Wednesday Jun 19, 2013
| Text Size
[-]
[+]
Search IPPmedia

Dawa zilizoisha muda zaitia serikali hasara

4th April 2012
Print
Comments
Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo

Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini “madudu” katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, baada ya kubaini hasara ya Sh. bilioni 6.3 zilizotokana na kuharibiwa dawa zilizoisha muda wake wa matumizi pamoja na manunuzi ya vifaa hewa.

Madudu hayo yalibainika jana Jijini Dar es Salaam baada ya uongozi wa wizara ukiongozwa na Kaimu Katibu Mkuu wake, Regina Kikuli, kukutana na kamati hiyo ambayo ilikuwa ikipitia mahesabu ya fedha kwa mwaka 2010/2011.

Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alisema wabunge wenzake wameshtushwa na dawa za bilioni 4.7 kuharibiwa baada ya kuisha muda wake huku wananchi wanaozihitaji wakizikosa. “Hospitali zetu zipo hoi kutokana na kukosa dawa, lakini nyinyi vitabu vyenu vya mahesabu vinaonyesha kwamba mmeharibu dawa za mabilioni kutokana na kuisha muda wake kwa hili tunataka maelezo ya kina,” alihoji Cheyo.

Aidha, Kamati hiyo baada ya kupitia vitabu vya mahesabu vya wizara, ilibaini vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh. bilioni 1.6 havikupokelewa wizarani ambapo wabunge walihoji na kutaka kupatiwa majibu.

Wakati huo huo, Kamati hiyo jana iliambiwa kuwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), inadaiwa  Sh. bilioni 45 na taasisi mbalimbali zinazoshirikiana nayo katika kufanya kazi.

Kamati hiyo iliambiwa kuwa deni hilo limetokana na MSD kushindwa kulipa tozo kwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambao wanakagua ubora na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ambao wanakagua dawa hizo ili kujiridhisha kama zinafaa kwa matumizi.

Kaimu Katibu Mkuu Kikuli aliwaambia wabunge hao kuwa MSD imeelemewa na mzigo wa deni hilo na kwamba kila mwaka linazidi kuongezeka badala ya ya kupungua.

Hata hivyo, alisema kwa sasa wameweka mfumo wa kompyuta ambao unawawezesha kujua dawa zote zinazokaribia kuisha muda wake na hivyo kuzitoa kwa haraka ili serikali isipate tena hasara.

Kuhusu ufanisi na kurahisisha utendaji wa kazi za  wizara, alisema wamenunua magari saba yenye thamani ya Sh. bilioni 1.6 likiwemo la Waziri.

SOURCE: NIPASHE
0 Comments | Be the first to comment