Monday May 2, 2016
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia
Badilisha Lugha KISWAHILI

Mholanzi amchapa vibao mwalimu mkuu

11th March 2012
Print
Comments

Raia mmoja wa Uholanzi, Marise Koch, anatuhumiwa kumfanyia kitendo cha udhalilishaji Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marera iliyopo kata ya Rhotia wilayani Karatu mkoani Arusha kwa kumpiga vibao mbele ya wanafunzi na walimu wenzake.

Taarifa ambazo NIPASHE Jumapili imezipata na kuthibitishwa na viongozi wa Idara ya Elimu wilaya ya Karatu na Jeshi la Polisi, ni kwamba kutokana na udhalilishaji uliofanywa, raia huyo ameshafunguliwa jalada lenye namba KRT/RB/835/2012 katika kituo cha polisi Karatu kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Marera, Emmanuel Ginwe, akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Karatu, alisema alipigwa vibao viwili na raia huyo wa Uholanzi ambaye ni mwanamke baada ya kuwakuta walimu wa shule hiyo wakipanga ratiba ya shule.

Ginwe alisema tukio hilo lililotokea Februari 14, mwaka huu majira 4:30 asubuhi ambapo raia huyo ambaye anaifadhili shule hiyo kwa kukarabati majengo ya shule, ofisi nyumba ya walimu na kompyuta ndogo za wanafunzi kufanyia michezo (games) na kujifunzia kuandika alifika shule hapo kutembelea kama kawaida.

Alisema Mholanzi huyo baada ya kufika shuleni hapo, alikuta walimu wakipanga ratiba ya shule na kuanza kuhoji kwanini walimu hawajaingia madarasani kufundisha wanafunzi madarasani ambapo alijibiwa kuwa wamepewa maelekezo ya kuandaa ratiba ya shule na baada ya kumaliza kazi hiyo wataingia madarasani kuendelea kufundisha.

Hata hivyo, majibu ya walimu hao hayakumridhisha ambapo Mholanzi huyo aliamua kwenda ofisini kwa Mwalimu Mkuu na kuanza kumfokea kwamba yeye (Mholanzi) anafadhili vitu vingi lakini kumbe walimu hawafundishi madarasani na kuanza kukusanya kompyuta zake ndogo (Exo-Laptop) kwa lengo la kuzichukua.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo hata hivyo alimsihi asichukue kompyuta hizo lakini alikataa na alipoona anazuiwa alimpiga vibao mwalimu huyo huku akiendelea kuzikusanya komputa akiwa na mwenzake ambapo kwa mara ya pili alimnasa vibao tena Mwalimu Mkuu huyo.

Kitendo cha Mwalimu Mkuu kupigwa vibao kiliwashitua walimu na wanafunzi wa shule hiyo ambapo walianza kuhoji kulikoni na walipoelezwa walisikitishwa na udhalilishaji uliofanywa na raia huyo wa Uholanzi kwa kutumia kigezo cha ufadhili kufanya udhalilishaji.

Ginwe alisema baada ya Mholanzi huyo kumfanyia udhalilishaji huo na kuchukua kompyuta zake 70 kati ya 93 zilizokuwepo na kuondoka zake, alikwenda kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji, kata na wilayani ambapo alishauriwa kufungua jalada la kesi katika kituo cha polisi.

“Nimedhalilishwa sana mbele ya walimu, wanafunzi na mke wangu ambaye ni mwalimu, tena mbele ya bendera ya Taifa iliyopo katika shule hii, namshukru Mungu wakati Mholanzi huyu ananipiga vibao japo ni mwanamke sikuweza kujibu mapigo,” alisema Ginwe.

Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilaya ya Karatu, Peter Simwanza, akizungumza na gazeti hili kuhusiana na tukio hilo, alisema kitendo alichofanyiwa Mwalimu Mkuu huyo ni cha kiudhalilishaji na kimedhalilisha taaluma ya ualimu na taifa kwa ujumla kwa sababu kimefanyika ndani ya ofisi ya mwalimu ambayo ni ya serikali.

Alisema CWT inataka kuona raia huyo wa Uholanzi anachukuliwa hatua kali za kisheria na vyombo vinavyohusika na kwamba chama hicho kitahakikisha kinamtafuta mwanasheria atakayemsimamia kesi ya Mwalimu Mkuu huyo ili haki iweze kutendeka.

Simwanza alisema baadhi ya wafadhili wanaosaidia katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani Karatu wamekuwa kero kubwa ambapo wamefikia hatua ya kuingilia utendaji wa maofisa wa elimu kiasi kwamba wanataka kuingiza mambo wanaoyataka wao ndiyo yafanyike kwenye mitaala ya elimu.

Hata hivyo taarifa ambazo gazeti hili imezipata ni kwamba raia huyo wa Uholanzi anajiandaa kuondoka nchini kwenda kwao baada ya kufanya udhalilishaji huo.

SOURCE: NIPASHE JUMAPILI
0 Comments | Be the first to comment

Articles

No articles