Friday May 6, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Kesi ya Lema: Shahidi ni mwongo

24th February 2012
Print
Comments
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema

Wakili Method Kimomogoro anayemtetea Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge wake, amemweleza shahidi  anayetoa ushahidi dhidi ya mbunge huyo kuwa ushahidi wake ni wa uwongo.

Aliieleza Mahakama wakati akimhoji shahidi huyo wa sita, Said Athuman, ambaye anatoa ushahidi wa upande wa wadai, Musa Mkanga, Happy Kivuyo na Agness Mollel ambao walifungua kesi hiyo.

Kimomogoro aliitoa madai hayo baada ya shahidi kuieleza mahakama kuwa hakumbuki siku, tarehe wala mwezi ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha,  kiilifanya mkutano wa kampeni za kumnadi aliyekuwa mgombea wake wa Jimbo la Arusha Mjini, Dk. Batilda Burian.

Awali  akiongozwa na katika mahojiano na  wakili wake, Modest Akida, shahidi Athuman alidai kuwa alihudhuria mikutano mitatu ya kampeni za uchaguzi mwaka 2010 ambayo ni ya Tanzania Labour, (TLP), CCM na Chadema.

Alidai kuwa mikutano hiyo ilifanyika eneo la wazi huko kwa Mrombo, katika Kata ya Terrat kwa siku tofauti.

Aidha aliiambia mahakama kuwa hakumbuki mkutano wa Chadema ulifanyika lini, lakini ilikuwa mwishoni Agosti, 2010.

Mahojiano kati ya Kimomogoro na Athuman yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Siku ulipohudhuria mkutano wa CCM kwa Mrombo Musa Mkanga alikuwepo (huyu ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo)?

Shahidi: Sikumuona.

Wakili: Na siku ulipohudhuria mkutano wa Chadema, Musa Mkanga alikuwepo?

Shahidi: Ndio nilimwona kwa mbali?

Wakili: Hamkusalimiana, siyo?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Ulimpungia mkono?

Shahidi: Wala, alikuwa mbali kidogo.

Wakili: Wewe ni mwanachama wa  Chadema?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kwa nini unakumbuka mkutano wa Chadema, lakini hukumbuki mikutano ya TLP au CCM kama ilikuwa ni mwanzoni au mwishoni. Chadema kinakuvutia sana, wewe sio mwanachama?

Shahidi: Chadema ni chama chenye nguvu hapa Arusha.

Wakili: Sasa haya maneno unayosema yalitamkwa na Lema kuhusu Dk. Batilda yalikufurahisha?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Yalikuudhi?

Shahidi: Ndio.

Wakili: Hayo maneno yalikuudhi kwa vipi?

Shahidi: Kilichoniudhi ni kwamba sisi Watanzania tumelelewa katika maadili ya kutokubaguana kijinsia, kidini wala kikabila.

Wakili: Baada ya kuudhika na maneno hayo kuna taarifa uliyotoa popote?

Shahidi: Ndio, niliwasiliana na mwalimu wa madrasa, Said Rashid.

Wakili: Hayo madrasa yapo wapi?

Shahidi: Pale kwa Mrombo na nyingine ipo kwenye kota za polisi Central.

Wakili:  Ilikuwa baada ya muda gani wa mkutano?

Shahidi: Baada ya wiki moja.

Wakili: Nimesikia ukisema kwa Mrombo ipo kata gani?

Shahidi: Kata ya Terrat.

Wakili: Ulikwenda kutoa taarifa kwa ofisa mtendaji wa mtaa au kata?

Shahidi: Sikwenda.

Wakili: Kuna ushahidi ulioletwa hapa kwamba kwenye mikutano hiyo kulikuwa na ulinzi, uliona hiyo?

Shahidi: Niliona.

Wakili: Wewe ni mwanachama wa chama gani?

Shahidi: Kwa kweli sijajiunga na chama chochote.

Wakili: Hata Chadema?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kutoka nyumbani kwako hadi ofisi ya mtendaji wa kata kuna umbali gani?

Shahidi: Kama kilomita moja hivi.

Wakili: Ni kweli kwamba mambo yaliyojiri kwenye mikutano ya kampeni ya Lema yalikuwa yakijadiliwa mitaani, sio?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Unafahamu kwamba maofisa watendaji wa kata walikuwa na jukumu la kufuatilia kampeni hizo katika maeneo yao?

Shahidi: Hilo sifahamu.

Wakili: Unafahamu maofisa wengine wa serikali waliokuwa wakifuatilia masuala ya kampeni?

Shahidi: Siwafahamu.

Wakili: Ni lini uliitwa kwa mara ya kwanza kuja kutoa ushahidi wa shauri hili mahakamani?

Shahidi: Kwa mara ya kwanza ni leo.

Wakili: Ni lini ulifuatwa kuja kutoa ushahidi wa kesi hii?

Shahidi: Ni  mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2011 nilipohitajika kuja kutoa maelezo.

Wakili: Aliyekutafuta kuja kutoa maelezo kwa wakili ni nani?

Shahidi: Ni Musa Mkanga.

Wakili: Alikuambia nini Musa Mkanga uende kwa wakili kufanya nini?

Shahidi: Yale niliyoyasikia kwenye kampeni za uchaguzi wa Chadema kwa Mrombo.

Wakili: Naomba nikuite mwongo! Unafahamu kwamba CCM haikuwahi kufanya mkutano kwa Mrombo mwezi wote wa Agosti na ndio maana hukumbuki ilikuwa ni tarehe gani?

Shahidi: Nasema hivi, kwenye tarehe na sehemu nyingine miezi sikumbuki.

Wakili: Na pia TLP haikuwahi kufanya mkutano wa kampeni kwa Mrombo mwezi wowote wa Agosti, huu ni uongo mwingine pia umetunga.

Shahidi: Sijatunga.

Wakili: Ndio nakuambia pia CCM na TLP hawajawahi kufanya mikutano mwezi wote wa Agosti?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Mwanzoni mwa Septemba, 2010 vyombo vya habari hapa nchini viliandika taarifa za malalamiko ya Dk. Batilda kuhusu kampeni, unakumbuka?

Shahidi: Hiyo sikumbuki.

Wakili: Anamuonyesha gazeti la Mtanzania, toleo namba 5229 la Jamatano, Septemba 8, 2010.

Shahidi: Anasoma kimya kimya

Wakili: Kichwa cha habari kinasemaje, soma kwa sauti.

Shahidi: Dk. Burian aweka mambo hadharani.

Wakili: Imeandikwa na nani?

Shahidi: Imeandikwa na waandishi wetu, Arusha na Dar.

Wakili Mughwai, anatewatetea walalamikaji  anasimama na kupinga maswali ya mahojiano hayo kuhusu taarifa za gazeti hilo.

Wakili Mughwai: Mheshimwa Jaji, shahidi anauliza maswali kuhusu ripoti iliyoandikwa na gazeti la Mtanzania la hiyo tarehe.

Shahidi aliyepo mbele yako sio mwandishi wa makala hiyo na wala sio mhariri, hivyo anaweza kuulizwa maswali juu ya maandishi aliyoyaandaa yeye mwenyewe kwa mujibu wa kifungu cha 64 (1) ya Sheria ya Ushahidi.

Pia alidai kuwa shahidi huyo hawezi kukumbushwa kuhusu taarifa ya gazeti hilo kuhusu ukweli wa taarifa hiyo na magazeti nchini baadhi yamekuwa na sifa ambayo sio mzuri kwa kupotosha mambo.

Akijibu pingamizi la wakili mwenzake, Kimomogoro alidai kuwa pingamizi hilo linafanana na pingamizi lililotolewa wakati shahidi wa nne, Salum Mpamba akihojiwa.

“Kimsingi, Jaji wakati wa kudodoswa,  shahidi anajiweka chini ya himaya ya mdodosaji isipokuwa tu pale mahakama itakapoona swali lipo nje ya shauri husika,” alidai Kimomogoro .

Aliendelea kudai kuwa kifungu namba 168 cha Sheria ya Uchaguzi hakihusiki katika cross examination, kinahusiana na examination – in- chief, mtu anaruhusiwa kujikumbusha kuhusu maandishi ambayo ameyaona au ameyafanyia kazi.

“Mheshimwa Jaji, maswali yanayokatazwa kwenye cross examination yametamkwa kwenye kifungu namba 160 cha Sheria ya Ushahidi,” alidai.

Baada ya majibizano hayo Jaji alitoa uamuzi akimtaka wakili Kimomogoro kuendelea kumhoji shahidi huyo kuhusu taarifa hizo za gazeti.

“Kwa kuuliza maswali ya aina hii yatasaidia kujua ukweli wa masuala hayo, hivyo, wakili Kimomogoro endelea kumhoji,” alisema Jaji Gabriel Rwakibarila.

Wakili Kimomogoro: Kulingana na taarifa hiyo, ni kweli masuala ya udini na ukabila yalikuwa yameanzishwa na baadhi ya wana-CCM?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili:  Ni kweli wewe hukupata taarifa ya chombo cho chote cha habari kilichoripoti hivi…haya maneno uliyomweleza Mheshimiwa Jaji?

Shahidi: Sina.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles