ya kuwaelimisha wakulima kuhusu  VISUMBUFU  VYA  MAZAO SHAMBANI ni mchango maridhawa hasa wakati huu ambao KILIMO KWANZA ni kauli mbiu ya kazi yetu ya Kilimo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles